Mahakama yamtaka IGP Kanja ajieleze kuhusu alipo Twaha, Polisi wasisitiza hayuko mikononi mwao

Ikariiah

JF-Expert Member
Joined
Jul 17, 2019
Posts
287
Reaction score
314
Your browser is not able to display this video.
Jaji wa Mahakama Kuu Alexander Muteti amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kujitokeza binafsi kueleza kinachoendelea kuhusu kupotea kwa mwanaharakati Mtanzania Twaha Mwaipaya, ambaye aliripotiwa kutoweka Oktoba 25, 2026, eneo la Kamulu, Kaunti ya Machakos.

Katika kesi ya maombi ya Habeas Corpus inayotaka Mwaipaya afikishwe Mahakamani au mamlaka zieleze alipo, Wakili wa Serikali, Christopher Marwa, aliiambia Mahakama kuwa uchunguzi kuhusu kutoweka kwake ulianza Oktoba 26, siku moja baada ya tukio kuripotiwa.

Marwa alisema Polisi wamewasiliana na kampuni za mawasiliano za Safaricom na Airtel pamoja na kampuni ya Bolt ili kupata taarifa zinazoweza kusaidia kumtafuta Mwaipaya. Aliongeza kuwa baadhi ya mashahidi wamehojiwa na kutoa taarifa, akiwemo James Gatunyi, ambaye alikuwa mwenyeji wa Mwaipaya.

Hata hivyo, alisema bado hawajapokea majibu kutoka kwa Safaricom na Airtel, hivyo wanaomba muda zaidi kuwasilisha kiapo rasmi kinachoeleza hatua za uchunguzi. Serikali pia iliiambia Mahakama kuwa Mwaipaya hayuko chini ya ulinzi au mikononi mwa vyombo vya dola.

Kauli hizo zimepingwa na Wakili Mkuu Martha Karua, aliyesema kuwa agizo la awali la mahakama halijatekelezwa kwa kuwa Mwaipaya hajafikishwa mahakamani wala mamlaka hazijaeleza mahali alipo.

Karua alihoji kwa nini polisi wanasema uchunguzi ulianza baada ya kuwasilishwa kwa maombi ya Habeas Corpus, ilhali taarifa za kutoweka kwa Mwaipaya zilikuwa tayari zimeripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi. Alisisitiza kuwa jukumu la polisi ni kulinda usalama wa watu na kwamba hawapaswi kusubiri amri ya mahakama ndipo waanze kutafuta mtu aliyeripotiwa kutoweka.

Wakili huyo pia alionya kuhusu visa vingine vya watu waliotoweka na baadayle kupatikana wakiwa wamefariki, wengine kuachwa kando ya barabara, huku wengine wakikosekana kabisa. Alitaka Inspekta Jenerali Kanja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wajitokeze wenyewe mbele ya Mahakama na kueleza hatua zilizochukuliwa.

Kwa upande wa DCI na Inspekta Jenerali, maafisa waandamizi wa sheria na polisi waliwasilishwa mahakamani kuwakilisha taasisi hizo. Hata hivyo, Karua alisisitiza kuwa wawakilishi hao hawatoshi kujibu maswali kuhusu kutotekelezwa kwa maagizo ya Mahakama na alitaka wakuu hao wawili wajieleze binafsi.

Soma Pia: Kenya: Mahakama Kuu, Kaunti ya Nairobi yaamuru Polisi kumrejesha Twaha Mwaipaya akiwa hai au amefariki

Katika hoja zake, Wakili Abner Mango, anayewakilisha upande unaotafuta haki kwa niaba ya Mwaipaya, alisema suala hilo linahusu madai ya kukamatwa kinyume cha sheria, kuzuiliwa na kushikiliwa bila mawasiliano na watu wengine. Alisema Mwaipaya na wageni wengine wanaotafuta hifadhi ya kisiasa wanastahili kulindwa na sheria, huku akisisitiza kuwa umma unahitaji majibu kuhusu alipo mwanaharakati huyo.

Kesi hiyo inaendelea kuibua maswali kuhusu hatua zilizochukuliwa na vyombo vya usalama tangu Mwaipaya aliporipotiwa kutoweka. Hadi sasa, kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na upande wa Serikali mahakamani, hakuna uthibitisho kwamba amepatikana au yuko chini ya ulinzi wa Polisi.

Je, maelezo ya Polisi kuhusu uchunguzi unaoendelea yanatosha au ni wakati Inspekta Jenerali na mkuu wa DCI wajitokeze wenyewe kutoa majibu kuhusu alipo Twaha Mwaipaya?
 

Attachments

  • 4141.jpeg
    61.6 KB · Views: 7
  • 4132.jpeg
    52 KB · Views: 6
  • 4135.jpeg
    146.9 KB · Views: 6
  • 4134.jpeg
    131.1 KB · Views: 7
Polisi wanajua alipo Twaha, sema kwasababu wana ushirikiano wa moja kwa moja na wasiojulikana, ndio maana wanakataa.

Polisi wanakana kwasababu kwa sasa maboss wao wasiojulikana bado wanamshikilia Twaha, ila ikitokea wasiojulikana wakamalizana na Twaha, hapo ndipo polisi wataambiwa mchukueni huyo hapo.

Baada ya hapo ndio polisi watakuja na taarifa zao za wanae kwa mahojiano wakimtuhumu kwa kosa fulani, uchunguzi ukikamilika watamfikisha mahakamani.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…