Kumekuwa na shutuma za mara kwa mara kuwa una ukaribu uliokithiri na Chama kuu pinzani kwa CHADEMA yaani CCM. Unasemaje kuhusiana na tuhuma hizo?
Ukitaka kummaliza mwanasiasa yeyote wa upinzani hapa Tanzania mhusishe na ama usalama wa Taifa au CCM. Ndivyo ilivyokuwa kwa Mabere Marando miaka ya Tisini. Marando ameishi kuweka sawa historia ingawa propaganda dhidi yake zilikuwa kali sana kiasi cha kuogopwa kweli kweli. Napita njia hiyo hiyo ya Marando na wanaonipaka matope haya wataona aibu sana ukweli utakapodhihiri.
Siku za mwisho za uhai wake ndugu Chacha Wangwe naye aliambiwa ni CCM na kwa kweli alikufa akiwa na chuki sana kuhusu tuhuma hii.
Faida kubwa niliyonayo mimi ni kwamba, mtaji wangu wa kisiasa ulikuwa ni mkubwa mno na ndio maana tuhuma hizi hazijaniathiri. Ninaamini tuhuma kama hizi zingekuwa kwa watu wengine wangekuwa wameshafutika kwenye historia ya siasa. Sijawahi kuwa mwanaCCM, familia yangu yote kabisa ni waanzilishi wa CHADEMA. Sina historia na CCM. Inawezekana wanaosema mimi ni CCM wengi wao wamewahi kuwa CCM, wana familia zao ndani ya CCM na wamewahi kula matunda ya CCM. Mimi sijawahi na wala sitawahi.
Inasemekana kua ukaribu huo unaweza kuonekana kupitia ukaribu wako na Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni rais wa Jamhuri wa muungano wa Tanzania, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Unasemaje hapa?
Kuhusu Rais Kikwete, kwanza ifahamike Jakaya Kikwete na Zitto Kabwe wana mahusiano yao nje ya siasa na hata siku moja hatujadili vyama vyetu. Rais Kikwete anaamini katika uzalendo wangu.
Mimi ninamheshimu Rais Kikwete kama Mzee wangu. Kuita sisi ni marafiki is understatement, yeye ni mzee wangu. Tunaheshimiana, lakini ninaiheshimu zaidi Tanzania na ninaipenda zaidi Tanzania. Kama inavyoonekana, kazi zangu zinajihidhirisha Bungeni kwamba ni mmoja wa wabunge ninayeisumbua sana Serikali yake. Kutokana na hoja zangu nimemlazimisha kufanya mambo kinyume na mipango yao. Leo tuna sheria mpya ya Madini kwa sababu ya hoja ya Buzwagi. Ninafurahi sasa mgodi wa TanzaniteOne hisa asilimia 50 zinachukuliwa na Watanzania kutokana na mapendekezo yangu mahususi kwamba vito vya thamani, mgeni asiwe na zaidi ya asilimia 50.
Mwaka huu nimemlazimisha kupangua baraza la mawaziri kufuatia hoja yangu ya kutokuwa na imani na waziri mkuu iliyoungwa mkono na wabunge wengi bila kujali vyama. Hebu niambie kama ningeweza kupata mafanikio kama haya dhidi ya Serikali ya mtu mnayesema rafiki yangu. Wengine watasema, aah JK huwa anamtuma kufanya haya. Iwe jua au mvua ni lawama tu. Lakini maisha ya kisiasa haya. Yana mwisho, Rashidi wa KULI alisema.
Mkuu, vipi kuhusu kuonekana kwako in public pamoja na rais sehemu tofauti hadi safari za nje ya nchi.
Suala la kusafiri na Rais ni suala la kawaida sana. Nashangaa sana namna linavyokuzwa wakati ni wazi kabisa kua Rais lazima asafiri na wabunge, na anae wateua wabunge ni Spika wa Bunge. Kila Rais, Makamu wa Rais au Waziri mkuu wanapo safiri huambatana na wabunge wa kambi zote mbili.
Kwa kuweka rekodi sawa Rais amesha safiri na wabunge wafuatao wa Chadema: Christina Lissu (Australia), Chiku Abwao (Burundi), Grace Kiweli (Scandinavia), Lucie Owenya (US), nk. Makamu wa Rais kesha safiri na Ezekiah Wenje (Uturuki) na Esther Matiko (Uturuki) Waziri Mkuu pia kesha safiri na wabunge wa Chadema.
Toka nimekuwa mbunge nimesafiri na Rais mara mbili tu: Mara ya kwanza ilikua sherehe za uhuru za Sudan Kusini. Nilikwenda kwa taratibu hizo za Bunge. Mara ya pili ni Ethiopia, Kumzika Meles Zenawi. Hii niliomba mwenyewe kwani nilipenda kwenda kumzika mwanasiasa huyu niliekuwa namheshimu sana barani Afrika.
Inasemekana kuwa ni Kwa sababu yako ndio maana rais JK hakumnadi mgombea wa ubunge wa CCM wa jimbo lako katika uchaguzi mkuu uliopita na kwamba ndio maana hukushiriki katika kuungana na wanachama wako katika kumsusia JK siku ile anafungia bunge.
Rais Kikwete hakufika jimboni kwangu kumnadi mgombea wa chama chake. Napenda niwakumbushe, sio mwaka 2010 tu, toka nimekuwa mbunge Rais Kikwete hajawahi kuja kwenye kampeni jimboni kwangu. Hakuna makubaliano yeyote, bali anaheshimu mchango wangu kwenye nchi yangu. Mwaka 2005 hakuja Kigoma Kaskazini. Mwaka 2010 hakuja Kigoma Kaskazini. Lipumba pia hakuja Kigoma Kaskazini kunadi mgombea wake wa CUF.
Mwaka 2005 katika Jimbo la Musoma Mjini, aliyekuwa mgombea Urais CHADEMA ndugu Mbowe, hakumnadi mgombea wa CHADEMA bali alimnadi mgombea wa CUF. Mwaka 2010 Slaa alipofika Kyela alimnadi mgombea wa CCM dkt Mwakyembe. Kama ilivyo kwa wengine wenye maamuzi ya kuthamini kazi za wagombea wa vyama vingine, Rais Kikwete naye anayo haki ya kuheshimu na kuthamini kazi zangu katika nchi yetu. Mwakyembe yupo kwenye majukwaa ya CCM licha ya kwamba alinadiwa na Mgombea Urais wa CHADEMA.
Vipi madai kuwa unatumwa na CCM ili kupunguza nguvu ya CHADEMA? Kama si kweli unadhani kwanini watu wanakuona kama pandikizi ndani ya CHADEMA?
Baadhi ya watu wanapandikiza chuki hizi kwa sababu zao wenyewe. Hawanisumbui maana najua ni kikundi kidogo cha watu wachache wenye malengo yao ovu. Wajue tu kwamba hawawezi kuwadanganya Watanzania ambao wanafanya maamuzi yao sio tokana na propaganda ila kutokana na matendo ya kila mmoja.
Onyo: Watu hao hawawezi kummaliza Zitto kisiasa bila kuiathiri CHADEMA maana the imaage of Zitto is so intimately intertwined with CHADEMA that you couldn't attack Zitto without jeopardizing the image of Chadema, and vice versa.
Wanaoeneza sumu hii hawana nia njema wala mapenzi na CHADEMA. Hawaelewi siasa. Wanafurahisha maadui wa CHADEMA. Maadui wanawachochea kwa kuwapa habari za uwongo na wao wanadhani watammaliza Zitto. Huwezi kummaliza Zitto bila kuiathiri CHADEMA. Hawatafanikiwa.
Ni kweli kuwa una mkakati wa kuhamia CCM kabla ya 2015?
Sijawahi wala kufikiria kuhamia CCM. Kama nilivyosema hapo awali, sijawahi kuwa mwanachama wa chama kingine chochote tofauti na CHADEMA. Namwomba mungu kuwa niondoke duniani nikiwa chama hiki hiki. Siamini katika kuhama vyama. Ninaamini katika mfumo imara wa vyama vingi nchini. Ninaamini katika demokrasia pana.
Vipi tetesi kuwa wewe na Kafulila mmeanzisha chama na una mkakati wa kutimkia huko?
Swali hili na lililotangulia yanaonyesha kuwa hizi kweli ni tetesi tu. Sasa kama unasema nina mkakati wa kuhamia CCM. Tena kuna tetesi nimeanzisha chama na nataka kuhamia huko, sasa mimi nina vyama vingapi nitakavyohamia. Sijawahi hata kufikiria kuanzisha chama cha siasa. Chama changu ni CHADEMA na sitaondoka CHADEMA. Kinachonisikitisha ni kwamba kuna viongozi wa CHADEMA wamekula sumu hii na bila woga wanaisema kana kwamba ni kweli.
It is very unfortunate Kiongozi wa chama makini kama CHADEMA kuamini ujinga na kuingia kwenye mitego kama hii. Nataka ijulikane wazi kabisa kwamba, CCM haitachoka kutugawa. Haitachoka kupandikiza chuki miongoni mwetu. Wameshajua udhaifu upo wapi na wahenga walisema kamba hukatikia?