BAADA ya viongozi wa asasi za kiraia (NGOs) kutajwa katika nafasi ya chini miongoni mwa makundi za wananchi wanaoaminiwa katika jamii, asasi wanazoziongoza zimeshutumiwa kwa kuwanufaisha watu binafsi zaidi ya jamii ambayo ndiyo chimbuko lake.
Utafiti uliofanywa na asasi ya kiraia ya Foundation For Civil Society kuhusu maoni ya umma juu ya asasi za kiraia Tanzania kwa mwaka 2009, umebaini kuwa sehemu kubwa ya wananchi wanazilaumu asasi hizo kwa kuwatajirisha watu binafsi zaidi ya jamii.
Shutuma hizo zimetolewa na jamii ya watu wanaozunguka miradi ya maendeleo ya asasi hizo walipotakiwa kuelezea mambo wanayoyachukia kuhusu asasi hizo.
Katika utafiti huo, watu 800 kwa kuzingatia jinsia kutoka mikoa minane iliyowakilisha kanda nane za Tanzania na Zanzibar, walihojiwa kwa njia ya ana kwa ana kwa dakika 20 kwa kila mwanajamii.
Kabla ya utafiti huo, utafiti mwingine uliofanyika mwaka 2007 kwa kuhoji jumla ya Watanzania 7,879 kuhusu makundi ya watu wanaoaminika sana na jamii, kati ya makundi 18 ya jamii yaliyotajwa kuaminiwa, viongozi wa asasi hizo walitajwa katika nafasi ya 13.
Walioongoza kwa kuaminiwa zaidi na Watanzania ni ndugu zao wa familia wakifuatiwa na viongozi wa dini, ndugu wa ukoo, walimu, watu wa kabila moja, wazee wa kike, wazee wa kiume, wenyeviti wa vijiji na kata, madaktari na wauguzi na viongozi wa mitaa huku vijana wa kiume na wageni wasio Watanzania wakishika nafasi za 17 na 18 ambazo ni za mwisho.
Utafiti huo wa mwaka 2007 uliofanywa na Asasi ya Utafuti wa Kuondoa Umasikini (Repoa), ambao ulikuwa moja ya tathimini za utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (Mkukuta), ulionesha pia kuwa wanasiasa walishika nafasi ya 11, wafanyabiashara 12 na polisi nafasi ya kumi na tatu.
Licha ya asasi hizo kushutumiwa kwa kuwatajirisha watu binafsi zaidi ya jamii, wananchi hao waliohojiwa katika utafiti wa Foundation For Civil Society pia walisema wanachukizwa na kukosekana kwa muundo sahihi wa menejimenti katika asasi hizo.
Baadhi ya mambo mengine yaliyolalamikiwa ni kukosa uwajibikaji katika fedha za miradi, hazishirikishi jamii katika mipango yao, kutawaliwa na tabaka la wasomi na kujali viongozi zaidi ya jamii.
Licha ya wanajamii wanaozunguka miradi ya asasi hizo, pia wadau wa asasi hizo wakiwemo maofisa wa serikali kutoka kiongozi wa kata, mabaraza na shehia mpaka mawaziri, vyombo vya habari, taasisi za elimu ya juu, jumuiya ya wafanyabiashara na wabia wa maendeleo walipohojiwa walitoa maelezo yanayofanana na ya jamii hizo.
Wadau hao walisema asasi hizo haziwajibiki katika fedha za miradi, zimekosa muundo sahihi wa menejimenti, zinawatajirisha watu binafsi zaidi ya jamii na haziwahusishi wanajamii katika mipango yao.
Hata hivyo, jamii hiyo na wadau walipoulizwa kama bado asasi hizo zina umuhimu katika jamii, asilimia 94 ya wadau walisema zina umuhimu na asilimia 81 ya wanajamii pia walisema zina manufaa kwao.
Walipotakiwa kueleza sekta ambazo asasi hizo zimeshindwa, sekta ya kilimo ilitajwa kuwa inayoongoza kutoshughulikiwa na asasi hizo ikifuatiwa na mazingira, utawala bora, maji safi na afya ya akina mama.
Sekta ambazo asasi hizo zimefanikiwa sana ni mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya Ukimwi, elimu, kutunza yatima na makundi ya pembezoni.
Kutokana na udhaifu huo baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa katika utafiti huo ni pamoja na asasi hizo kutakiwa kuweka msukumo katika miradi ya kilimo kwa kuwa Watanzania wengi wanajihusisha nacho na kwenye mazingira na maji safi.
Aidha zimeshauriwa kutengeneza mkakati wa mawasiliano ulio dhahiri ili kupunguza hisia kwamba zinakosa uwazi, uwajibikaji na zina wafujaji.
Pia zimeshauriwa kuwajibika kwa watu kwa kuwa wao ndio wanaowafanyia kazi, kwa wafadhili kuhalalisha walichokifanya na sababu zake na kwa serikali kwa kuwa ni mdau mwenye maslahi katika utoaji wa huduma kwa umma.