Makapuku Forum

Serikali ya Korea Kaskazini imepiga marufuku wananchi wake kufuga mbwa na kuishi nao kama sehemu ya familia, badala yake wametakiwa kufuga kwa ajili ya kula nyama na kuchuna ngozi yake.

Tangazo la kupiga marufuku ufugaji wa mbwa kama wanyama pendwa wa kuzurura nao mitaani, lilitolewa kwenye mkutano wa Umoja wa Wanawake wa Kisoshalisti wa Korea kwenye jimbo la kusini la Pyongan lililopo kaskazini mwa mji mkuu wa Pyongyang. Korea Kaskazini inaongozwa na Kim Jong Un.

Akizungumza na gazeti la Daily NK la nchi jirani ya Korea Kusini, mmoja wa wanaharakati (bila kutaja jina lake) aliorodhesha makosa ambayo mmiliki wa mbwa anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria na Serikali ikiwamo ufugaji mbwa kama mwanafamilia.

“Kumfanya mbwa kama sehemu ya familia, kula na kulala naye kwenye familia ni kinyume na maelekezo ya serikali na kunatakiwa kuepukwa,” alisema mtoa taarifa.

Pia, alisema makosa mengine ni kumvalisha mbwa nguo, kama alivyofanya Paris Hilton wa Marekani kwa mbwa wake. Paris Hilton aliyezaliwa Februari 17, 1981 ni mfanyabiashara, mwanamitindo, mwimbaji, DJ, na mwigizaji ambaye familia yake ndiyo inamiliki mtandao wa hoteli za Hilton duniani kote.

 
Serikali katika kupunguza uhaba wa usafiri pamoja na msongamano katikati ya Jiji la Dar es Salaam, imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo wa mabasi ya mwendo wa haraka awamu ya pili (BRT 2) Mbagala Rangi Tatu kupita Chang’ombe, Magomeni Mapipa hadi Barabara ya Sokoine ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 98.

Mradi huo wa BRT 2 ni moja ya miradi ya kimkakati 11 ambayo Serikali inaendelea kutekeleza ndani ya Jiji la Dar es Salaam ndani ya miaka mitatu ambapo mitano kati ya hiyo imekamilika huku sita ikiendelea kutekelezwa.

Hayo yamebainishwa Machi 13, 2024 na Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka awamu ya tatu (BRT 3) kilometa 23 katika barabara ya Tanganyika kutoka Karume hadi Buguruni unaendelea pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Mabasi yaendayo haraka awamu ya nne (BRT 4) unaoanzia maktaba ya Taifa – Mwenge – Sam Nujoma kilometa 13.5 ambao unapita pia katika barabara ya Mwenge hadi Tegeta kilometa 15.63.

Pia upanuzi wa barabara ya Morogoro kutoka njia mbili kwenda njia nane kilometa 19 na maegesho ya magari Kiluvya yenye urefu wa mita za mraba 36,000, lengo likiwa ni kuondoa maegesho yasiyo rasmi pembezoni mwa Barabara ya Mandela na hivyo kupunguza foleni zinazoweza kuepukika.

 
Wakati watu waliowateka wanafunzi zaidi ya 250 nchini Nigeria wakitoa agizo la kulipwa ili kuwaachia huru, Rais wa nchi hiyo Bola Tinubu amesema hakuna kulipwa chochote huku akiagiza maofisa usalama kuhakikisha wanafunzi hao wanapatikana haraka.

Awali wanafunzi hao walitekwa wakiwa shuleni wiki iliyopita katika Kijiji cha Kuriga, jimbo la Kaduna, hali iliyosababisha wazazi na ndugu wa wanafunzi hao kutoa taarifa kuwa watekaji wametaka kiasi kikubwa cha fedha ili kuwaachia huru watoto wao.

Inaelezwa washambuliaji waliizingira shule hiyo inayomilikiwa na serikali iliyoko jimbo la Kaduna wakati wanafunzi walipokuwa wanajitayarisha kuanza masomo.

Katika taarifa iliyochapishwa hii leo na Shirika la Habari la AFP, Waziri wa Habari wa Taifa hilo la Afrika Magharibi, Mohammed Idris amesema kwa kuzingatia msimamo rasmi wa Serikali, Rais ameagiza isitoke pesa yoyote.

 
Wakati leo Alhamisi Machi 14, 2024 ikiwa ndio mwisho wa kuondoa kwa hiari namba zilizoongezwa ukubwa ‘3D’ kwenye magari, Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani, limeainisha hatua zitakazochukuliwa kwa mtu ambaye gari lake litabainika kuendelea kutumia namba hizo zilizopigwa marufuku.

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani, Kamanda Ramadhani Nga’nzi, amesisitiza muda wa wiki mbili walioutoa kwa watu kuondoa 3D kwa hiari unaisha leo, hivyo kuanzia kesho Ijumaa Machi 15, wataanza msako utakaohusisha watengenezaji na wanaoendelea kukaidi kuziweka.

Kamanda Nga’nzi amesema miongoni mwa hatua watakazozichukua ni kupiga faini, kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watakaobainika kuendelea kuzitengeneza na watumiaji.

Februari mwaka huu, jeshi hilo lilipiga marufuku matumizi ya namba 3D katika magari kwa sababu sio namna rasmi katika nchi ya Tanzania, badala yake lilielekeza wamiliki wa magari kutumia namba za 2D zilizoidhinishwa na msajili wa magari kupitia mawakala.

Sababu nyingine ya kupiga marufuku 3D ni kwamba namba hizo haziko kwenye mfumo wa Tanzania, kwa kuwa hazina ubora unaotakiwa, zinatengenezwa na watu wasioidhinishwa kuwa mawakala wa namba za magari.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Machi 14, 2024 Kamanda Nga’nzi amesema, “Tukiwakuta wameweka namba za 3D tutaziondoa na kuwataka kuweka namba 2D au kuwaandikia faini ya Sh30,000 makosa ya papo kwa papo kwa kutembea na namba zisizoruhusiwa.
 
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Ombeni Kilawa (43) mkazi wa Kijiji cha Lusese kata ya Igurusi wilayani Mbarali kwa tuhuma za mauaji ya mkewe Happyness Mwinuka(40) kwa kumkata na kisu shingoni .

Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 14, 2024 na kwamba tukio hilo limetokea Machi 13 mwaka huu.
RPC Kuzaga amesema taarifa za awali zimeeleza kabla ya umauti kumkuta Happyness, uliibuka ugomvi kati ya wanandoa hao waliokuwa wakiishi kitongoji cha Masista Kijiji cha Lusese wilayani Mbarali.

Kuzaga amesema baada ya ugomvi huo kudumu kwa dakika kadhaa ndani ya nyumba wanaoishi, ndipo mtuhumiwa alichukua kisu na kumkata mke wake shingoni na kumsababishia umauti

Imeleezwa kuwa uchunguzi wa awali, umebaini chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi baada ya mtuhumiwa kumhisi na kumtuhumu mke wake kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanaume wengine.

Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa jamii hususan wanandoa kuwa wawazi inapojitokeza migogoro ya kiuhusiano, ili kuepuka na matukio ya kuchukua sheria mikononi kwa kufanya mauaji na kuacha familia zikihangaika.
 
Wabunge wa Baraza la Wawakilishi nchini Marekani wamepitisha muswada wa sheria wa kupiga marufuku mtandao wa TikTok nchini humo, iwapo wamiliki wake watakataa kuuza sehemu ya udhibiti wake kwa Marekani ndani ya kipindi cha miezi sita.

Uamuzi huo umepitishwa leo na wabunge wa vyama vyote vya Republican na Democratic, sasa unasubiri uamuzi wa Kampuni ya ByteDance ya China inayomiliki mtandao wa TikTok kukidhi matakwa ya Baraza na ikishindikana muswada utapelekwa kwenye Seneti kutungiwa sheria na atapelekewa Rais Joe Biden kutia saini kuwa sheria kamili.

Baraza la Wawakilishi lina wajumbe 435, wengi wanatoka chama cha Republican ikifuatiwa na Democratic, huku Seneti yenye jumla ya wajumbe 100, wengi wanatoka chama cha Democratic ikifuatiwa na Republican.

Seneti na Baraza la Wawakilishi ndio wanaunda Bunge la Marekani linaloitwa ‘Congress’ lenye majukumu kama vile kutunga sheria, kutangaza vita, kumshitaki Rais na kupitisha wateule wa Rais.

Uamuzi wa kuifunga TikTok utaiondolea Marekani mapato ya matangazo yanayokadiriwa kufikia Dola 8.66 bilioni ikilinganishwa na mapato ya Dola 1 bilioni ya mwaka 2020.

Hata hivyo, uamuzi huo umepitishwa wakati tayari Rais Joe Biden amefanya utambulisho wake wa kugombea tena urais kwa njia ya TikTok, huku baadhi ya wanasiasa wakiwamo wa chama chake cha Democratic na wale wa Republican wakimshutumu kutumia mtandao huo wa China.

 
Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Rodick Msilwa (20) baada ya kumpata na hatia ya kumbaka mtoto wa kaka yake mwenye umri wa miaka 10.

Hukumu ya kesi hiyo namba 1,392 ya mwaka 2024 imetolewa jana Machi 13, 2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Benedict Nkomola.

Akisoma shtaka hilo, Hakimu Nkomola amesema tukio hilo limetokea Desemba 12, 2023 mchana huko Kijiji cha Luholofu, Kata ya Mgololo, baada ya mtoto huyo kutumwa shambani na mama yake kwenda kuchukua maharage, lakini wakati anarudi ndipo alikutana na mshtakiwa na kubakwa.

"Alitumwa shambani na mama yake akiwa na mdogo wake wakiwa shambani waliitwa na mshtakiwa ambaye ni baba yake mdogo.Alimchukulia na kumpeleka kwenye nyasi kisha akamlaza chini na akamvua nguo yake ya ndani akiwa amemziba mdomo ili asiweze kupiga kelele na kumbaka na baada ya kumaliza alimuahidi atampa Sh1,000 pamoja na pipi." ameeleza hakimu huyo.

Baada ya mshtakiwa kusomewa hati ya shtaka lake, alikana kutenda kosa hilo ndipo Mahakama ikaalika upande wa mashtaka kwa ajili ya kuthibitisha shtaka hilo.

Hakimu huyo amesema upande wa mashtaka ulithibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka kwa kuleta mashahidi sita pamoja na kielelezo kimoja cha PF3 cha ofisa tabibu, ambacho kilionyesha mtoto huyo aliingiliwa sehemu zake za siri kwa sababu alikuwa na michubuko.
 
Hahahahaha...kumbe nao wanakula imbwa...km kasai
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…