Mwenda_Pole
JF-Expert Member
- Jul 5, 2008
- 281
- 66
HARAKATI za kuwania ubunge kwenye majimbo mbalimbali mkoani Tanga zimeshika kasi, huku kukizuka malalamiko katika baadhi ya maeneo kuwa baadhi ya vigogo wa CCM wameanza mchezo mchafu; akiwemo Katibu Mkuu, Yusuf Makamba ambaye anadaiwa kumwandalia njia kijana wake.
Makamba anadaiwa kuwa ameingia katika baadhi ya majimbo na kuendesha kampeni za kuwang'oa wabunge waliopo na kuwawekea mazingira ya ushindi watoto wake.
Hata hivyo Makamba alikanusha kufanya kampeni hizo chafu kwa sababu yeye ni kiongozi wa juu wa chama na kwamba, wanaosema hivyo wamkome kabisa kumsingizia.
Inadaiwa kuwa mtendaji mkuu huyo wa CCM ameandaa kundi maalumu linaloendesha kampeni kwa mgongo wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) likiwa na kauli mbiu ya kutaka majimbo yote ya Tanga yanyakuliwe na wabunge vijana.
Malalamiko dhidi ya Makamba yameenea katika majimbo ya Bumbuli na Korogwe Vijijini ambako anadaiwa ameanza mikakati ya kumuandaa mtoto wake Januari Makamba, ili awanie ubunge katika moja ya majimbo hayo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili umebaini kwamba, mwezi uliopita Makamba aliandaa ziara ya kutembelea kata za Jimbo la Bumbuli, lakini akakumbana na vikwazo na kulazimika kubadilisha msimamo na kuondoka.
Viongozi wa CCM waliopo wilayani Lushoto walidai kuwa akiwa katika jimbo hilo alikuwa akifanya mikutano ya ndani ya wanachama wa CCM akiwashawishi wasimchague Mbunge wa sasa,William Shellukindo katika uchaguzi ujao badala yake atamleta kijana wake Januari kuchukua nafasi hiyo.
Inadaiwa kuwa katika mikutano hiyo ya ndani Makamba alieleza wazi kuwa asingependa Shellukindo apewe tena nafasi ya ubunge kwa kuwa yupo mstari wa mbele katika kuendesha mapambano dhidi ya mafisadi.
Diwani wa Kata ya Baga CCM, Charles Ndege alisema mchezo unaofanywa na Makamba katika Jimbo la Bumbuli sio wa kuunyamazia kwa sababu unaleta mvurugano miongoni mwa wanachama wa CCM.
Alisema wananchi wanashangaa kuona kiongozi kama Makamba, anaamua kucheza mchezo mchafu wa kupiga vita wanaopambana na ufisadi.
"Hata nikipelekwa popote sitanyamaza, Makamba amefanya vikao vya siri katika kijiji cha Mahezangulu, Kwebaga na vijiji vingine, akimponda Shellukindo," alisema Ndege na kudai kuwa kundi la UVCCM linalopita vijijini linaongozwa na baadhi ya viongozi wake wa Wilaya ya Lushoto.
Diwani huyo alisema miongoni mwa mambo yanayofanywa na timu hiyo ya vijana, ni kuonyesha picha ya Januari ambayo alipiga pamoja na Rais Jakaya Kikwete, wakidai kuwa rais ameagiza achaguliwe kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Mbali na Januari anadaiwa pia kumuandaa binti yake, ili awanie nafasi ya ubunge wa viti maalumu kupitia Jumuiya ya Wanawake (UWT), Mkoa wa Tanga.
Alipohojiwa na Mwananchi Jumapili kuhusiana na taarifa hizo, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, William Shellukindo alisema hata yeye amesikia, lakini hana hofu kwa wagombea kwenda kuwania nafasi hiyo huku akisisitiza kuwa wafuate taratibu badala ya kutumia mchezo mchafu.
"Hilo mimi nimelisikia wananchi wakilalamika, lakini ninachosema ni kwamba, kama wanajiamini hakuna haja ya kutumia mchezo mchafu wa kuanza kampeni kabla ya wakati, badala yake wasubiri muda ufike halafu wapige kura wataamua," alisema Shellukindo.
Katika Jimbo la Korogwe Vijijini linaloshikiliwa na Lous Mhina, wanaCCM wamedai kuwa, Makamba amekuwa akipima upepo kuona iwapo mtoto wake Januari anaweza kulichukua.
"Makamba anafanya vikao vya siri na kuwapanga wapiga debe maalumu kwa ajili ya mtoto wake huyo, lakini mbona anaanza kampeni mapema?
Inakuwaje yeye ni kiongozi halafu anakuwa wa kwanza kuvunja utaratibu tuliojiwekea ndani ya chama," alisema kada mmoja wa CCM anayeishi Kata ya Mashewa wilayani Korogwe.
Mwananchi Jumapili ilipozungumza na Mbunge wa jimbo hilo alisema siyo rahisi jimbo lake kutwaliwa na mtu mwingine kama baadhi ya watu wanavyodhani.
"Mimi si mtu wa kujisifu, lakini kuna mambo mengi ya maendeleo nimeyafanya na wananchi wanatambua hilo. Makamba namheshimu kama Katibu Mkuu wangu wa CCM na pia mzee wangu; hivyo sitegemei kama atakuwa mstari wa mbele katika kuongoza mchezo mchafu. Lakini hayo nimeyasikia,"alisema Mhina.
Alipoulizwa na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusiana na tuhuma hizo, Makamba, alikanusha vikali na kusisitiza kuwa yeye ni kiongozi wa ngazi za juu wa CCM, hivyo hawezi kushiriki katika kampeni za mchezo mchafu.
"Mimi na Shellukindo ni kitu kimoja, huyu ni kada wetu muhimu sana bungeni na ni kiongozi anayeheshimika si kwa Tanzania pekee hata nje ya nchi, amesaidia mambo mengi katika taifa hili. Hao wanaosema hivyo wanikome," alisema Makamba.
Kuhusu Jimbo la Korogwe Vijijini, Makamba alisema yeye ni mzaliwa wa huko na kutaja eneo la Mahezangulu kuwa ndipo nyumbani kwake na kwamba, huwa anakwenda huko wakati wowote hivyo si kufanya kampeni.
"Mimi nilishasema sigombei ubunge, hili nilitangaza rasmi tena pale Korogwe, sasa suala la Januari kama anagombea, hilo mimi siwezi kumuingilia kwani naye ni mwanaCCM na ana matakwa yake," alisema Makamba.
Chanzo: Mwananchi 17.10.2009