NINATOAKA WAPI?
Hili ni swali la pili la msingi. Watu wengi wamejaribu kutafuta jibu la swali hili, hata wengine wakabuni kuwa BinAdamu alitokea ghafla tu kwa bahati nasibu. Hii ni sababu ambayo kwa kweli haina msingi wa kiakili, kwa sababu ikiwa hata utando wa buibui hauwezi kutokea kwa bahati nasibu, iweje binadamu na mpangilio wake wa kimaumbile atokee kwa bahati nasibu?
Wengine wanatoa hoja kuwa mtu alianza kuwa nyani na ndipo akabadilika taratibu hadi akawa mtu. Hata hivyo hadi leo wanaotoa maelezo haya wameshindwa kutoa uhakika wake kwani hadi leo manyani ni manyani na watu ni watu tu, hakuna kiumbe aliyewahi kuonekana popote duniani hivi karibuni ambaye nusu ni nyani na nusu ni mtu, akiwa bado yumo kwenye hayo mabadiliko.
Sisi Waislamu tunasema kuwa hakuna Binadamu ambaye ataweza kutuambia sisi asili yetu ni nini, au tunatoka wapi kinyume na anavyotueleza yule aliyetuumba. Watu wote ni wageni tu katika dunia hii, hivyo mtu hawezi akajifanya yeye ni mwenyeji sana kiasi cha kujua asili ya watu wakati na yeye kajikuta tu duniani kama sisi.
Hivyo ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayeweza na ndiye mwenye haki ya kutuambia sisi tunatoka wapi na asili yetu ni nini, na ndiye anayetuambia:-
"Hakika ulimpitia Binaadamu wakati mrefu katika dahari hakuwa kitu kinachotajwa."
(Q 76:1).
Aya hii inatuambia kuwa kuna wakati, tena mrefu mno, ambapo Mwanaadamu hakuwepo kabisa. Hivyo ni wazi kuwa alikuwa na mwanzo. Kuhusu mwanzo huu Mwenyezi Mungu anatuambia:-
"Na (kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika, 'Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo mkavu unaotoa sauti, wenye kutokana na matope meusi yaliyovunda!"
(Q 15:28).
Aya hii inatupasha habari ya kuumbwa kwa mtu. Baada ya kupita muda mrefu bila ya kuwepo duniani, mtu aliumbwa kwa udongo.
Pengine mtu anaweza kubishia maelezo haya ya Muumba kuwa mtu aliumbwa kwa udongo, maana inaweza kuwa vigumu kwake kuulinganisha mwili wake unaowaka kwa mafuta na udongo. Lakini kwa vile huu ni Ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia, tunaweza kuhakikisha maneno ya Mwenyezi Mungu kuwa ni ya kweli pasi na shaka kwa kuangalia uhusiano uliopo kati ya udongo na mwili wa Binaadamu.
Ukiuchunguza mwili wa Binadamu utakuta una aina mbali mbali za madini kama vile chuma, carbon, calcium, phosphate, iodine n.k., ambayo mtu hawezi kuyapata pengine popote duniani ila ardhini kwenye udongo. Kwa hiyo kuna uhusiano mkubwa kati ya mwili wa mtu na udongo.
Vile vile ukichunguza mahitaji ya mwili wa Binadamu utakuta kuwa yanatoka ardhini kwenye udongo. Mahitaji ya mwili ni yale yanayopatikana kwenye chakula, kwa mfano wanga, protini, mafuta, sukari, n.k. Kwa vile Binadamu anavihitaji vitu hivi kwa ajili ya mwili wake, na vitu hivi viko ardhini, lakini kwa udhaifu wake hawezi kuvipata, Mwenyezi Mungu kwa Rehma zake akaamua kumrahisishia kwa kumuumbia mimea na kisha ile mimea akaipa kazi, kila mmoja ukiwa unafyonza kitu chake. Kwa mfano, muwa unafyonza sukari kutoka ardhini na kuihifadhi kwenye shina lake ili mtu aipate kirahisi; wanga unafyonzwa na mimea kama mihindi, ngano, mpunga n.k., mafuta yanafyonzwa na ufuta, pamba, minazi n.k.; na protini inafyonzwa na mimea ya asili ya maharage. Vyote hivi vinafyonzwa kutoka ardhini, udongoni ili vitumike kuujenga mwili ambao umeumbwa kwa udongo hivyo ni lazima ujengwe kwa vitu vyenye asili ya udongo. Mwenyezi Mungu anatukumbusha kwa kutuambia:-
"Hebu Mwanadamu na atazame chakula chake. Hakika Sisi tumemimina maji kwa nguvu, kisha tukaipasua ardhi, mpasuo maalum, tukaotesha humo chembe chembe, na mizabibu na mboga, na mizaituni na mitende, na mabustani (mashamba) yenye miti iliyo songana barabara, na matunda na malisho, kwa ajili ya matumizi yenu na wanyama wenu.
(Q 80:25-32).