Makapuku Forum

Mshambuliaji wa Atletico Madrid Antoine Griezmann, 32, yupo mbioni kuondoka kwenye timu yake hiyo ifikapo Januari mwakani na kutua kwenye Ligi Kuu ya Marekani ambako amepokea ofa kutoka timu mbalimbali ikiwemo na Inter Miami inayoitumikia Lionel Messi.
.
Atletico imeonyesha nia ya kumuachia straika huyo na tayari imedaiwa kuwa imeshapata mbadala wake ikiwa Griezmann ataamua kuondoka. Mara kadhaa straika huyo amenukuliwa akisema kwamba ndoto yake siku moja ni kucheza Ligi Kuu ya Marekani pale atakapoondoka Ulaya.
.
Licha ya utayari wa kumuuza, Atletico imesisitiza kwamba inahitaji ofa nzuri itakayoweza kuwashawishi kufanya hivyo kwani bado ina mkataba na Griezmann hadi mwaka 2026. Atletico inamuangalia straika wa Juventus, Federico Chiesa, kama mbadala wa Griezmann.
 
Mkongwe wa Liverpool, Jamie Carragher anaamini Mohamed Salah ataondoka katika klabu hiyo siku za usoni baada ya dili kubuma katika dirisha la usajili la kiangazi.
.
Mchambuzi huyo wa Kituo cha Televisheni cha Sky Sports alitoa maoni yake akidai ni suala la muda tu na hatashangaa kama Salah akiondoka katika kipindi cha miezi 12 ijayo.
.
“Mkataba wake utamalizika kabla ya mashabiki kujua. Nadhani hisia za mashabiki wengi wa Liverpool wanadhani Salah atacheza zaidi ya msimu mmoja. Kama Liverpool itamuuza Salah itapata pesa ndefu na itasajili mbadala wake siku za usoni, lakini ngumu sana kupata mchezaji wa ubora wake, labda atatokea sijui nafikiri. Liverpool ina miezi 12 ya kufikiria mchezaji mwingine ambaye atakuja kuziba pengo lake.”
.
Taarifa ziliripoti Salah alilazimisha kuondoka Anfield hata hivyo, Liverpool ilisisitiza nyota huyo wa kimataifa Misri hauzwi kwa dau lolote. Al-Ittihad ilikuwa na nia ya dhati ya kumsajili Salah na ilitoa ofa zaidi ya Pauni 200 milioni hata hivyo Liverpool ikapiga chini.
 
Beki wa zamani wa Chelsea, John Terry amepata shavu la kuwa kocha wa Al-Shabab inayoshiriki Ligi ya Saudia kwa mujibu wa ripoti. Terry alifuatwa na klabu hiyo miezi miwili iliyopita tayari amefikia makubaliano na wakati wowote atajiunga.
.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 42 amepewa mkataba wa miaka miwili, lakini anaweza kuendelea kuinoa zaidi ya miaka miwili mkataba wake utakapokamilika.
.
Terry anaungana na nyota wengi wa zamani wa Ligi Kuu England kwenye ligi hiyo akiwemo mchezaji mwenzake wa zamani wa Timu ya Taifa ya England, Steven Gerrard ambaye anainoa Al-Ettifaq.
 
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa @innocentbash ameuagiza Wakala wa Majengo (TBA) kuhakikisha wanakuja na mikakati itakayosaidia kujenga nyumba za bei nafuu hasa kwa Vijana wanaoajiriwa katika utumishi wa umma hususani Dodoma ili kuweza kumudu gharama za maisha.

“Kuna Vijana ambao wanaingia kwenye kada ya utumishi wa umma na bado hawajawa na uwezo wa kujijengea nyumba, kupitia TBA mnaweza kujenga nyumba za bei rahisi kwa ajili ya Vijana hao ili kuwarahisishia gharama za maisha”

Bashungwa pia ameutaka Wakala huo kuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo Watalaamu walionao ili kuenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia hasa katika suala la ujenzi na uendelezaji wa majengo mbalimbali.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, amesema kuwa Wakala huo utahakikisha unatafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo na kumuahidi Waziri Bashungwa kuandaa mikakati mizuri itakayosaidia Wakala huo kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Awali, Arch. Kondoro ameeleza kuwa hadi sasa TBA inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma eneo la Nzuguni Dodoma ambapo awamu ya kwanza ya nyumba 150 utekelezaji umefikia asilimia 95 na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 150 utekelezaji wake umefikia asilimia 10, miradi mingine ni ujenzi wa nyumba 20 za Viongozi Jijini Dodoma ambazo zililenga kukabiliana na uhaba wa nyumba za Viongozi baada ya Serikali kuhamia Dodoma ambapo mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na nyumba zimeanza kutumiwa na Viongozi.
 
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limesema nafasi za kujiunga na Mafunzo ya JKT kwa kujitolea kwa mwaka 2023 haziuzwi bali zinatolewa bure kwa Vijana wote wa Kitanzania wenye sifa zilizoainishwa hivyo Watu wachukue tahadhari wasitapeliwe.

“Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele hivi karibuni alitoa wito kwa Vijana wote wa Tanzania Bara na Visiwani wenye sifa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa kujitolea kwa mwaka 2023 katika taarifa yake iliyotolewa na Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena ilianisha kuwa utaratibu wa kuomba, kufanya usaili hatimaye kuchaguliwa unaratibiwa na Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambako Mwombaji anaishi na sio Makao Makuu ya JKT”

“Aidha, Jeshi la Kujenga Taifa linapenda kuwasisitiza Wazazi, Walezi na Vijana kuwa nafasi hizo haziuzwi bali zinatolewa bure kwa Vijana wote wa Kitanzania wenye sifa zilizoainishwa katika Taarifa kwa Umma iliyotolewa Makao Makuu ya JKT Chamwino, Dodoma tarehe 25 Agosti 2023, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele anawakumbusha Wazazi, Walezi na Vijana kujiepusha na Matapeli” imeeleza taarifa ya JKT.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…