Makapuku Forum

Mwanzilishi wa Benki ya Access duniani, Herbert Wigwe (57) amefariki dunia kwa ajali ya helikopta iliyotokea California, nchini Marekani.

Benki ya Access yenye makao makuu nchini Nigeria ina matawi katika nchi za Tanzania, Congo, Ghana, Kenya, Uganda, Nigeria, Rwanda, Gambia, Guinea, Cameroon, Sierra Leone, Msumbiji, Botswana, Afrika Kusini, Zambia, Ufaransa na Uingereza.

Katika ajali hiyo iliyotokea juzi Februari 10, 2024 saa nne usiku, wengine waliofariki dunia ni mkewe, mtoto wake wa kiume na watu wengine watatu waliokuwa ndani ya chopa hiyo.

Wigwe ambaye ni mzaliwa wa Ibadan nchini Nigeria, alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Access Holding ambayo ni kampuni mama ya Benki ya Access.

Chopa ya Wigwe ambaye pia ni mmiliki na mwanzilishi wa Chuo Kikuu cha Wigwe, ilikuwa ikielekea Las Vegas kabla ya kupata ajali mpakani mwa Nevada na California, usiku wa Ijumaa.

Mamlaka ya anga nchini Marekani imethibitisha hakuna aliyenusurika katika ajali hiyo na wanaendelea kuchunguza chanzo chake.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Afrika Magharibi, Rais wa Nigeria, Bola Tinubu ameeleza kusikitishwa na ajali hiyo akisema kifo cha Wigwe ni pigo kwa sekta ya benki nchini Nigeria na Afrika kwa ujumla.

 
Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa unatarajiwa kuzikwa Februari 17, mwaka huu kijijini kwao Ngarash wilayani Monduli Mkoa wa Arusha.

Lowassa amefariki dunia Februari 10, 2024 saa 8 mchana katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango jana, Lowassa alifikishwa katika taasisi hiyo baada ya kuugua shinikizo la damu, matatizo ya mapafu na kujikunja kwa utumbo.

Taarifa kuhusu maziko yake, imetolewa leo Februari 11, 2024 na msemaji binafsi wa Lowassa, Aboubakar Liongo nyumbani kwa mwanasiasa huyo, Masaki jijini Dar es Salaam.

Amesema ratiba rasmi ya mazishi itaanza Februari 13, 2024 itakayohusisha taratibu zote za kiserikali.

"Taarifa zaidi kuhusu mazishi itatolewa baadaye, lakini kwa sasa maziko yatafanyika Ngarash Monduli mkoani Arusha siku ya Jumamosi, Februari 17, 2024 saa 8 mchana," amesema Liongo.

 
Rais wa Hungary, Katalin Novak, mshirika wa karibu wa Waziri Mkuu, Viktor Orban, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kutokana na hasira ya umma juu ya msamaha uliotolewa kwa mtu aliyehusishwa na kesi ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto.

Muda mfupi baadaye mfuasi mwingine wa Orban, waziri wa zamani wa sheria, Judit Varga naye alitangaza kuwa anajiondoa kwenye utumishi wa umma kutokana na jambo hilo.

Uamuzi wa Novak kujiuzulu umetokana na shinikizo kubwa kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na maandamano ya wananchi nje ya Ikulu ya Rais Ijumaa jioni.

“Ninajiuzulu wadhifa wangu,” alisema Novak (46), akikiri kwamba alifanya makosa.
“Ninaomba msamaha kwa wale niliowaumiza na waathiriwa wote wanaoweza kuwa na maoni kwamba sikuwaunga mkono,” alisema Waziri wa zamani wa Sera za Familia.

“Mimi niko, nilikuwa na nitabaki katika neema ya kulinda watoto na familia.”
Novak alikuwa mwanamke wa kwanza kushikilia nafasi ya urais katika taifa hilo Machi 2022.

Mzozo huo ulichochewa na msamaha aliopewa aliyekuwa naibu mkurugenzi wa makazi ya watoto. Alikuwa amesaidia kuficha tuhuma za unyanyasaji wa kingono za bosi wake kwa watoto waliowasimamia.

 
Serikali imewahakikishia majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, kuwa inafanyia kazi maoni na mapendekezo yao kuhusu maboresho ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema hayo leo Februari 10,2024 wakati akifunga kikao kazi cha mafunzo ya uelimishaji kwa majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, kanda ya kusini na watendaji wa tume ya usuluhishi na uamuzi (CMA) mjini Songea.

“Mapendekezo ya kuboresha kifungu cha 39 (2) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura 263 kilichoweka ukomo wa muda wa kuwasilisha madai bila kutoa wigo wa kupokea madai hayo iwapo kuna sababu za msingi za kucheleshwa, tumeyafanyia kazi na tunatarajia muswada wa marekebisho kuwasilishwa bungeni hivi karibuni.”amesema Ndalichako

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani aliwahimiza waajiri nchini kujisajili kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), na kutoa taarifa za ajira za wafanyakazi wao ili kulinda haki zao pindi wanapopatwa na majanga wakiwa kazini.

Mkurugenzi wa WCF, Dk John Mduma amesema Mahakama ya Tanzania ni wadau muhimu wa mfuko huo katika utekelezaji wa majukumu yake, kwa kuwa unategemea maamuzi mbalimbali ya Mahakama katika utekelezaji wake wa majukumu ikiwemo maamuzi ya kesi za mirathi.
 
Rais wa Yanga Eng. Hersi Said katika kuadhimisha miaka 89 ya Klabu ya Yanga ametangaza rasmi kuwa Mfadhili wa Timu hiyo Ghalib Said Mohammed (GSM) amekubali kujenga uwanja wa Yanga katika eneo la Jangwani.

“Baada ya mazungumzo ya muda mrefu na Mdhamini na Mfadhili wa Klabu yetu, Ghalib Said Mohammed (GSM), nipende kuwataarifu Wanachama na Mashabiki wa Klabu yetu kuwa leo, GSM ameridhia kwa dhati kushiriki kwenye kufanikisha ujenzi wa uwanja wa kisasa wa Young Africans Sports Club, katika eneo la Makao Makuu ya Klabu yetu, Jangwani, Jijini Dar Es Salaam.

“Nichukue fursa hii kumshukuru sana GSM kwa dhamira hiyo inayokwenda kutimiza ndoto ya Uongozi wangu, Kamati ya Utendaji na Wanachama na Mashabiki wa Young Africans kwa kuwa na uwanja wetu”
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…