Date::12/10/2008
Majambazi yapora mchana kweupe Dar yaua mmoja
Ummy Muya na Tumsifu Sanga
Mwananchi
SASA ni dhahiri; wimbi la ujambazi limerudi upya baada ya kutulia kwa muda mrefu.
Majambazi wanne jana saa 3:00 asubuhi walivamia kituo cha mafuta cha Gapco, kilicho katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Kawawa umbali wa hatua zisizozidi 150 kutoka kituo cha polisi cha Magomeni, na kumpiga risasi mhasibu wa kituo hicho cha mafuta kabla ya kupora mamilioni ya fedha na kutoweka.
Tukio hilo la uporaji wakati jua likiwa limeshashamiri, ukiacha matukio ya kuteka vijiji, mabasi na masoko, ni salamu tosha kwa Jeshi la Polisi kwamba wimbi la ujambazi lililokuwa likifanyika waziwazi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, sasa limerudi upya.
Matukio ya ujambazi yalikuwa yametulia tangu serikali ilipoamua kufanya operesheni maalum ya kupambana na uhalifu huo, ikiongeza askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufanya doria barabarani na kutumia pikipiki kudhibiti nyendo za majambazi, hatua ambayo ilikuwa na mafanikio makubwa.
Lakini jana, majambazi yaliyovamia kituo hicho cha mafuta yalionekana kurudia ukatili wao wa kuua wakati yalipokuwa yamepania kupora fedha za kituo hicho ambazo zinasadikiwa kuwa ni mauzo ya siku nne.
Mashuhuda wanasema risasi kadhaa zilipigwa hewani na majambazi wawili, wakati wenzao wakiwa wamevamia kituo hicho.
Majambazi hayo, kwa mujibu wa mashuhuda, walitinga kituoni hapo wakiwa na gari aina ya Toyota Mark ll. Wakionekana kuwa walishajua nyendo za mhasibu, majambazi hayo yalizuia gari lililomchukua mhasibu huyo, Seraphine Madenge na mkurugenzi wa kituo hicho, George Kretson, 74 ambaye ni raia wa Ugiriki, na kulisimamisha.
Baadaye, kwa mujibu wa mashuhuda hao, jambazi mmoja alishuka na kwenda kugonga kwenye kioo cha gari hilo na alipoona hawafungui ndipo alipokivunja kwa ngumi na baadaye kuomba apewe fedha. Alipokataa ndipo walipomuua mhasibu huyo kwa risasi.
Mmoja wa walinzi wa eneo hilo, aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema majambazi hao walimuua mhasibu huyo katika kujibu mapigo baada ya mlinzi mmoja kufyatua risasi hewani katika kutaka kuwazuia wasitekeleze nia yao.
"Mlinzi mwenzangu ambaye analinda kituo hiki cha mafuta baada ya kuona majambazi hao wanalizuia gari la mkurugenzi, akahisi kuna hali ya hatari na akaanza kupiga risasi hewani bila kujua kama maadui hao wana silaha ama la," alisema.
Alisema baada ya majambazi kusikia mlio huo wa risasi walivunja kioo cha mlango wa gari lililokuwa likitumiwa na mkurugenzi na mhasibu huyo kabla ya kumuua na kumsababishia majeraha mkurugenzi huyo.
"Mkurugenzi huyo aliwahi kushuka na kukimbilia ofisini na kumwacha mhasibu wake ndani ya gari ambaye aliamrishwa kuzisamilisha fedha alizokuwa nazo, lakini aligoma," alieleza mlinzi huyo na kuongeza:
"Majambazi hao walimpiga risasi ya mbavu na ikatokea upande wa pili kisha wakamtoa kwenye gari na kumtupa chini hapa sasa ndio kazi ikaanza hawa wawili wakawa wanaendelea kupiga risasi hewani na wengine wanachukua fedha na kuweka katika gari yao."
Kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni, Mark Karunguyeye alikiri kutokea kwa mauaji hayo na kubainisha kuwa ilikuwa jana majira ya saa 3:30 asubuhi.
Alisema majambazi hayo, ambayo bado hayajatiwa nguvuni, yalikuwa yakitumia gari ndogo nyeupe aina ya Toyota Mark 11 ambayo iliingilia Barabara ya Kawawa na kuizuia kwa mbele gari iliyokuwa ikitumiwa na mkurugenzi na mhasibu wa kituo hicho cha mafuta.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Evarist Mangala alithibitisha kutokea kwa tukio hili na kusema kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi.
"Hatukufahamu mapema walikuwa na silaha ngapi, isipokuwa jambazi mmoja alikuwa akitumia bunduki aina ya SMG ndio aliyofyatua risasi na kuvunja kioo huku akiamuru apewe fedha ambazo ni mauzo ya siku nne tangu Jumamosi hadi leo (jana)," alisema Karunguyeye.
Baada ya majambazi hayo kutoweka mkurugenzi wa kampuni hiyo na marehemu walikimbiziwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kabla ya mauti yake. Kretson alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani kwake.
Karunguyeye alisema kuwa ganda la risasi lililookotwa linaweza kutumika katika bunduki aina ya SMG na SAR na kuongeza kuwa jeshi la polisi linaendelea na msako, ili kuwanasa hatuhumiwa wa tukio hilo ambao wamesababisha mauaji.