Wana JF haya ni malamiko niliyadokoa sehemu ya wakazi wa ukonga ambako MAKONGORO ndie mbunge wao, hivi hata pesa za kuweka mafuta greda la manispaa hakuna? Pesa wanazokusanya ushuru ktk maziziz wanapeleka wapi? sehemu ya dakika 5 unatembea nusu saa, si diwani si mbunge anaejali,ama kweli CCM ina wenyewe
TUNAMUOMBA MUNGU AWAPE MIOYO YA HURUMA VIONGOZI WA MANISPAA YA ILALA na MAHANGA.
Ninaandika kwako kutoa dukuduku langu kwa viongozi wetu wa Manispaa ya Ilala. Mimi ni mmoja wapo wa wakazi wa Ukonga Mombasa.
Ni muda mrefu sana tumekua na kilio cha ubovu wa barabara yetu ambayo kwa muda mrefu imeachwa kama motto yatima wakati barabara nyingine pacha kama za Kitunda na Kinyelezi aidha zimetengenezwa kwa kiasi Fulani cha lami au zimekua zikichongwa na kuwekewa vifusi mara kwa mara.
Tunamuomba Mwenyeezi Mungu awape mioyo ya huruma viongozi wetu watukufu nikianzia na Katibu mtendaji wa kata, Diwani, Meya, Mbunge, Mkurugenzi wa Manispaa, Mhandisi wa Manispaa na viongozi wote wanaohusika katika ufatiliaji na ukarabati wa barabara husika.
Hivi ni kweli hata kupitisha tingatinga inashindikana? Ni vipi wananchi hatuelezwi hatua yeyote kuhusiana na ukarabati wa barabara hiyo? Chakusikitisha ni kwamba mnamo tarehe 02 mwezi wa Tisa 2007 walikuja watumishi wa Kampuni ya ujenzi ya KAJIMA na kijiko cha kuchimbia mashimo ambacho walitumia kukwangulia barabara kipande cha urefu meta takiribani mia na hamsini tu na hakuna kilichofanyika zaidi ya kuzidi kuiharibu, au waliku wana msafishia njia Mheshimiwa mmoja Mtumishi wa Wizara ya Miundo mbinu ambae anakaa meta chache kutoka barabara kubwa? Hii sio rushwa?
Ni kweli bajeti ya kukarabati barabara hii ya ukonga mazizini haijatengewa pesa kwa kipindi cha miaka mitano sasa? Naona umefika wakati kwa wazee wa TAKUKURU watutetee wanyonge sie walau kwa kwenda kuchungulia na kukagua vitabu vya mahesabu ya Manispaa ya Ilala kujua kama kweli bajeti ya barabara hiyo haijatengwa, na iweje itengwe ya kukarabati kinyelezi mara kwa mara na huku isiwepo wakati wote tupo jimbo moja, ama ni kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ndiko kwenye makazi yake? Na kama kuna mis allocation of fund, tunaomba tuelezwe ni vipi pesa hizo zipelekwe katika sehemu nyingine ilihali nasie ni walipa kodi na tuna hitaji kugawana hako ka SUNGURA kwa kuletewa maendeleo.
Kwa kifupi barabara hii ni moja wapo ya barabara ambazo waheshimiwa hao naona wanampango wa kuja kuigeuza shamba la migomba, haya na waje maana mashimo yapo ya kutosha. Ni mwaka umepita sasa tokea Mheshimiwa Makongoro Mahanga (MB) alipotamka ya kuwa barabara hiyo itatengenezwa karibuni. Tunakuomba Mheshimiwa uachane na ziara za Mikoani kwenye zomeazomea na uje walau uone kwa macho yako na utueleze kinachoendelea kwa watendaji wako.
Tulipokea habari hizo kwa shingo upande kwani si maneno ya leo huwa mara kwa mara tunaambiwa vivyo, pamoja na hayo cha kujiuliza hivi ni kweli barabara hiyo haijapangiwa pesa ya kukarabatiwa kwa mwaka wa tano sasa? Cha aibu ni pale mwaka juzi kipindi cha kampeni waheshimiwa hao walikwenda Uwanja wa ndege na kuchukua lami iliyotolewa katika barabara ya kukimbilia ndege na kuja kuiweka katika maeneo machache hata hivyo ni aibu kwani walichofanya ni kama wamechukua limao na kusafishia shaba katu haiwi dhahabu. Diwani wetu upo wapi?Meya wa Manispaa ya Ilala upo wapi? Ahadi zenu tamtam zipo wapi?Tumechoka kutoa pesa za kusomesha watoto kwa kutengeneza magari.
Hivi ni kweli hakuna hata greda la kuja kuchonga hii barabara wakati tukisubiri hayo matengenezo makubwa? Mbona ya kuvunja vibanda vya walalahoi yapo?hata mgonjwa wakati anasubiri upasuaji mkubwa hupewa panadol ili apunguziwe maumivu.
Namalizia tena kumuomba bwana Mungu alie hai awape mioyo ya huruma na mtutengenezee barabara hiyo.