Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imeitisha jalada la shauri la madai ya mahari lililotolewa hukumu na Mahakama ya Wilaya ya Meatu Machi 14 mwaka huu, kwa ajili ya kulipitia upya.
Mahakama hiyo ya Meatu, Mkoa wa Simiyu iliamuru nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Nkoma mkoani humo, Selemani Mussa (65) kuuzwa ili kulipa deni la Sh1.1 milioni analodaiwa ili kukamilisha mahari ya kijana wake.
Uuzwaji wa nyumba hiyo ni kufikia Sh2.2 milioni walizokubaliana kabla ya ndoa ya kimila kufungwa mwaka 2019 ikiwa ni makubaliano ya ng'ombe 15 kwa thamani ya Sh150,000 kwa kila ng'ombe mmoja.
Julai 28 mwaka huu, Mwananchi Digital iliripoti habari hiyo na kuibua mjadala kwenye maeneo mbalimbali juu ya suala hilo.
Mwishoni mwa wiki Saidi Kisamba anayemuwakilisha mdaiwa Seleman Mussa alisema Mahakama imeliagiza jalada kutoka Mahakama ya wilaya ili kulifanyia kazi, hivyo baada ya kulipitia wanaweza wakatoa maelekezo mengine.
Hukumu ya shauri la madai namba 81 ya mwaka 2020 ilitolewa na hakimu F. F. Madungu ikiamuru kukamata nyumba namba 27 B ya Seleman Mussa iliyopo kijiji cha Nkoma wilayani Meatu mkoani Simiyu kufidia deni la mahari la Sh1.1 milioni kati ya Sh2.2 milioni walizokubaliana.
Akizungumza na Mwananchi Digital Kisamba alisema “Mahakama Kuu ina mamlaka ya kuita jalada la kesi kufanyia mapitio, baada ya hapo litarudishwa mahakama ya wilaya kwa ajili ya utekelezaji kwa amri itakayokuwa imetolewa na jaji.
Alisema alipigiwa simu kutoka Mahakama Kuu akiarifiwa hatua hiyo kwa ajili ya kumtaarifu mteja wake na kwa sasa wanasubiri uamuzi wa Mahakama.
Mwananchi Digital ilizungumza na Seleman Mussa ambaye ni mdaiwa katika shauri hilo alisema Septemba 4, mwaka huu alipokea taarifa kwa njia ya simu akiambiwa shauri lake lipo Mahakama Kuu.
"Niliambiwa kesi yangu imefika kule kwa hiyo nisubiri maamuzi yatakayotolewa na jaji," alisema Seleman.