Rais Samia Suluhu Hassan ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCA).
Hatua hiyo inamfanya Rais Samia kuwa mkuu wa nchi wa pili ndani ya bodi hiyo inayojumuisha wajumbe watano, akiwemo Rais wa Senegal, Macky Shall.
Mbali na marais hao, wajumbe wengine katika bodi hiyo ni Moussa Mahmat ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinumwi Adesina na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Kristalina Georgieva.
Hata hivyo, nafasi hiyo inamfanya Rais Samia kuwa na nguvu ya kupeleka hoja moja kwa moja kuzishinikiza nchi zilizoendelea zitekeleze ahadi ya kutoa fedha za uhilimivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea kama inavyoelezwa na wadau.
Taarifa ya uteuzi huo, imetolewa na Mwenyekiti wa bodi hiyo, Ban Ki-Moon walipokutana na Rais Samia katika mikutano wa wakuu wa nchi kuhusu mabadiliko ya tabianchi, uliofanyika Nairobi nchini Kenya.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Septemba 12, 2023 Meneja wa Mipango wa Shirika la linalojishughulisha na athari za mabadiliko ya tabianchi (ForumCC), Msololo Onditi amesema uteuzi huo ni tija kwa Tanzania.
Tija hiyo inatokana na kile alichoeleza, mkuu huyo wa nchi atakuwa na nguvu ya kuwasilisha moja kwa moja hoja za kuzishinikiza nchi zilizoendelea kutoa fedha za kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa nafasi hiyo atakuwa na sauti ya kupaza kwa nchi zilizoendelea kutoa fedha za uhimili wa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea kama zilivyoahidi,” amesema.
Lakini wadhifa huo, Onditi amesema unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zitakazokuwa na fursa ya kupata taarifa ya fedha za mabadiliko ya tabianchi haraka na kujiandaa kuzipokea.