Cute Wife
JF-Expert Member
- Nov 17, 2023
- 1,906
- 5,000
====
Aliyekuwa mshambuliaji wa Mashujaa FC, Athuman Masumbuko 'Makambo Jr' amejiunga rasmi na Klabu ya 1.FCA Darmstadt ya Ujerumani kwa mkataba wa miaka mitatu.
Nyota huyo awali ilielezwa amemalizana na Coastal Union ili kuitumikia msimu ujao wa mashindano ikiwemo Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika, lakini ameibukia Ujerumani.
Akizungumza baada ya kukamilisha dili hilo, Makambo alisema ni furaha kubwa kwake kuanza changamoto mpya huku akiweka wazi kwamba atahakikisha anapambana kwa ajili ya kuitangaza nchi kimataifa kama ambavyo wamekuwa wakifanya wachezaji wengine.
Kwa upande wa Kocha Awadh Juma 'Maniche' aliyemfundisha mshambuliaji huyo akiwa na timu ya vijana ya Mtibwa Sugar chini ya miaka 20, alisema ni fursa nzuri kwa nyota huyo kuzidi kujitangaza kimataifa kwani kabla ya hapo alimtabiria kufika mbali zaidi kutokana na uwezo wake.
"Mchezaji anapopata nafasi ya kutoka nje ya mipaka ya Tanzania ni jambo la kushukuru kwa sababu anazidi kupata uzoefu wa kucheza na wachezaji mbalimbali, ni kijana mdogo mwenye malengo makubwa, hivyo tumuombee kwa niaba ya taifa," alisema.
Nyota huyo alijiunga na Mashujaa msimu uliopita wa 2023/2024 baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiichezea timu ya vijana ya Mtibwa Sugar iliyobeba ubingwa, huku akiibuka pia mfungaji bora kwa kutupia kambani mabao saba akiwa na kikosi hicho cha Umri chini ya miaka 20 (Mtibwa U20).
1.FCA Darmstadt iliyoanzishwa Septemba 10, 1954, kwa sasa inashiriki Verbandsliga Hessen Süd ambayo ni Ligi Daraja la Sita Ujerumani Ukanda wa Hesse.
Mwananchi