Jeshi la Polisi linawashikilia na kuwahoji walimu watano tarajali wa mafunzo ya ualimu (BTP) wanaofundisha Shule ya Msingi Mrupanga mkoani Kilimanjaro, kwa madai ya kuhusika na kifo cha mwanafunzi wa darasa la kwanza, Jonathan Makanyaga (6).
Mwanafunzi huyo, mkazi wa Kijiji cha Kimanganuni chini, Kata ya Uru Kusini wilayani Moshi, alifariki dunia Machi 10, mwaka huu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC alikolazwa kwa matibabu, kwa kile kinachodaiwa alichapwa viboko na mmoja wa walimu hao baada ya kuchelewa shuleni.
Inadaiwa Februari 28 2024, mwanafunzi huyo akiwa na wenzake wawili walichapwa na mwalimu huyo (jina halijatajwa) baada ya kuchelewa shuleni hapo akiwamo Jonathan aliyechapwa sehemu mbalimbali mwilini, kisha kuangushwa chini.
Akizungumza na Mwananchi Machi 12, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema mama na bibi wa Jonathan walikwenda shuleni kuhoji kwa nini mtoto wao amerudi nyumbani akiwa na hali hiyo na ndipo walimu waliwapoza na wakashirikiana nao kumpeleka hospitali bila kutoa taarifa polisi.
View attachment 2933475