Jamani mwenzenu ni mgeni ktk safu hii, lakini ukweli ni kwamba nahitaji msaada wa juu ya suala hili la malaria. Tangu mwezi wa saba nasumbuliwa na hii homa, kuna dawa nikitumia nakaa kama wiki moja hivi, halafu hali inarudi tena vilevile. Kila nikienda kupima nakuta nina malaria 2 au 3, tangu mwezi wa saba, haiongezeki wala kupungua zaidi ya hapo. Hivyo wadau kama kuna anayeijua tiba, tufahamishane..!
Pole Dogo Lao....Hii issue ya Malaria sugu inachanganya sana watu na madaktari, hasa kutokana na mgonjwa anavyojieleza. Ni vyema kama mgonjwa yuko ana kwa ana na daktari akamuuliza maswali ili kubaini kama kweli ni Malaria sugu au la.
Kuna vitu watu wanachanganya...kuna Malaria Sugu (sio yule wa jukwaa la siasa), maana yake Malaria imethibitika kwa vipimo (hasa hadubini/microscopy) na kutibiwa kwa dawa sahihi (Mseto au Quinine) na kumaliza dose lakini kipimo cha hadubini kikaonyesha bado wadudu wa Malaria wapo kwenye damu.
Au kuna Malaria new infection (maambukizo mapya) umepata muda si mrefu baada ya kutumia na kumaliza dozi sahihi ya dawa sahihi ya Malaria kwa kurudia maisha yako ya kutojilinda na Malaria.
Au ni tatizo jingine ambalo dalili zake zinafanana na za Malaria lakini si Malaria na hospitali wanashindwa kuthibitsha hilo wanabaki kusingizia Malaria (ili wauze dawa, hii ni common sana kwenye hospitali binafsi, ukipima Malaria mara nyingi utakuwa nayo hata kama ni homa ya mafua!).
Sasa basi....kabla hujasema ni Malaria Sugu (ambayo siamini kama una Malaria Sugu, tangu mwezi wa saba ungekuta tushakuzika (samahani lakini ndio ukweli)), ni vyema ucheck mlolongo mzima wa kuugua kwako tangu huo mwezi wa saba mpaka sasa...una dalili gani, ukaenda hospitali zipi, ukafanyiwa kipimo kipi cha Malaria, ukapewa dawa zipi, ukabadilishiwa na kupewa dawa zipi, ulitumia dozi na kumaliza kama ulivyoshauriwa, ulijisikia afadhali kwa siku kadhaa kabla ya dalili kurudi tena, unajikinga na Malaria? Majibu ya maswali hayo yatathibitisha ni Malaria sugu, au new infection, au ni tatizo jingine na sio Malaria kabisa!
Dawa ya kutibu Malaria (uncomplicated) kwa sasa zenye ufanisi bora kuliko zote duniani ni mseto (Artemisinin Combined Therapy ACT), hapa kwetu kuna ALu (Coartem), DuoCotexcin na brand nyingine kadhaa. Je ulitumia mseto na kumaliza dozi kama ulivyoshauriwa? Bado Tabia ya watu kwenda hospitali na kupewa SP hasa Metakelfin ipo sana, hii dawa ilishashindwa kutibu Malaria kwa kiwango kikubwa sana mpaka kutolewa kwenye muongozo except kwa kina mama wajawazito tu.
Dawa ya kutibu Malaria Kali (complicated) na Malaria Sugu ni aidha dawa za Artemisinin za kuchoma sindano mfano Artemether au Artesunate, au dawa ya kuchoma sindani au dripu ya Quinine. Ambazo unatumia kwa siku chache au kadhaa, kisha unamalizia na dozi nzima ya mseto. Je, ulishawahi kutibiwa hivyo?
Kama majibu ya maswali yangu hayo mawili ni ndio, na bado maabara (yenye technician wa kuaminika) zilionyesha una wadudu wa Malaria kwenye damu...basi una Malaria Sugu, na unapaswa kupelekwa India kwa matibabu badala ya Zitto.