Kudo
JF-Expert Member
- Nov 2, 2017
- 1,821
- 6,119
MALAIKA NDANI YA KIWILIWILI CHA BINADAMU
Desemba 1994, Rapa Tupac Shakur alihukumiwa kifungo jela kuanzia mwaka mmoja na nusu mpaka minne na nusu. Kosa likiwa kumnyanyasa kingono mwanamke mkazi wa Brooklyn, New York, Marekani.
Kesi hiyo ilitokana na tukio la Novemba 19, 1993, mwanamke huyo aliyekuwa na umri wa miaka 19, alidai kuwa alimwamini Tupac kwa sababu ya umaarufu wake, hivyo aliingia naye chumbani kwenye Hoteli ya Le Parker Meridien, New York, lakini wakiwa ndani alimgeuzia kibao na kumnyanyasa kingono.
Tupac alijitetea kuwa mwanamke huyo akiwa na wenzake, walimvamia chumbani na kutaka kumuibia, alipowakabili ndipo walimfungulia mashitaka ya usumbufu wa kingono. Pamoja na utetezi huo Tupac alihukumiwa kifungo jela, ingawa aliachiwa miezi tisa baadaye kwa dhamana ya dola 1.4 milioni, sawa na Sh3 bilioni kwa sarafu ya sasa.
Msingi wa kuandika kumbukumbu ya kesi hiyo iliyomtupa jela Tupac ni tukio la familia moja, mtu na mkewe kumwandikia barua jaji aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, George Wu, wakimweleza umuhimu wa kumsamehe Tupac kwa sababu ni mtu mwema kupata kumshuhudia.
Wanandoa hao, Abdul-Hakim na Diane Torres, walimweleza Jaji Wu kwamba hata kama mahakama ingemtia hatiani Tupac kwa tuhuma alizofikishwa nazo mahakamani, atambue kuwa upo upande bora zaidi wa mwanamuziki huyo ambao unapaswa kuzingatiwa.
Barua hiyo ya familia ya Torres inaweza kukupa maswali; mtu ambaye anatuhumiwa kumdhalilisha mwanamke kingono anawezaje kuwa mwema mpaka familia hiyo ijitokeze kumtetea?
Ni wema gani ambao Tupac aliufanya kwa familia ya Torres mpaka waumie na kumwandikia barua Jaji Wu ili asimpeleke jela? Na je, ni nini hasa ambacho walikiandika ili kumshawishi Jaji Wu kwamba Tupac alikuwa mtu mzuri?
JAWABU HALICHELEWI
Abdul-Hakim na Diane ni wazazi wa Joshua Torres ambaye alikuwa mgonjwa wa ukosefu wa nguvu kwenye misuli (muscular dystrophy), hivyo kusabisha moyo wake uwe mkubwa. Joshua alikuwa shabiki mkubwa wa muziki na filamu za Tupac.
Joshua alimpenda Tupac kwa kila alichofanya. Alikariri mashairi ya nyimbo za Tupac na kuwaimbia marafiki na ndugu zake. Alitazama filamu ambazo Tupac alicheza na kwenda kusimilia. Simulizi kuhusu Tupac hazikuisha kwa Joshua.
Februari 1993, Tupac alitoa albamu yake ya pili, "Strictly 4 My N.I.G.G.A.Z", Joshua alifanya juu chini akaipata, akasikiliza nyimbo zote lakini akatokea kupenda wimbo Keep Your Head Up ambao ulipotoka uliwapa uchizi wanawake wengi hususan Wamarekani weusi.
Oktoba 1993 familia ya Torres iliingia kwenye kipindi kigumu sana. Hali ya Joshua ilifikia wakati mbaya, hivyo Abdul-Hakim na Diane walijitahidi kufanya chochote ili kumpa tabasamu mtoto wao katika nyakati za mwisho wa uhai wake.
Abdul-Hakim na Diane walimuuliza Joshua nini wamfanyie ili apate tabasamu? Joshua akajibu angependa kuonana ana kwa ana na Tupac au ikishindikana basi azungumze naye japo kwa simu.
Tupac alikuwa maarufu mno, mamilioni ya watu walitamani kukutana naye, halafu alikuwa mwenye shughuli nyingi za muziki, vilevile filamu. Sasa mtu wa namna hiyo unampataje? Hilo liliwasumbua sana Abdul-Hakim na Diane lakini walitamani kumuona mtoto wao anatabasamu kabla hajafa.
Abdul-Hakim na Diane waliifuata taasisi ya kufanikisha ndoto za watu, Make A Wish Foundation ili iwasaidie kumuunganisha Joshua na Tupac lakini haikuwezekana. Taasisi hiyo iliwajibu taarifa ni ya muda mfupi na wao waliishi mbali.
Familia hiyo iliishi Aberdeen, Maryland, hivyo walihangaika kila namna kumpata mtu awasaidie kumfikishia ujumbe Tupac ili ikimpendeza apige simu azungumze na Joshua.
Katika kutapatapa, Oktoba 14, 1993, Diane alipiga simu kwenye kituo cha Redio WPGC FM ambacho ni kikubwa na kikongwe Washington DC na Marekani yote. Diane alipopiga simu alizungumza na mratibu wa promosheni, Dawn Scott.
Baada ya WPGC kurusha tangazo kuwa Tupac anahitajika na mtoto mgonjwa ili azungumze naye ampe tabasamu japo kwa saa za mwisho kabla ya kuaga dunia, ulipita muda wa kama dakika 30, Tupac akawa hewani anazungumza na Joshua kwa simu.
Tupac baada ya kupata taarifa kuhusu kiu ya Joshua kuzungumza naye na hali yake ya kuumwa, alipiga simu ya Diane (mama yake Joshua) ambaye ndiye aliacha namba ya simu.
Diane alipopokea simu ambayo mpigaji alijitambulisha kuwa ni Tupac, aliruka kwa furaha, aliona miujiza kwamba hatimaye sauti itakayompa tabasamu mtoto wake yupo nayo kwenye simu.
Huku machozi yakimtoka, Diane alimfuata Joshua aliyekuwa amelala kitandani akiwa dhaifu mno, akamwambia: "Josh, huyu hapa Tupac kwenye simu, ongea naye."
Joshua aliposikia jina Tupac akachangamka ghafla, akapokea simu na kuzungumza kwa furaha. Diane alisema: "Josh alinishangaza, alitabasamu na alifurahi sana kuzungumza na Tupac. Lilikuwa tukio la hisia kali, maana Josh kuzungumza na Tupac kwa simu ilikuwa ndoto kugeuka kweli."
Mazungumzo ya Joshua na Tupac kwa simu yalichukua karibu saa nzima. Joshua alimsimulia Tupac kuhusu ugonjwa wake na jinsi alivyokaribia kifo. Alimweleza anavyompenda na anavyofuatilia nyimbo zake na filamu anazocheza.
Joshua alimwambia Tupac kuwa anaweza kurap nyimbo zote za albamu ya Strictly 4 My N.I.G.G.A.Z, akamweleza wimbo anaoupenda zaidi ni Keep Your Head Up.
Mwisho Tupac alimuuliza Joshua nini amfanyie ili angalau aridhike? Joshua akajibu: "Natamani unitembelee unione na nizungumze na wewe ana kwa ana."
SAFARI YA ABERDEEN
Ombi hilo la Joshua lilimpa wakati mgumu Tupac. Kwa jinsi alivyoelezwa ni wazi kuamka siku iliyofuata yalikuwa majaliwa ya Mungu. Hivyo, Tupac aliona kuwa ili kutimiza matarajio ya Joshua ilipaswa aonane naye siku hiyohiyo.
Tupac alimjibu Joshua kuwa ampe muda aangalie uwezekano wa kusafiri. Tupac alikuwa New York na familia ya Joshua ilikuwa Aberdeen, Maryland, umbali wa kilometa 257. Kwa gari ni safari ya saa 2:40 wakati kwa ndege ni dakika 40.
Baada ya kupiga hesabu na kuona uzito wa ombi la Joshua, aliamua kusitisha ratiba zote kwa siku hiyo. Tupac alimpigia simu Abdul-Hakim (baba yake Joshua) na kumuomba anuani ya makazi yao.
Alipomaliza kuzungumza na Abdul-Hakim, alitafuta ndege ya kukodi. Tupac akiwa na wasaidizi wake walikwea jet na ndani ya dakika 40 wakawa Aberdeen, moja kwa moja wakawasili nyumbani kwao Joshua.
"Ilichukua saa 2 hadi 3 hivi tangu Tupac kuzungumza na Josh mpaka kufanya uamuzi wa kuchukua ndege na kuja Aberdeen kumuona Josh," alisema Abdul-Hakim.
Tupac alifika Aberdeen saa 2 usiku kwa saa za Marekani, Joshua alipomuona alichangamka kama vile anaelekea kupona. Walizungumza na kubembelezana. Kuna wakati Tupac na Josh walilia wakiwa wamekumbatiana.
"Ilikuwa siku ya hisia sana, Josh alirap wimbo mzima wa Keep Your Head Up na nyimbo nyingine. Walikaa pamoja kwa zaidi ya saa moja ndipo Tupac aliaga na kuondoka kurejea New York," alisema Abdul-Hakim na kuongeza:
"Ilichukua dakika 40 mpaka 50 tangu Tupac alipoondoka ndipo Josh akawa amefikwa na mauti, nilimpigia simu Tupac akiwa ameshafika New York, nikamjulisha Josh amekufa, alisikitika sana, ila nilimshukuru kwamba alimpa Josh tabasamu kabla hajakata pumzi ya mwisho."
Kwa tafsiri yoyote ile, maneno ambayo yanaweza kufaa kwa namna Tupac alivyoitikia wito wa Joshua, alivyositisha kila alichokuwa anafanya na kusafiri kutoka New York mpaka Aberdeen, unaweza kuita; uitikio wa kimalaika ili kumpa Joshua tabasamu muhimu na la mwisho kwenye kitanda cha mauti.
Baada ya kifo cha Joshua, Tupac alibadili jina la kampuni yake kutoka Ghetto Gospel na kuiita Joshua's Dream. Yote hiyo ni kumuenzi mtoto ambaye alikutana naye dakika za mwisho kabla Mungu hajamchukua.
Ni kwa sababu hiyo, Abdul-Hakim na Diane hawakukaa kimya kipindi Tupac akikabiliwa na kesi, wakaona wampe ushuhuda Jaji ni kiasi gani mwanamuziki huyo alikuwa mtu mwema, kwani alimfanya Joshua afariki dunia akiwa anatabasamu.
Kwa msisitizo kabisa, Abdul-Hakim aliandika kwenye barua hiyo kwenda kwa Jaji Wu: "Walikuwepo watu maarufu wengine wanne ambao Joshua alisema angependa kusikia sauti zao au kuwaona kabla hajafa, mke wangu alipopiga simu WPGC FM, aliwataja lakini hakuna aliyejibu isipokuwa Tupac.
"Fikiria wote tuliowaomba japo watupigie simu waongee na Josh ili wampe tabasamu lakini hawakujibu isipokuwa Tupac peke yake, akapiga simu saa nzima kuongea na Josh, haikutosha akakatisha kila alichokuwa anafanya na kukodi ndege kuja kumuona. Huyo ni mtu mzuri sana. Tupac ni mtu wa watu."
MTOTO JIMMY NA MFALME ALI
Mwaka 1974 ulikuwa muhimu mno kwa Mfalme wa Boxing, Muhammad Ali. Alikuwa anakwenda kwenye pambano la kurejesha ubingwa wa dunia ambao alipokonywa mwaka 1967 kutokana na uamuzi wake wa kukataa kujiunga na Jeshi la Marekani kwa ajili ya Vita ya Vietnam.
Ali alitoa sababu za kukataa kujiunga kwamba Vita ya Vietnam ilikuwa batili, vilevile alisema kuwa asingejitolea kupigana kwa ajili ya taifa ambalo lilikuwa linaendekeza ubaguzi wa rangi, huku Wamarekani weusi wakinyanyaswa.
Msimamo huo ulisababisha Ali azuiwe kucheza Boxing na kunyang'anywa leseni. Agosti 11, 1970 ndipo Ali alirejeshewa leseni ya kupigana ambayo alipewa na Kamisheni ya Michezo ya Jiji la Atlanta, kazi kubwa ya ushawishi ikifanywa na seneta mweusi wa Seneti ya Jimbo la Georgia, Leroy Johnson.
Septemba 1970, alishinda kesi Mahakama Kuu, ushindi ambao uliilazimisha Kamisheni ya Boxing New York imfungulie na mwezi uliofuata (Oktoba 1970), Ali alipanda ulingoni na kumpiga Jerry Quarry raundi ya tatu (KO), Desemba 1970, Ali alimpiga Oscar Bonavena raundi ya 15 (KO).
Baada ya ushindi huo, Ali alipewa kibali cha kupigana pambano la ubingwa dhidi ya aliyekuwa bingwa, Joe Frazier. Pambano lilifanyika Machi 8, 1971 na Frazier alishinda kwa uamuzi wa majaji wote (unanimous decision). Hilo lilikuwa pambano la kwanza Ali kupoteza.
Mwaka 1972 Ali alipigana mapambano sita na kushinda yote, mwaka 1973, Ali alipoteza pambano lake la pili alipopigwa na Ken Norton lakini waliporudiana Ali alishinda kisha Januari 28, 1974, alirudiana na Frazier na kufanikiwa kulipa kisasi kwa unanimous decision.
Wakati huo Frazier hakuwa bingwa, kwani alitoka kupigwa na George Foreman ambaye alitawazwa bingwa wa uzito wa juu duniani. Baada ya Ali kumpiga Frazier, akapata fursa ya kupigania ubingwa dhidi ya Foreman.
STORI ILIPO
Ali alikuwa anajiandaa na pambano muhimu dhidi ya bingwa Foreman ili kurejesha ubingwa alioupoteza tangu mwaka 1967 na alioshindwa kuurejesha mwaka 1971 alipopokea kipigo cha kwanza katika historia yake ya masumbwi kutoka kwa Frazier.
Ali alikuwa kipenzi cha watoto. Wengi walipenda kumtembelea kumuona anavyojifua. Ali alipenda watoto na aliwaruhusu kuingia kumuona anavyojifua bure. Watu wazima walilipa kiingilio, lakini pesa zote zilizokusanywa ziligawanywa kwa watoto. Hivyo kila mtoto aliyekwenda mazoezini kwa Ali aliondoka amejaa mfuko.
Ilikuwa Mei, Ali akiwa kwenye mazoezi makali akijiandaa dhidi ya Foreman katika pambano lililoitwa Rumble In The Jungle, lililofanyika Kinshasa, Zaire (DRC) Oktoba 30, 1974, alipokea ugeni. Baada ya mazoezi Ali alikutana na mgeni wake kwa mazungumzo.
Mgeni wa Ali ni mtoto aliyeitwa Jimmy, alikuwa mmoja wa waliohudhuria mazoezi ya Ali akisindikizwa na baba yake, lakini akaomba kuzungumza faragha na Ali.
Kwanza Ali alimshangaa Jimmy kwa kofia aliyokuwa ameivaa, akamuuliza: "Mbona umevaa hii kofia?"
Jimmy akamjibu Ali: "Nina kansa ya damu (leukemia), natumia tiba ya mionzi (chemotherapy), hapa nilipo sina nywele kabisa."
Kisha Jimmy akamwambia Ali: "Nimekuja hapa ili kukupa ujumbe ujue ni kiasi gani nakupenda na utambe ni kiasi gani unanifanya niwe mwenye furaha."
Ali alizungumza na Jimmy na kumtia moyo. Walipiga picha ambayo ilikuzwa na kuwekwa kwenye fremu, Ali akaiandika picha hiyo maneno "Kwako Rafiki Yangu Jimmy", halafu akasaini.
Wakati wa kuagana Ali alimnong'oneza Jimmy: "I am going to beat George Foreman. You are going to beat cancer."
Kiswahili: Nitampiga George Foreman. Utaishinda kansa.
Baada ya hapo waliagana. Wiki mbili zilizofuata, wasaidizi wa Ali walipokea ujumbe kutoka kwa wazazi wa Jimmy, wakiomba kama Ali angeweza kumtembelea Jimmy hospitali, maana alikuwa amezidiwa na dhaifu mno.
Saa chache baadaye, Ali akiwa na wasaidizi wake, alifika hospitali. Jimmy alikuwa amelala, pembeni yake kukiwa na ile picha kwenye fremu aliyopiga na Ali. Jimmy alipojulishwa Ali amefika, alichangamka na kumwambia Ali: "Muhammad nilijua ungekuja."
Ali alikuwa mpole maana Jimmy alidhoofika zaidi. Ali alimwambia Jimmy: "Jimmy unakumbuka kile nilichokwambia? Nitampiga George Foreman. Utaishinda kansa."
Ali aliposema hivyo, Jimmy alirusha ngumi kumpiga Ali ambaye hakuikwepa. Kisha Jimmy akasema: "Hapana Muhammad, nakwenda kukutana na Mungu, ila nitamwambia wewe ni rafiki yangu."
Baada ya maneno hayo ya Jimmy, chumba kizima kilipoa, ukimya ukatawala. Ikashuhudiwa Ali akitoa machozi, kisha chumba kizima wote walilia. Mwisho Ali aliaga na kuondoka huku akisisitiza angempiga Foreman, hivyo Jimmy naye aishinde kansa. Jimmy alisisitiza kwenda kuonana na Mungu ili amwambie Ali ni rafiki yake.
AHADI ILITIMIA
Ali alimwahidi Jimmy kumpiga Foreman, akataka na Jimmy naye aishinde kansa, lakini Jimmy alimwambia Ali kuwa lazima aende akakutane na Mungu na kumweleza kwamba Ali ni rafiki yake.
Wiki moja baada ya Ali kuondoka hospitali, Jimmy alikuwa wa kwanza kutimiza ahadi yake. Alifariki dunia. Oktoba 30, 1974, Ali alitimiza ahadi, alimpiga Foreman kwa KO raundi ya nane na kuurejesha ubingwa wa dunia. Kila ahadi ikawa imetimizwa.
Jimmy alifariki dunia akiwa anatabasamu baada ya kuunga urafiki na mtu aliyemhusudu sana. Kwa Ali ilikuwa jambo jema kumpa faraja Jimmy angalau katika siku za mwisho za kuelekea tamati ya maisha yake duniani.
Ali hakuweza kuhudhuria mazishi ya Jimmy kutokana na mazingira magumu aliyokuwa nayo kuelekea pambano lake na Foreman, lakini alituma wawakilishi ambao walishiriki kikamilifu msiba wa Jimmy kwa niaba yake.
Bila shaka, Jimmy kama alivyotimiza ahadi ya kukutana na Mungu na ikatimia, basi hakuacha kuitimiza na ile ya kumwambia Mungu kwamba Ali ni rafiki yake, ingawa inafahamika kuwa Mungu hatetwi, hata bila Jimmy kumwambia tayari alishasikia na alishaona.
MALAIKA NDANI YA BINADAMU
Joshua kwa Tupac na Jimmy kwa Ali, unaona kabisa kuwa malaika anaweza kupatikana kwenye kiwiliwili cha binadamu. Inategemea macho pamoja na tafsiri.
Joshua alimuona Tupac malaika sawa na Jimmy alivyomtazama Ali. Na iwe fundisho kwa kila mmoja kumpa mwenzake tabasamu hasa nyakati ambazo tabasamu linakuwa linahitajika zaidi.
Julai 7, mwaka huu, ulimwengu ulitangaziwa kifo cha mtoto aliyekuwa na mapenzi makubwa na soka, Bradley Lowery, miaka 6. Bradley aliipenda sana Klabu ya Sunderland ya England. Zawadi kuu kwake ilikuwa jezi ya Sunderland.
Bradley alikuwa anaumwa kansa ambayo ilimtesa sana. Bradley alimpenda sana Jermain Defoe ambaye ni straika wa Bournemouth, inayocheza Ligi Kuu England, vilevile Timu ya Taifa ya England.
Defoe alikuwa faraja kubwa kwa Bradley. Alimtembelea hospitali alipolazwa na hata nyumbani. Bradley alipokuwa na nafuu alimtembelea Defoe kwenye mazoezi hata katika mechi, ikiwemo zile za kimataifa, akiichezea England.
Bradley akawa mtoto maarufu mno mpenda soka. Mazishi yake yalihudhuriwa na watu wengi maarufu hususan jamii ya wanasoka. Watu walivaa jezi za klabu mbalimbali ili kumuenzi Bradley kwa mapenzi yake ya soka.
Unaweza kukumbuka mahudhurio hayo ya mazishi au sauti ya Bradley akiimba wimbo "Smile" wa Charlie Champlain, uliopata pia kuimbwa na Michael Jackson, ambao ulisindikiza mazishi yake. Bradley aliimba tabasamu hata kama unaumia au unajisikia kukata tamaa.
Unaweza kuikumbuka sauti ya Bradley tena akiimba wimbo "One Call Away" wa Charlie Puth, ambao nao ulisindikiza mazishi yake. Mimi kumbukumbu yangu ni jinsi Defoe alivyompa tabasamu Bradley mpaka siku ya mwisho, akashiriki kumzika rafiki yake. Defoe akabubujikwa machozi mengi akimuaga Bradley.
Kwa Bradley, alimuona Defoe malaika kwenye kiwiliwili cha binadamu, kama Joshua kwa Tupac na Jimmy kwa Ali. Nawe ukipata wasaa, mpe tabasamu japo mmoja, nawe utakuwa malaika kwenye kiwiliwili cha binadamu.