Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, leo inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili Miriam Steven Mrita, mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, bilionea Erasto Msuya.
Miriam pamoja na mshitakiwa mwenzake, Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray, wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya kukusudia, wanadaiwa kumuua kwa kumchinja, Aneth Elisaria Msuya ambaye ni wifi yake Miriam.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, Miriam na mwenzake Muyella wanadaiwa kutenda kosa hilo la mauaji ya kukusudia Mei 26, 2016 huko nyumbani kwa Aneth, Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Aneth alikuwa mdogo wa bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi kwa kutumia bunduki ya kivita aina ya SMG eneo la Mijohoroni, Barabara Kuu ya Moshi-Arusha wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.
Hukumu hiyo inayotarajiwa kusomwa na Jaji Edwin Kakolaki aliyeisikiliza kesi hiyo, ndio itakayoamua hatima yao iwapo wana hatia au la.
Na kama wana hatia, adhabu ni kunyongwa hadi kufa na kama hawana, wanaweza kuachiwa huru.
Mpaka leo hukumu hiyo inapotolewa, washitakiwa wameishi mahabusu kwa takribani miaka minane wakisubiri kukamilika kwa usikilizwaji wa kesi, kwa kuwa shtaka la mauaji linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria nchini.