*WASOMI WASEMA MALUMBANO YAO MTAJI KWA UPINZANI
Waandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amepinga kauli ya makamu mwenyekiti wa zamani, John Malecela kwamba, chama hicho kitakuwa na wakati mgumu katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Juzi Malecela alisema CCM itakuwa na wakati mgumu katika uchaguzi huo wa mwaka 2010 kwa sababu ya tuhumu nyingi za ufisadi na baadhi ya wabunge wake kushindwa kutekeleza ilani ya chama hicho ya mwaka 2005.
Kwa mujibu wa Malecela, vita dhidi ya mafisadi ni ngumu kwa sababu ndani ya CCM kuna baadhi ya watu wanaokichafua chama kwa tabia zao za kuungana na mafisadi.
Lakini, Makamba jana alisema ufisadi anaozungumzia Malecela kwamba utakisambaratisha chama hicho mwakani ni wa kufikirika kwa sababu mpaka sasa hakuna mwenye ushahidi unaodhihirisha kwamba fulani ni fisadi.
"Mimi siwajui hawa mafisadi. Hebu wewe nitajie jina la mtu mmoja ambaye una ushahidi kuwa ni fisadi," alisema Makamba.
Alipoulizwa kuhusu baadhi ya makundi ya mafisadi ambayo tayari yameanza kampeni ya kusambaza pesa za kuwaangusha kwenye majimbo wabunge walio mstari wa mbele katika vita dhidi yao, Makamba alisema, "siyo kweli ila ni jambo ambalo linakuzwa tu."
Makamba pia alisema Spika wa Bunge, Samuel Sitta atatetea kiti chake kwenye uchaguzi ujao licha ya mbunge huyo wa Urambo kudai kuwa kuna kundi la wabaya wake limeanza kujipitisha kwenye jimbo hilo kwa lengo la kumwangusha katika uchaguzi ujao.
"Kule (Urambo) nilipita, wananchi wengi bado wanampenda. Hakuna kipingamizi chochote, atashinda tu akiomba tena kugombea," alisema Makamba.
Hata hivyo, Makamba alisema kutakuwa na hali ngumu ndani ya CCM katika uchaguzi ujao wakati wa kipindi cha kura za maoni na kwamba wanaotetea nafasi zao watakuwa na wakati mgumu.
"Upinzani watakaoupata CCM utakuwa ni wa wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama na siyo kutoka kwa vyama vya siasa vya upinzani.
Baada ya mchakato huo wa kura za maoni ambazo zitaiwezesha kupata wagombea wake, CCM watashinda kwa kishindo dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani," alisema katibu huyo wa chama tawala.
Makamba alifafanua kuwa, upinzani katika kura za maoni ndani ya CCM, utatokana na ongezeko la wanachama wenye sifa za kuwa viongozi ambao kimsingi sasa wanajipanga kugombea ubunge.
Alijigamba kuwa CCM ina hazina kubwa ya viongozi wenye sifa, jambo ambalo litawapa wakati mgumu wanachama kuchagua.
Hata hivyo, kauli ya Malecela ilionyesha wazi kuwa, ndani chama hicho mambo si shwari kutokana na kuwepo na vita kali baina ya wabunge wanaojinadi kuwa wanapambana na ufisadi na wale wanaotuhumiwa kuwa mafisadi.
Kundi la wabunge wanaojinadi kuwa wanapambana na ufisadi limekuwa likituhumu kuwepo kwa njama za mafisadi kuhakikisha wapambanaji wote wanashindwa kwenye uchaguzi ujao, huku kundi jingine likionekana kutotaka kujitokeza hadharani.
Kutokana na hali hiyo, Malecela, ambaye ni mume wa Anne Kilango ambaye anachukuliwa kuwa mmoja wa vinara wa vita dhidi ya ufisadi, alisema tuhuma hizo zitawaweka baadhi ya wabunge kwenye hali ngumu katika uchaguzi ujao.
Malecela pia alisema baadhi ya wabunge wamekiweka chama hicho kwenye wakati mgumu kutokana na kushindwa kwenda kwenye majimbo yao na kutofuatilia utekelezaji wa ilani ya chama chao.
Wakati Makamba akieleza matumaini hayo ya ushindi wa CCM mwaka 2010, baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wamesema CCM imepasuka katika makundi matatu na kwamba mpasuko huo unaweza kutumiwa na wapinzani kama mtaji wa kisiasa.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema CCM ya sasa ni tofauti na ile ya Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa imegawanyika katika makundi waliyoyataja kuwa ni ya Mtandao, Mpasuko, na CCM Asili.
Profesa Mwesiga Baregu alisema mpasuko huo ni baraka kwa Watanzania kwa kuwa unaweza kuleta mapinduzi ya uongozi kwa kuwachagua wapinzani.
"Inaonekana kuwa ndani ya CCM kuna mpasuko ambao unaweza kukipeleka chama hicho kubaya na kusababisha kuwakwamisha katika uchaguzi ujao wa mwaka 2010," alisema Baregu na kukishauri chama hicho kujipanga upya na kuondoa makundi hayo.
Alifafanua kuwa kundi la Mpasuko limekuwa likipigia kelele vita vya ufisadi na kuitaka serikali kuwachukulia hatua wahusika.
Alisema kimsingi makundi ya CCM Mtandao na CCM Asili yanavutana kimaadili na mtazamo juu ya uongozi.
"Kundi la CCM Mpasuko likisukumwa na kusaidiwa, linaweza kuingia katika kundi la CCM Asili ambao wanataka maendeleo ya taifa na si kujinufaisha mmoja mmoja," alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, CCM inapaswa kuwa makini katika uchaguzi ujao ikijaribu kujenga utaratibu wa kurudisha imani kwa wanachama kwa kushughulikia matatizo mbalimbali yanayokikabili.
Kauli ya Profesa Baregu iliungwa mkono na Profesa Issa Shivji aliyesema kuwa, ni ukweli ulio wazi kwamba, hali si shwari ndani ya CCM kwa kuwa imeanza kulea makundi.
"Mpasuko upo ndani ya CCM, na hii inaweza kuwa faraja kwa wapinzani kwa sababu watayatumia matatizo ya CCM kama muda mwafaka kwao kupitisha sera zao kwa wananchi, jambo ambalo wanaweza kufanikiwa kupata ushindi, wakati huo ndani ya CCM kunaweza kusababisha matatizo," alisema Profesa Shivji, ambaye ni mwanaharakati wa masuala ya ardhi.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, CCM ina kazi ya kuyarekebisha matatizo yake ili wananchi waweze kurudisha imani kwa chama hicho kikongwe na kwamba, hilo litaweza kusaidia kupunguza mmomonyoko.
Alisema viongozi wana wajibu wa kushirikiana na wananchi wao ili kuhakikisha kuwa wanarekebisha mapungufu yao ili kukisaidia chama kupata ushindi katika uchaguzi ujao wa mwaka 2010.
Juzi, akikabidhiwa na Kanisa la Christian Mission Fellowship vifaa mbalimbali vya walemavu vyenye thamani ya Sh58 milioni, Malecela alionya kuwa, mafisadi wasipodhibitiwa watakisambaratisha chama.
Kuhusu uchaguzi hujao akasema: "Utakuwa mgumu kwa CCM hasa wabunge kwa sababu baadhi yao hawaendi majimboni na hawafuati ilani ya CCM. Ugumu mwingine upo katika suala zima la mafisadi," alisema Malecela na kuongeza:
"Vita dhidi ya mafisadi ni ngumu kwa sababu ndani ya CCM kuna baadhi ya watu wanaokichafua chama kwa tabia zao za kuungana na mafisadi." Habari hii imeandaliwa na Leon Bahati, Hussein Issa na Patricia Kimelemeta.
SOURCE: MWANANCHI.