Date::12/31/2009Nyumba nyingine BoT yagharimu Sh1.2 bilioni
Kizitto Noya
WAKATI Wizara ya Fedha na Uchumi ikiwa katika uchunguzi wa gharama za ujenzi wa nyumba ya gavana wa BoT inayodaiwa kugharimu Sh1.4 bilioni, imebainika kuwa nyumba nyingine ya mmoja wa manaibu wake imegharimu Sh1.2 bilioni.
Taarifa ya BoT iliyowekwa kwenye mtandao wake wa
www.bot-tz.org jana mchana ilieleza kuwa nyumba ya gavana iliyoko katika kiwanja namba 12 Barabara ya Tumbawe maeneo ya Oysterbay ilipendekezwa kujengwa kwa gharama ya kati ya Sh1,399,184,549.00 hadi Sh1,847,763,537.00, lakini benki iliidhinisha Sh1,274,295,025.26.
"Mapendekezo kutoka kwa makandarasi yalikuwa na viwango vya gharama kuanzia Sh1,399,184,549.00 hadi Sh1,847,763,537.00 kwa kiwango cha juu.
Baada ya tathmini ya zabuni hizo na kufanya masahihisho ya tarakimu zilizowasilishwa, mzabuni aliyeshinda kwa kuwa na gharama ya chini kuliko wote alikuwa ni M/S Eletrics International Co. Limited. Gharama yake baada ya masahihisho ilikuwa ni Sh1,274,295,025.26," ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:
"Taarifa ya tathmini hiyo ilipitia tena kwenye Bodi ya Wazabuni na ndipo ilipofikia uamuzi wa kumteua M/S Eletrics International Co. Limited kwa bei ambayo haitabadilika (fixed price) ya Sh 1,274,295,025.26 ya kukamilisha ujenzi huu katika wiki 32."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo mkataba wa ujenzi na mkandarasi huyo ulitiwa saini Juni 3, mwaka 2008 na kazi ya ujenzi ikaanza mara moja.
Taarifa imeeleza kuwa Bodi ya Zabuni (DSM) ya Benki Kuu ikaridhia pia kuwa kampuni ya Remco (International) Limited ishughulikie masuala ya vipoza hewa; Ginde EAP Services Ltd masuala ya maji safi, mabomba na maji taka na Pomy Engineering Co.Ltd ishughulikie masuala ya umeme.
Wakati nyumba hiyo ikigharimu kiasi hicho cha fedha nyumba nyingine namba 57 Mtwara Crescent imejengwa kwa gharama ya Sh1,272,348,512.00 kwa muda wa majuma 24 na kampuni ya Holtan Builders Ltd.
Taarifa imefafanua zaidi kuwa ujenzi huo umetokana na mabadiliko ya Sheria ya Mwaka 2006, yaliyoitaka benki hiyo kuwa na manaibu gavana wanne badala ya wawili.
"Hapo awali gavana alikuwa anaishi Barabara ya Mahando kiwanja namba 387 Masaki na Naibu Gavana Barabara ya Msese kiwanja Namba 43,"ilieleza taarifa hiyo na kuongeza kuwa;
"Baada ya mabadiliko ya Sheria ya mwaka 2006, Benki Kuu ina viongozi wakuu wanne; Gavana na Manaibu wake watatu na kwa mujibu wa mikataba iliyowekwa kila mmoja anastahili kupata nyumba ya kuishi."
"Nyumba zote mbili zilipangwa ziwe za ghorofa moja, vyumba vitano vya kulala, wenyeji na wageni, sebule ya wageni, sebule ya familia, mahali pa kulia na vyoo na mabafu yanayoendana na idadi ya vyumba," ilieleza taarifa hiyo na kutaja majengo ya nje kuwa ni pamoja na nyumba ya kuishi watumishi, gereji ya magari, bwawa dogo la kuogelea, ukuta, vyombo vya usalama na kibanda cha walinzi.
Kazi zingine zilizoongeza gharama za majengo hayo ni pamoja na mashine ya umeme (generator), mashine ya kupoza hewa, matanki ya kuhifadhi maji na kutengeneza mahali pa kuegesha magari na bustani.
Kabla ya ujenzi wa nyumba hizo, taarifa ilieleza kuwa Benki Kuu ilikodi nyumba mbili, moja kiwanja namba 480 Barabara ya Bray, Masaki na nyingine kiwanja namba 591, Msasani Peninsular kwa matumizi ya viongozi hao wawili ambao walikuwa bado wanaishi kwenye nyumba zao mbali na ofisi.
"Kati ya Oktoba 2007 aliporipoti kazini kama Naibu Gavana hadi Aprili 2008, Profesa Ndulu aliishi kwenye nyumba yake iliyoko Mbezi Beach, na Naibu Gavana Mkila naye pia aliishi nyumbani kwake kabla ya kuhamia kwenye nyumba hizi zilizokodishwa,"ilieleza taarifa na kuongeza: "Benki Kuu iliamua kumhamisha Naibu Gavana Juma Reli kwenda Barabara ya Mahando Masaki ili kuruhusu matengenezo ya nyumba aliyokuwa anaishi Kinondoni Barabara ya Msese."
Taarifa imeeleza kuwa Naibu Gavana Dk Bukuku anaishi kwenye nyumba yake na Benki Kuu inatoa posho ya nyumba kulingana na mkataba. "Nyumba hizo mbili zilizojengwa chini ya miradi iliyotajwa, sasa hivi zimekamilika. Gavana wa Benki Kuu, Profesa Ndulu alihamia nyumba namba 12 Barabara ya Tumbawe Desemba 17,2009 na Naibu Gavana Mkila alihamia nyumba namba 57 Mtwara Crescent Desemba 4,2009," ilieleza taarifa hiyo.