Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imelikataa pingamizi la mbunge wa zamani wa viti maalum (CCM), Vicky Kamata la kupinga mtoto wa ‘mumewe’, asiteuliwe kuwa msimamizi mirathi na mali za marehemu, Dk Servacius Likwelile zenye thamani ya zaidi ya Sh4 bilioni.
Machi 19, 2016, Vicky Kamata aliyekuwa mbunge kwa vipindi viwili vya Bunge la 9 na Bunge la 10, alifunga ndoa na aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile ambaye, alifariki dunia Februari 19, 2021.
Katika hukumu ya shauri la kuomba kuwa msimamizi wa mirathi ya Dk Likwelile iliyofunguliwa na mwanae, Raymond, iliyotolewa Septemba 15, 2023, na Jaji Augustine Rwizile, amesema Vicky hakuwa mke aliyeolewa kihalali na marehemu.
Kwa hiyo Mahakama imeamuru mali ambazo Vicky alikuwa akipinga kuingizwa katika orodha ya mali za marehemu akidai ziliingizwa kimakosa, zijumuishwe katika orodha ya mali za marehemu.
Mali hizo ni nyumba iliyopo kiwanja namba 116 iliyopo Mbweni, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambayo alisema walichuma pamoja na nyumba mbili zilizopo huko Mpiji Magoe jijini humo kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 9.5 ambayo alidai ana hisa asilimia 50.
Mbali na hizo, ipo nyumba viwanja namba 387 na 389 iliyopo kitalu D Sinza iliyopo kwa jina lake, nyumba iliyopo Kibamba kwa jina la mtoto wake Gloria Likwelile na viwanja namba 318,319,320 na 321 vilivyopo Mpigi Magoe Ubungo.
Viwanja hivyo vinamilikiwa na kampuni ya Beda Group Limited na Beda Farms Limited ambavyo Vicky alidai kuwa na asilimia 50 ya hisa na pia alipinga gari aina ya Toyota Prado namba T731 CQR na pikipiki Toyota namba MC 588 AHT.
Katika hukumu hiyo iliyopatikana katika mtandao wa mahakama jana Jumanne, September 19, 2023, mtoto wa marehemu aitwaye Raymond Likwilile ameteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi na atatakiwa kabla ya kupewa barua, atimize takwa la kanuni namba 66 la mirathi.
Jaji Rwizile alisema tangu kufariki kwa Dk Likwelile familia yake haijawahi kuwa na utulivu ambapo kuliibuka vita ya kisheria kati ya watoto wa marehemu na Vicky aliyekuwa akionekana mke halali wa ndoa wa marehemu.