HANSARD YA ALICHOSEMA MAKAMBA .
MHE. YUSUFU R. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekaa muda mrefu sana bila kuzungumza, nilikuwa shuleni, maana sisi tuliozoea kuzungumza kwenye mikutano ya "pasua baba" ukiingia hapa unaweza kuharibikiwa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili Tukufu, naomba nichukue nafasi kwanza ya kumshukuru Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuniteua kuwa Mbunge. Deni la fadhila hulipwa kwa fadhila. Nina deni kubwa sana kwake, natafuta namna ya kulilipa, sijui… lakini nafikiri namna nzuri ya kulipa deni hili ni kujitahidi kwa uwezo wangu wote kutumia nchi yetu na Chama changu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Maandiko Matakatifu ndani ya Biblia yanasema, "anayetamani Uaskofu, anatamani kazi njema". Sasa leo nazungumza Spika hayupo, lakini nafikiri yatamfikia. Kama anayetamani Uaskofu anatamani kazi njema, basi anayetamani Uspika naye anatamani kazi njema, lakini ni ngumu. Kwa hiyo, nataka nichukue nafasi hii kumpongeza Spika na mimi naridhika na namna anavyotuongoza. Nafurahi hasa kwa kuzingatia kwamba ni Spika anayetoka Chama changu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vile vile nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Siku njema, huanza mapema, ameanza vizuri! Labda niseme tu kwamba pengo la jino la dhahabu limezibwa kwa jino la dhahabu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Nabii Yeremia anapewa unabii, aliogopa sana, lakini Mwenyezi Mungu akamwambia usiogope, nitatia maneno yangu katika kinywa chako na wewe utazungumza kwa niaba yangu, ndipo Yeremia akapewa utume. Kwa hiyo, hayupo hapa, lakini nataka nimwambie kwamba asiogope, huyo anayemteua kwa kawaida huweka maneno katika kinywa chake ambaye ni Rais na Chama chake. Kwa hiyo, mimi nafikiri atafanya vizuri, tumtie moyo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uniruhusu vile vile na mimi niwashukuru Wabunge wa Chama changu. Ninapotembelea Jimbo langu la Uchaguzi, ninawakuta huko wanajitahidi sana katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mimi nataka niwaondoe hofu, tukienda namna hii, 2010 kazi ni rahisi. Tukiendelea namna tunavyokwenda hivi sasa, kazi yetu mwaka 2010 ni rahisi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba na mimi niseme mambo machache na wala sitasema mambo makubwa sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, mtaniwia radhi, Mzee Ngombale alipokuwa anachangia hapa Bungeni, alisema anaipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa kazi nzuri inayoifanya na hasa Mheshimiwa Rais kwa kusimamia utekelezaji wa Ulani ya Uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku mbili baada ya hotuba ya Mzee Ngombale, alisimama Mbunge mwingine (kwa staili ile ya waandishi wa habari, jina ninalo) akasema sisi wenzenu wa Kambi ya Upinzani, masikio tunayo, macho tunayo na midomo tunayo. Haya tunayoyasema tunayaona, haya tunayoyasema tunayasikia, akamaliza. Lakini na mimi nataka niseme, asubuhi yake gazeti liliandika "Mzee Ngombale awekwa kitanzini".
Sasa na mimi nataka niseme, unaweza ukawa na macho, unaweza ukawa na masikio, lakini unapoona mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ya CCM, unaweza ukayafumba tu usione. Unaweza ukawa na masikio, lakini ukayaziba, ukayatia hata na pamba ili usisikie mambo mazuri yanayozungumzwa juu ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Hata ukaambiwa kwamba pale Dodoma kinajengwa Chuo Kikuu, unaweza lile jengo ukalipa kisogo usilione. Unaweza hata kitabu kizuri hiki cha bajeti tuliyosomewa leo, mipango mizuri hii ya kilimo usiione, ukaona Ibara moja ndogo tu ambayo kwako unaona ina upungufu, ukakazana na hiyo, ukashindwa kujua kwamba hotuba yote hii imetengenezwa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu kuwa na masikio si hoja, kuwa na macho si hoja. Sasa ninachotaka kusema ni kwamba ukijua kulaumu, ujue kusifu, vinginevyo wenzako watakwambia una kilema, maana yale unayoyasema hayafanyiki, yanafanyika hata kwenye Jimbo lako, watu wako wanaona, wewe huoni! Nafikiri mmenielewa! Nasema ukijua kulaumu, ujue kusifu, vinginevyo utaambiwa una kilema!
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nataka sasa nimpongeze Mheshimiwa Rafiki yangu Wasira kwa hotuba nzuri na ili nisije nikasahau, basi naunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani tunaye bingwa wa kuandika maandiko mbali mbali ya Chama cha Mapinduzi. Tulianza mwaka 1972 na Siasa ni Kilimo, kitabu ninacho hapa. Lakini kabla ya 1972 kulikuwa na Mwongozo wa 1971 umezungumza kilimo. Azimio la Iringa limezungumza kilimo, Sera za CCM katika miaka ya 1990, zinazungumza kilimo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu inazungumza kilimo. Sasa naomba mniruhusu nilitazame lile Azimio la Iringa la Mwaka 1972, Ibara ya 36, inasema hivi; "Watumishi wa kilimo hawawezi kuwepo katika kila kijiji wakati ule ule wanapohitajika, lakini maarifa ya kilimo lazima yaenezwe kila mahali hivi sasa, 1972".
Mheshimiwa Mwenyekiti, Azimio hilo hilo la Iringa linasema "kazi za viongozi (Ibara ya 36) ni nne:- Ya kwanza, wajifunze wao wenyewe kanuni za kilimo". Hizi humu ndani, tujifunze sisi wenyewe kanuni za kilimo. Sina hakika Wasira unazijua kwa kiasi gani! Nimemtaja ni rafiki yangu, hatanipeleka kokote! Pili, "wawaeleze wananchi kwa nini Kilimo cha kizamani hakifai tena na kuwafanya wakulima wawe na hamu ya kujifunza na kutumia maarifa mapya". Tatu; "kuhakikisha pembejeo na zana nyingine zinawafikia wakulima kwa wakati unaofaa". Hivyo ndivyo tunavyoelekezwa kwamba sisi wenyewe tujifunze kanuni za kilimo bora. Sasa ukisoma hotuba iliyotolewa hapa ukurasa wa 20, Ibara ya 31, Waziri anatuambia mwaka 2007/2008 wataalam wa ugani 309 waliajiriwa, lakini lengo ni 2500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri hata ukifikisha lengo hili la 2500, mimi kwangu nafikiri namna nzuri ambayo tunaweza tukafanya… nchi hii ina viongozi wengi sana, viongozi wa CCM wanaanzia kwenye Shina, Kata, Wilaya, Mkoa. Kwa maelekezo ya kitabu hiki ni kwamba sisi wenyewe lazima tuongoze kwa mfano. Hivi ukilitazama shamba la rafiki yangu Siraju, ni mfano? Watu wako wanaweza wakaja wakajifunza kwenye shamba lako? Usikasirike! Wewe mtani wangu! Shamba la rafiki yangu Lowassa, ng'ombe nakubali, maana ng'ombe wako nimewaona. Lakini shamba lako je? Shamba la rafiki yangu Kapuya ni mfano? Nataka nichukue nafasi hii, Waheshimiwa Wabunge wenzangu, tunaandika sana, tunasema sana, lakini tatizo ni kwenda kutekeleza yale ambayo tunayasema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kitabu cha Mathayo 23 kinasema; "maneno ya Makuhani hawa na Mafarisayo, yasikilizeni kwa sababu wamekaa katika kiti cha Musa, lakini kwa mfano wa matendo yao msifuate. Wananena, hawatendi, wanawatwika watu mizigo mikubwa, wenyewe hawagusi hata kwa vidole". Ndani ya Quran maneno hayo yamo, kwa wale wenzangu waliobobea, wakina Siraju. Yanasema: "Yaa aiyuhalladhina amanu limatakuluna malatafaaluna". "Enyi mlioamini mbona mnasema maneno ambayo ninyi wenyewe hamtendi?". Sasa sisi tunazungumza kilimo, mashamba yetu mabaya na wananchi wanatusikiliza hapa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya CCM katika miaka ya 1990 inasema hivi; "Serikali inatakiwa kutambua na kuwaenzi wakulima kwa mfano. Pili, kuanzisha mashindano ya kilimo, tatu; kuwatumia wakulima bora kuwafundisha wakulima wengine. Kwamba hata wale wakulima bora ambao tayari kwenye maeneo yetu tulionao wanaweza kuwa Maafisa Ugani kwa kuwafundisha wakulima wengine, wapo? Kwenye mashindano ya Nane Nane, TASO inaendesha mashindano, wanapatikana wakulima bora kutoka kila vijiji na kata, lakini je, wanaporudi kule, tunawaenzi? Je, tunawatumia kuwafundisha wengine? Hatufanyi! Lakini maandiko yako pale, kila mtu akiandika, anaya-quote, kuyatekeleza hamna! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Uchaguzi ya 2005, 31(e) inazungumza zawadi, tuzo kwa Mikoa na Wilaya. Inasema hivi; "Serikali itatakiwa kuhimiza kutoa vivutio, zawadi na tuzo kwa Mikoa na Wilaya ambazo wakulima wake wataweza kuongeza maradufu tija na mazao yanayovunwa katika heka katika kipindi cha Ilani hii. Msisitizo utawekwa kwenye mazao ya mahindi, mpunga, migomba, kunde, tumbaku, chai". Inaendelea; "viongozi waongoze mapinduzi ya kilimo kwa kutena wao wenyewe". Ni sura ya 9 ya Ibara ya 132.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo Mikoa ambayo tayari imekwishaonyesha mfano katika uzalishaji wa mahindi; Rukwa, Mbeya, Iringa na Ruvuma. Mimi sikumbuki, labda Wiziri atakapomaliza atuambie, mmewatia moyo kwa tuzo gani!
(Hapa kengele ya pili ililia kuashiria kumalizika muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Makamba, hiyo ni kengele ya pili, mchango wako ni mzuri sana, lakini muda tu.
MHE. YUSUFU R. MAKAMBA: Nilikwisha unga mkono hoja!
MWENYEKITI: Tunashukuru sana kwa hilo!
MHE. YUSUFU R. MAKAMBA: Asante sana! (Makofi)