SoC02 Maisha ni Safari

SoC02 Maisha ni Safari

Stories of Change - 2022 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Joined
Jun 3, 2021
Posts
609
Reaction score
604
Nilipohitimu shahada yangu ya kwanza ya elimu mwezi wa saba mwaka 2014 kule Mtwara kwenye chuo cha STAMUCO nikaamua kurejea nyumbani Dar-es-Salaam, nikaona nisibweteke na kungojea ajira za Serikali, nikaamua kujiunga na shughuli za hapa na pale angalau niwe napata hata fedha za kuweza kununua vocha, hivyo nikawa fundi simu pale Kariakoo mtaa wa Aggrey kwenye ofisi ya kaka wa rafiki yangu mmoja niliyesoma naye sekondari.

Ujanja ujanja wangu ukanisaidia kuvielewa baadhi ya vitu na haikuchukua muda mrefu nikaweza kutamani ufundi wa simu hasa simu janja zilizoenea siku hizi.

Kila kazi huwa ina changamoto zake, kama zilivyo kazi zingine.

Pamoja na kunipatia kiasi kidogo cha kuniwezesha kupata mlo wa siku lakini changamoto kubwa ambayo ilikuwa ikinipa shida ni uongo. Mimi sikuwa muumini wa kusema uongo, sasa hili lilinitofautisha sana na mafundi wenzangu wa pale Aggrey. Hivyo wateja wakavutika na ile tabia yangu ikawa kila wakija wananiulizia mimi na hawakutaka simu kutengenezewa na yeyote isipokuwa mimi. Hili hawakulipenda baadhi ya mafundi wenzangu.

Yote tisa kumi ni mambo ya wanawake, fundi simu usipokuwa makini utakuwa unabadili wasichana kila siku hasa katika zama hizi ambazo fedha imekuwa shida kidogo wasichana wengi wamekuwa rahisi sana.

Hili liliniogopesha nisije nikaingia kwenye majanga mengine nisiyoyatarajia. Mimi niliona ishara ya haya, ili nisiharibu ndoto zangu nikaona ni vema nibadili kazi ya kufanya, vinginevyo ufundi simu utaniletea maafa hasa kutokana na vitimbii vya wale wasichana. Nilikuwa fundi simu kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.

Wakati nipo pale Aggrey nilisoma kozi ya udereva miezi mitatu veta ya Chang’ombe. Nikafanikiwa kupata leseni ya kuendesha magari madogo na ya kati.

Nilipoacha ufundi simu nikaona ngoja nijaribu bahati kwenye kazi ya udereva. Kwa bahati nikapata gari daladala ruti ya Kariakoo-Masaki. Ulikuwa mwaka 2016 huo miezi ya mwanzoni, nilifanya kazi ile kwa bidii sana. Kwanza nilijitahidi kuwa msafi ili niwe dereva wa kupigiwa mfano. Kitu ambacho nilijitahidi ni kujiwekea upekee wa huduma hasa kwenye usafi wa gari.

Hata hivyo niliona udereva wa daladala hauna maslahi hasa nikilinganisha na ile kazi ya ufundi simu. Nafsi yangu ilinishauri niendelee kuwa na subira huenda mambo yakabadilika huko mbeleni. Lakini mambo halizidi kuwa vilevile, posho ilikuwa ndogo kiasi sikuweza hata kuwa na akiba. Nilifanya kazi ile kwa miezi nane tu kisha nikaamua niiache kwa ridhaa yangu mwenyewe.

Ingawa kuna mjomba wangu mmoja alikuwa ananihamasisha sana niingie kwenye mambo ya siasa. Hivyo nilipomwambia kuwa nimeacha kazi ya udereva akaniunganishia mipango nikapata kadi ya chama chapchap na kuniambia kuwa natakiwa nianze harakati za chama kule Mbagala.

Kwa kuwa nilikuwa na shahada yangu nikapewa cheo cha ukatibu wa vijana wa chama tawala tarafa fulani hapa mjini. Kipindi hiki kila mtu alitamani ajiunge kwenye chama maana ilionekana huko ndiko kwenye ulaji. Kuwa mwanasiasa kunahitaji moyo mgumu sana, uwe mvumilivu kwelikweli vinginevyo asubuhi tu unarudisha kadi. Ilinilazimu niwe kada ndindindi wa chama ili nile na wakubwa, na mimi sikufanya ajizi.

Nilitoa juhudi zote na muda wangu wote kukitumikia chama. Hapo ndipo nilipata kukutana na viongozi wengi wa chama na serikali, hata hivyo sikuweza kupata mwanya wa kupata teuzi za mbele mbele ijapokuwa nilijipendekeza sana.

Kilichonifanya niwaze kuachana na siasa ni mambo ya mazingara na mambo fulani fulani ya Pwani. Unajua kwenye siasa hayo mambo huwezi kuyaepuka, unalazimika tu uingie ili ufanikishe unachokitaka. Sasa mimi imani yangu haikuwa yenye kuamini hayo mambo, hivyo nilipatwa na sokomoko kubwa la moyo nikawa na mgogoro binafsi. Na yale mambo ya kila siku vikao vya kumjadili fulani na fulani vilichochea kwa kiasi kikubwa.

Kipindi hicho ilikuwa ndicho kipindi cha kujiandaa na uchaguzi mkuu mwaka unaofuata kwa hiyo hekaheka haziishi maofisini. Ingawa nilikuwa na mawazo sana lakini niliendelea kujikaza huku nikijipa moyo huenda kwenye uchaguzi mkuu nitapewa nafasi pahala. La haula! Hakuna cha teuzi wala nini nilishangaa watu wanateuliwa tu na kupewa nafasi. Mwisho wa siku nikakata kauli na kunawa ukada wa chama nikarudi kujipanga tena.

Kipindi nipo kada wa chama nilifanikiwa kununua pikipiki mbili nikazitumia kufanya bodaboda. Na nikapata fremu moja pale Tandika sokoni nikamuweka kijana mmoja anauza simu ndogondogo za kichina. Nikawa nasimamia miradi yangu hii, ili maisha yasiende fyongo nikaamua kwenda shamba huko Mkuranga nikapata shamba la hekari kumi tu la kukodi, nikalima mananasi na mihogo.

Kuhakikisha usimamizi na mimi nikahamia shambani, nimekaa huko miaka miwili mjini nikawa nakuja mara moja moja. Kama unataka mali utaipata shambani. Misimu yote miwili ya shambani sikuambulia kitu, mazao yalikuwa ya kawaida tu sikuweza kutoka kupitia kilimo kwa misimu hiyo miwili.

Nikaona nitamaliza umri na mafanikio nitayasikia tu kwa wasanii. Sikutaka niendelee kukaa shamba kwani nilianza kuona mabadiliko sio ya mwili tu hata fikra zangu zikawa zinadidimia. Hivyo nikarudisha majeshi mjini tena kuja kuendeleza mapambano.

Niliporudi nikachukua pikipiki yangu moja nikafanya kazi ya bodaboda huku nikisuka mipango ya kutafuta kazi ya kudumu. Kituo changu cha kazi kikawa Kariakoo. Mafundi wenzangu wa zamani walinitumia sana kusafirisha mizigo yao kuipeleka kituo cha mabasi Ubungo, Temeke na mara nyingine hata Mbagala hasa walipotaka kuisafirisha mizigo hiyo mikoni.

Ubodaboda ulinipa kipato, niliona pesa ikikaa angalau ingawa sikufanya kwa muda mrefu kwani baadaye nilipata kazi ofisi moja ya wahindi kule posta kama msimamizi wa vibarua wa kampuni. Hapo sasa maisha yakawa nafuu. Wahindi wa pale walinikubali sana kwa utendaji kazi wangu uliotukuka.

Wakati huo sasa ndio nikakutana na rafiki yangu Dotto C. Rangimoto ambaye aliniambia kuwa nina kipaji cha uandishi hivyo nikiendeleze, akawa ananipa baadhi ya miongozo katika uandishi. Kweli nami nikaanza kuandika hadithi fupi, riwaya na hata mashairi ya Kiswahili. Kadiri miaka ilivyozidi kusonga na mimi nikawa napata uzoefu katika uandishi.

Pale kazini kuna jamaa mmoja namuhifadhi kwa jina, maana ni maarufu sana hapa mjini. Akaanza kunifanyia majungu, alitamani nafasi na cheo nilichopewa. Hivyo alitumia kila njia na hila ili mimi nionekane sifai, mwisho wa siku nikatakiwa kwenda kozi.

Nikawa sina budi isipokuwa niende Arusha kwenye kozi maalumu ya uongozi miezi sita. Kumbe ule ulikuwa ni mpango wa siri uliofanywa na mwana wa bosi na huyo jamaa ili mimi nikitoka jamaa achukue nafasi yangu. Kweli, nilipotoka kwenda kozi yule jamaa akapewa ile nafasi aikaimu kipindi mimi nipo nje ya ofisi.
 
Upvote 5
Back
Top Bottom