Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
JAMES BRENNAN NA MAPENZI YAKE NA HISTORIA YA TANZANIA
“The Secret Lives of Dennis Phombeah: Decolonization, the Cold War, and African Political Intelligence, 1953–1974”
James R. Brennan
Nimefahamiana na James Brennan sasa yapata miaka 20 alipokuja Tanga kunihoji wakati anafanya Ph D yake na kutoka hapo tumekuwa marafiki wakubwa.
Miaka ile alikuwa kijana mdogo sana namkumbuka akiwa katika T Shirt na mfuko wake wa mgongoni na ''note book,'' yake na akikisema Kiswahili vizuri kabisa.
Jim kama ninavyopenda kumwita amekuwa ananiletea vitu vingi sana katika historia ya Tanzania.
Haji Dar es Salaam ila atanitafuta na anakuja sana kwani yeye ni mpenzi mkubwa wa historia ya Tanzania.
Rafiki yangu Jim hivi sasa ameniletea "paper," yake inayohusu kachero Dennis Phombeah aliyekuwa ndani ya TAA na TANU wakati wa kudai uhuru (Angalia link).
"Paper," hii imenikumbusha mengi niliyopata kuzungumza na yeye hasa urafiki uliokuwapo baina ya Dennis Phombeah na Oscar Kambona.
Huyu kwenye picha hapo chini jina lake ni Charles Mzingeli lakini kwenye kitabu cha Abdul Sykes nimeandika jina lake kuwa ni Charles Mzengele kwa kuwa Ally Sykes aliyekuwa ananileza habari zake huyu bwana ndivyo alivyolitamka hili jina.
Jim kaliandika kama linavyostahili kuandikwa.
Ally Sykes na Dennis Phombeah walikutana na Mzingeli Salisbury, Southern Rhodesia mwaka wa 1953 walipokuwa njiani wakitokea Dar es Salaam kuelekea Lusaka kwenye mkutano ulioitishwa na Kenneth Kaunda Secretary General wa African National Congress (ANC) uliokusudiwa kuhudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa vya Afrika Chini ya Jangwa la Sahara vilivyokuwa vinapigana kuzikomboa nchi zao kutoka utawala wa kikoloni.
Huu mkutano ulihujumiwa pakubwa na wakoloni na haukufanyika kwani wajumbe wote Waafrika wa mkutano ule walidakwa na makachero njiani kabla hata hawajafika Lusaka na haya ndiyo yaliyoukuta ujumbe wa Tanganyika.
Ally Sykes na Dennis Phombeah walikuwa wanaiwakilisha TAA.
Huyu Mzingeli alikuwa kachero mkubwa aliyewasaliti nduguze ndani ya Rhodesia na Ally Sykes na Dennis Phombeah hawakusalimika walipoingia mikonomi mwake usiku mmoja hapo Salisbury.
Jim kanisomesha mengi katika hii "paper" yake kiasi imenitia hamu nirejee katika mazungumzo yetu ya siku za nyuma niandike kitu.
Nitaeleza In Shaa Allah historia ya Dennis Phombeah kama nilivyokutananae katika Nyaraka za Sykes zaidi ya miaka 30 iliyopita na jinsi nilivyokutananae tena hivi sasa katika hii ‘’paper’’ ya James Brennan, Dennis Phombeah akiwa katika maisha yake ya ukachero akianza kazi hii na Special Branch Tanganyika mwaka wa 1954 na baadae akiwa Uingereza na makachero maarufu duniani MI5 na mashirika mengine ya kijasusi ya Ulaya ya Mashariki enzi za Vita Baridi.
Picha: Charles Mzingeli, Dennis Phombeah na James Brennan na Mwandishi wakiwa Kisutu, Dar es Salaam.