Kundi la Nchi Saba (G7)na Jumuiya ya Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini (NATO) hivi karibuni kwa nyakati tofauti vitafanya mikutano ya kilele. Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinachukulia makundi hayo mawili kama majukwaa ya kupinga nchi nyingine, kitendo kinachokwenda kinyume na utaratibu halisi wa pande nyingi, na hakitafanikiwa.
Kabla ya kufanyika kwa mkutano wa G7, serikali ya Marekani ilitangaza kwamba, katika mkutano huo, itazindua mpango wa kimataifa wa ujenzi wa miundombinu. Wachambuzi wanaona kuwa, mpango huo unalenga pendekezo la China la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na nia yake halisi ni kuzuia ushawishi unaoongezeka wa China duniani na kudhibiti maendeleo ya China.
Mgogoro wa Ukraine ni mada nyingine muhimu ya mkutano huo wa G7. Mkutano huo uliwaalika viongozi kadhaa wa nchi zisizo wanachama wa G7 akiwemo Waziri Mkuu wa India Narendra Modi kuhudhuria mkutano huo, wakitumai kuzishawishi nchi hizo kubadilisha msimamo wao kuhusu Russia. Madhumuni halisi ya Marekani ni kuongeza nguvu ya kundi lake linaloipinga Russia, ambayo ni “mpinzani wake wa kimkakati”. Lakini vitendo hivyo havitasaidia hata kidogo kutatua mgogoro wa Ukraine, ambao umesababisha changamoto nyingine kwa dunia nzima ikiwemo mfumuko wa bei ya nishati na upungufu wa chakula.
Mada kuu za mkutano wa kilele wa NATO utakaofanyika mara baada ya mkutano wa G7 ni pamoja na kuendelea kuiunga mkono Ukraine, kupitia maombi ya Finland na Uswidi kujiunga na Jumuiya hiyo, na kupitisha wazo jipya la kimkakati la maendeleo ya muongo ujao. Mbali na kuilenga Russia, mkutano huo pia umealika nchi nne zisizo wanachama wa NATO, ambazo ni Japan, Korea Kusini, Australia na New Zealand. Madhumuni ya kufanya hivyo ni kuzishawishi nchi hizo nne kuipinga China.
Hivi leo dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali kubwa ikiwemo janga la COVID-19, kuzorota kwa uchumi, mgogoro ya Ukraine na upungufu wa chakula. Badala ya kuhimiza ushirikiano wa kimataifa ili kutatua changamoto hizo zinazowakabili wanadamu wote, baadhi ya nchi za Magharibi zinazoongozwa na Marekani bado zina wazo la vita baridi, na kuanzisha makundi ya kupinga nchi nyingine. Kitendo hiki kinakwenda kinyume na utaratibu wa pande nyingi, na hakitafanikiwa.