Maisha ya Vijijini na imani za Kishirikina

Maisha ya Vijijini na imani za Kishirikina

gstar

JF-Expert Member
Joined
Jun 19, 2011
Posts
790
Reaction score
1,373
Mimi nilizaliwa Kijiji kimoja huko mkoa wa Tanga katika wilaya ya Korogwe, japo baba yangu alitokea mkoa wa Kilimanjaro alihamia hapo kijijini kikazi. Vijiji vingi vya mkoa wa Tanga vilitawaliwa na imani za kishirikina, nikweli kwamba wanaposema katika kila mtaa lazima awepo mzee anayehisiwa kuwa ni mchawi na lazima iwepo nyumba mtakayokatazwa kwenda kunywa maji hata kuwasalimia kwa kuwapa mikono ama kucheza na watoto wao.

Sikumoja tukiwa mtaani mimi na dada yangu nikiwa na umri wa miaka takribani kumi katika kutembea tembea tulikutana na bibi mmoja tunaye mfahamu, huyo bibi litusalimia kwa madaha huku akitusifia kwamba eti mimi na dada yangu tumefanana kama wachina! kumbe alikuwa akituchota akili zetu kwa sababu ya utoto tukawa tukifurahia na kucheka alitumia mwanya huo kututupia zongo. Baada ya hapo mimi niliumwa kwa muda mrefu nilivimba tumbo na kufikia nikicheua inakuwa kama yai viza, nilipelekwa kwa mganga wa kienyeji ili anitoe hilo zongo, nilipona kwa nguvu za Mungu.

Kwa kawaida kule kijijini usiku unakuwa wa kutisha kuliko mchana, hapo kijijini japo kulikuwa na umeme sio nyumba zote zilifanikiwa kuvuta umeme kwahiyo zipo sehemu ama njia ambazo ukipita usiku huwa ni giza totoro na kunatisha balaa, sasa changamoto inakuja pale unapotumwa dukani majira ya usiku huwa inakuwa ni mtihani unaweza ukatembea ukakutana na mauzauza njiani hasa vibwengo.

Kibwengo ukimuona kwa mbali ni kama moto unao tembea, ule moto ni jicho lake moja linalowaka taa kwani kibwengo huwa nikama nusu ya mtu, anajicho moja, pua nusu, mkono mmoja na mguu mmoja ila utashangaa alivyokuwa na kasi ya kutembea. Mara nyingi vibwengo hawamdhuru mtu ila wanakuletea vitisho na mauzauza hasa ukiwa mtoto huwezi kuhimili kuwatazama utajikuta unakimbia kwa kasi lakini mara utashangaa umekutana nacho tena kwa mbele yako, hiyo ndio ilivyokuwa mbinu zao.

Wachawi kuwanga usiku ni utaratibu wa kawaida kwa vijijini, wachawi wanaishi kwenye jamii ama vikundi vyao, kila wachawi wana tamaduni zao kulingana na asili yao ama makabila yao, kwakuwa kijiji chetu kilikuwa na mchanganyiko wa makabila kama Wazigua, Wasambaa na Wabondei. Pia makabila ya bara yalikwepo kama Wakinga, Wapangwa na Wangoni.

Katika tukio moja ambapo Padre wa parokia ya karibu na kijiji chetu alikwenda usiku makaburini kwa miujiza alisimama pembezoni na mara wachawi wakaja kuwanga hapo makaburini huku wakiwa wamevaa rozali zao. Inasemekana walizivua rozali na kuzitundika kwenye kisiki kilichokuwa pembezoni mwa makaburi hayo kisha wakaanza shughuli yao ya kucheza ngoma za usiku, basi baada ya shughuli zao kwisha walikitafuta kile kisiki na hawakukiona, mwisho wa siku walikuja kuumbuliwa siku ya jumapili kanisani padre aliposimama na kuonyesha rundo la rozali alizozipata usiku makaburini. Wachawi wengi hujificha kwenye kivuli cha dini, wengi waliona aibu kwa kutazama chini asilimia kubwa wakiwa ni wamama watu wazima.

Wakati tukiishi hapo kijijini usiku ndio ulikuwa wakutisha kuliko mchana, kuna sauti unaweza kuisikia ikikuita usiku ukiwa umelala mara nyingi huwa inafanana na mtu wako wa karibu kabisa mfano anaweza kuwa mama au baba au dada, sheria inataka usiitike kabisa kwani mara unapo itika inaweza kukutokea jambo baya sana, inakuwa ni kama umewapa funguo za kukuingia mwilini mwako hapo wanaweza kukutendea mabaya yoyote wayatakayo, ndivyo tulivyo aminishwa na wazee wetu. Mara nyingi ningeweza kuzisikia sauti ikiniita kwa jina langu ama kusikia ngoma ikipigwa mlangoni mwa nyumba yetu, kuna wakati niliitika bila kujua.

Wachawi walikuwa wa makabila mbalimbali kwani kule Tanga wilayani Korogwe kuna vijiji ambavyo hapo zamani vilikuwa ni makambi ya wafanyakazi wa viwanda vya mkonge. Asilimia kubwa ya wafanyakazi wa viwanda hivyo walichukuliwa kutoka mikoa ya Iringa, Songea ama Mtwara, hivyo asilimia kubwa ya wakaazi wa vijiji hivyo vya makambi walikuwa ni Wamakonde, Wangoni, Wakinga, Wapangwa na Wabena. wapo makabila mengine waliohamia kwa ajili ya kutafuta maisha mambo yalivyokuwa mazuri walienda bara na kuleta ndugu zao na familia zao.

Hali hii ilifanya waanze kuishi kitamaduni na hasa kuendeleza imani zao za kishirikina. Lakini katika wote makabila yaliyoongoza kwa uchawi ni Wa*** na Wa***. Hawa walifuga majini na misukule na waliongoza kuogopwa na kuhisiwa vibaya, waliweza kukuchekea usoni tu kama watu wema lakini moyoni mwao walikuwa myeusi tii na kila kukicha walikuwa wakipanga mbinu za kuwamaliza vijana na watoto, hivyo ndivyo tulivyo hisi.

Na kwakuwa wachawi walivyokuwa wengi ndivyo waganga pia walivyokuwa wengi. Kwa kila kijiji hapakukosa waganga wa kienyeji wasiopungua watano mpaka sita hao walikuwa wakiagua kwa kuchanja chale na kutumia tunguli ama uganga wa kupiga ramli n.k. Haikuwa jambo la ajabu kutembea na kukuta mtu akigangwa hadharani. Wateja wengi walikuwa wageni kutoka mikoani ama wengine walikuwa ni wa hapo hapo.

Kikubwa kilichonifanya niandike uzi huu ni jinsi mzee mmoja jina nalihifadhi alipomaliza familia nzima kwa kuwauwa kichawi mpaka ukoo mzima ulipomwendea kwa kumpigia magoti na kumwomba msamaha. "Mzee kama tumekukosea tunaomba utusamehe sisi usije ukatumaliza wote!" Yule mzee alikohoa na kucheka kisha akasema, "Nilijua mgekuja tangu mapema japo mmechelewa, ila kwakuwa mumeuona umuhimu basi nimewasamehe."

Ilikuwa hivi, kijana mmoja aliyekuwa wa umri kati ya miaka 10 mpaka 14 alipofariki dunia kwa hali ya kutatanisha. Kijana alikwenda shambani na wazazi wake kulima akatoroka na kwenda kwenye mkorosho kuangua mabibo wakati anapanda bahati mbaya alianguka lakini mkorosho haukuwa mrefu sana, basi alipata majeraha na kukimbizwa hospitali ya teule Muheza, huko walisema anapaswa kufanyiwa operesheni kubwa kwakuwa walisema apepasuka baadhi ya viungo vya ndani basi operesheni ile ndiyo ilikuwa mwisho wake alifariki pale hospitali baada ya kukaa kwenye mashine ya oxygen kwa siku mbili.

Msiba ule ulitikisa kijiji kizima nakumbuka kwa kipindi kile hata mimi nilikuwa mdogo lakini niliona karibu kijiji kizima kilizizima watu wote hawakwenda mashambani wala makazini walikusanyika nyumbani kwa yule mzee aliyefiwa na mwanaye vilio na majonzi vilitawala. Ila cha ajabu usiku wa msiba watu wakiwa wamelala kwenye maturubai alikuja yule mzee akatangaza bila woga kwamba mimi ndiye niliye muuwa huyu kijana, watu walimshangaa huyu mzee ila hakuna aliyesema kitu.

Nakumbuka kijana baada ya kuzikwa haikupita mwezi mama yake mlezi naye akafariki, alikosa choo kwa muda mrefu alilazwa na kufariki, na hapo pia yule mzee alikuja kujitapa tena kwamba yeye ndiye aliyefanya unyama ule wa kutoa roho ya yule mama wa watu. Ndipo ukoo mzima walipoitana kutoka vijiji mbalimbali na kukusanyika kwenda kumuomba msamaha yule mzee, nadhani kufikia hapo ndio ikawa pona yao japo aliwasamehe lakini aliwaachia majeraha ambayo ingechukuwa muda mrefu sana kuyasahau.
 
Yani some la ufupisho hukuwepo darasani inakuwaje muhtasari ni mrefu kuliko kiini cha story
 
Yaani mtu aje mbele ya kadamnasi aseme kwamba yeye kaua watu Fulani Kwa uchawi halafu watu wamwangalie TU? labda Kwa vile ni hadithi kama hadithi zingine.
 
Back
Top Bottom