Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema wameanza mchakato wa kudhibiti matumizi ya shisha ili yeyote atakayeuza awe na kibali na iuzwe kwenye maeneo maalum badala ya kila Mtu kuuza, hii ni baada ya kubaini Wauza shisha wanaichanganya na bangi na unga na kuathiri Watumiaji kwa kupata kansa ya koo na madhara mengine.
Akiongea Jijini Dar es salaam, Lyimo amesema “Shisha tunaifanyia kazi na mchakato upo ili kuidhibiti, yeyote atakayeuza shisha atakuwa na kibali na maeneo maalum sio kila Mtu ataweza kuiuza, wanaochanganya bangi na Heroin kwenye shisha hawatoweza maana itakuwa maeneo machache na tutapima mara kwa mara kuhakikisha hilo halifanyiki”
“Matumizi ya shisha na uchanganyaji wa dawa za kulevya ukiendelea madhara yake ni makubwa sana, tumeshuhudia Watumia shisha wengine wana kansa ya koo, wanavimba makoo, wengine wana kansa ya utumbo mfumo wa hewa ina madhara makubwa ukienda Hospitali za kansa mtakutana nao”
“Watanzania msitumie vitu vya kuiga, mbaya zaidi wanaodanganywa zaidi ni Wadada ukienda klabu kubwakubwa Wadada ndio wanatumia kwa wingi, wengine Mtu kama anampenda Mdada anamsumbuasumbua wanatumia shisha wanamuwekea dawa za kulevya kule mwisho wa siku anaondoka nae tayari ameshaambukizwa magonjwa n.k, lakini pia Mdada akichanganyiwa shisha na dawa za kulevya mwisho anachukuliwa na Mtu ambaye hajawa na mahaba nae”