*ASEMA NCHI INA UFISADI WA KUTISHA, ATABIRI UGUMU KWA WABUNGE 2010
Na Ramadhan Semtawa
SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta amejitosa katika mjadala ulioanzishwa na makamu mwenyekiti wa zamani wa CCM, John Malecela, akisema ufisadi nchini umefikia kiwango cha kutisha kutokana na baadhi ya watu, wakiwemo wanasiasa kuwa na utajiri ambao vyanzo vyake havina maelezo.
Wiki iliyopita Malecela alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa suala la ufisadi litawaweka pabaya wabunge wengi wa CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010, huku akisema baadhi ya wabunge wanaweza kupoteza viti vyao kutokana na kutoenda majimboni na kutofuata ilani ya CCM.
Kauli hiyo iliibua mjadala baada ya katibu mkuu wa chama hicho tawala, Yusuf Makamba kumjibu mkongwe huyo akisema haoni mafisadi wala ugumu kwa chama kushinda mwakani, huku Naibu Waziri wa Kazi Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk Makongoro Mahanga akiibuka na kusema mafisadi ndani ya CCM ni wanne tu.
Jana Spika Sitta, akizungumza na Mwananchi kwa simu akiwa Entebe, Uganda, alisema ufisadi uliopo sasa nchini unatisha na akatabiri ugumu kwa baadhi ya wabunge kurejea kwenye chombo hicho cha kutunga sheria.
"Ahaa... mimi ninachofahamu suala si kusema kuna mafisadi wanne ndani ya chama au wangapi, tunazungumzia suala zima la kuporomoka kwa maadili ya uongozi," alisema Spika Sitta ambaye zaidi ya wiki moja iliyopita aliomba kuongezewa ulinzi akidai kuwa wapinzani wake wa kisiasa wanamuandama, akiwatuhumu kuwa ni mafisadi.
"Unaponiambia sijui kuna mafisadi wanne sikuelewi. Hivi sasa kuna ufisadi mkubwa, watu wana utajiri wa kutisha ambao maelezo yake hayaeleweki.
"Kwa mwanasiasa wa kawaida kuwa na utajiri wa kutisha, inatia mashaka sana."
Sitta, ambaye alijinadi kuwa bunge lake litakuwa la "kasi na viwango" mara baada ya kuvishwa joho la uspika, alisema kuporomoka kwa maadili ndiko kunakofanya kuwepo mafisadi kuanzia ndani ya chama.
"Hivi sasa hakuna miiko ya uongozi ndiyo maana kuna ufisadi wa kutisha, zamani kulikuwa na miiko ya uongozi," alisisitiza.
Aliongeza: "Kwa mfano, mimi nilikuwa mtumishi wa umma kwa miaka 40, lakini nisingeweza kuwa na utajiri kama baadhi ya watu walivyo, sasa iweje mwanasiasa tu wa kawaida uwe na utajiri wa ajabu?" alihoji.
Alisema hata kama wapo wanasiasa wafanyabiashara, bado kuna mashaka na utajiri wao.
"Unaweza kukuta mtu ana magari ambayo idadi yake inatisha; ana majumba mikoani na fedha za ajabu. Utajiri huu unatoka wapi kwa mtu mwanasiasa tu,"alihoji.
Alisema watu siku hizi wanaangalia haki binafsi badala ya maslahi ya umma, ndiyo maana hata baadhi yao hushiriki katika mikabata mibovu ya kifisadi.
"Mtu anachungulia atapata nini katika mkataba fulani, anasahau kabisa maslahi ya jamii,"alisema Spika Sitta.
Kuhusu kauli nyingine ya Malecela kwamba wabunge wa CCM wanaoishi mijini watakabiliwa na wakati mgumu mwakani, alijibu: "Hilo liko wazi.'
Spika alisema siku zote mbunge awe wa CCM au wa chama cha upinzani ambaye haendi jimboni kwa wapigakura wake, ana wakati mgumu kutetea kiti chake.
"Sijui kama wabunge wa CCM ambao watakabiliwa na ugumu jimboni ni wengi au wachache, lakini mbunge yoyote ambaye hayuko karibu na wapigakura wake mwakani atakuwa katika wakati mgumu," alisisitiza.
Alisema kwa kawaida mbunge anapaswa kuwa karibu na wapigakura wake ili kushiriki katika mambo mbalimbali, yakiwemo ya kijamii.
Alisema kuna mambo ya ndani ambayo wananchi wanaamini mtu pekee wa kumweleza ni mbunge, sasa asipokuwa karibu na wapigakura lazima utapata wakati mgumu tu mwakani.
Kuhusu utekelezaji wa ilani ya chama, alisema: "Hilo kwa sehemu kubwa linapaswa kutekelezwa na serikali na imekuwa ikifanyika hivyo, lakini mbunge lazima ufike jimboni."
Pamoja na mambo mengine, Malecela alisema: "Vita dhidi ya mafisadi ni ngumu kwa sababu ndani ya CCM kuna baadhi ya watu wanaokichafua chama kwa tabia zao za kuungana na mafisadi."
Mzee Malecela aliwasha moto huo wakati tayari kukiwa na mvutano mkubwa ndani ya CCM baina ya kambi inayopambana na ufisadi, ambayo imekuwa ikijionyesha waziwazi na ile inayotuhumiwa kuwa ya ufisadi ambayo vita vyake vinaonekana kuwa vya chinichini.
Malecela, mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya CCM, alienda mbali zaidi alipoonya baadhi ya wabunge kwa tabia zao za kutokwenda kwenye majimbo yao na kwamba, hawafuati ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
source......Mwananchi Date::8/10/2009