Dar es Salaam.
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Jumatatu tarehe 6, Septemba 2021, inatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na Ugaidi.
Mbowe na wenzake wanapinga hati ya mashtaka yanayowakabili wakidai kuwa ina kasoro za kisheria na hivyo wanaiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali
Katika pingamizi hilo pamoja na mambo mengine wakidai kuwa Sheria ya Ugaidi ambayo wanashtakiwa nayo haijafafanua viambato vya kosa la Ugaidi na kwamba upande wa mashtaka haujazingatia masharti ya lazima ya sheria hiyo ambayo ni kueleza kusudio la vitendo vya ugaidi ambavyo washtakiwa wanatuhumiwa kuvitenda
Hata hivyo mawakili wa Serikali wanaoongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Robert Kidando, wamepinga vikali pingamizi hilo wakidai kuwa hoja zao hazina mashiko.
Wamedai kuwa hati ya mashtaka iko sahihi na haina kasoro hizo zinazodaiwa na kwamba hati ya mashtaka imekidhi matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ambazo zinawawezesha washtakiwa kufahamu makosa wanayoshtakiwa.
Hivyo, wameiomba mahakama ilitupilie mbali pingamizi hilo ili kesi hiyo iendelee kusikilizwa katika hatua ya awali.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote Jaji Ekinaza Luvanda amesema atatoa uamuzi wa pingamizi hilo la washtakiwa Jumatatu.
Serikali inawakilishwa na timu ya mawakili wa Serikali watano huku upande wa utetezi ukiwa na mawakili zaidi ya 14 wakiongozwa na Peter Kibatala.
Washtakiwa wa kwanza Halfan Bwire Hassan, wa pili Adamu Hassan Kasekwa, wa tatu Mohamed Abdillahi Ling'wenya na wa nne Freeman Aikael Mbowe.
Chanzo: Mwananchi