This is what Malecela said yesterday.
MHE. JOHN S. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru sana kwa kunipa nafsi hii ya kuwa msemaji wa kwanza katika mjadala huu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, kama alivyoiwasilisha leo asubuhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, na kumuhakikishia kwamba Chama Cha Mapinduzi, na watanzania wote watakuwa naye bega kwa bega katika kuona kwamba sera za Chama Cha Mapinduzi, zinatekelezwa kwa ukamilifu kama tulivyozipanga na kwamba sisi Wabunge, tutampa kila ushirikiano. Na lazima niseme hili kweli, kwamba Waziri Mkuu, umeanza vizuri na endelea hivyo. Waheshimiwa Wabunge, ningependa niwarudishe kwenye ajenda ya sasahivi nayo ni hotuba ya Waziri Mkuu, akiwasilisha mapato na matumizi ya Ofisi yake. Kwasababu haya mengine yote yaliyosemwa tunaweza tukayachukua kama ajenda ya siku nyingine, lakini kwa leo tuna ajenda ya hotuba ya Waziri Mkuu. Narudia tena hotuba ya Waziri Mkuu (Makofi).
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, ningependa na mimi niseme moja au mawili. Ninataka kulihakikishia Bunge hili na watanzania wote kwamba Chama Cha Mapinduzi, kamwe hakitaficha maovu. Ya kwamba Chama Cha Mapinduzi, kila mara kitakuwa katika mstari wa mbele wa kuona kwamba uovu unaondolewa katika nchi yetu. Twende kwenye hatua za kweli, nani aliyeyaleta haya mambo ya EPA mara ya kwanza? Alikuwa ni Dokta Chegeni, wa Chama Cha Mapinduzi, kutoka Jimbo la Busega. Halafu jambo la pili nitoe mfano tu juzi hapa nyinyi wenyewe mliona Chama cha Mapinduzi, Mheshimiwa Mbunge wa Same Mashariki amesema kwa nguvu zake zote tunaye Mheshimiwa Mpendazoe Fred Mpendazoe Tungu, Mbunge wa Kishapu amesema kwa nguvu. Kwa hiyo ninataka niwahakikishie hata mimi ninarudia tena, hela za EPA zitarudi, lakini nataka nisem
Mheshimi Naibu Spika, ndiye aliyeyaona maovi haya na yeye ndiye aliyeunda hiyo tume ambayo tunasomewa hapa vipande na akaahidi kwamba itakapokuwa tayari ataileta kwenye Bunge hili tuje tuizungumze kihakika. Sasa mimi nashangaa kwamba kitu ambacho Rais alikiunda na tunamshukuru sana na tunampongeza kwamba alichukua hatua ya Chama cha Mapinduzi kupambana na ufisadi na akasema kwamba hela zote lazima zirudishwe chini ya EPA na ripoti italetwa Bungeni tutaizungumza, sasa wenzetu kama wanataka wangoje naona wanafanya haraka mno ..................................
KUHUSU UTARATIBU
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.
NAIBU SPIKA: Kuhusu utaratibu, naomba nataka kusikiliza kuhusu utaratibu.
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 68.
NAIBU SPIKA: Soma, naomba uisome Kanuni.
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Kama huna kanuni wewe shauri yako. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujua kama ni utaratibu kuzungumzia ................................... (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tafadhali soma.
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nitaisoma wengine hapa hawasomi, Kanuni ya 68 inasema, Mbunge anaweza kusimama wakati wowote na kusema maneno kuhusu utaratibu ambapo Mbunge yeyote ambaye wakati huo atakuwa anasema atanyamaza na kukaa chini, na Spika atamtaka Mbunge aliyedai utaratibu ataje Kanuni au sehemu ya Kanuni iliyokiuka. (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Sasa ndiyo hiyo taja sasa. (Makofi)
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Kanuni ambayo imekiukwa ni Kanuni ya 68 (7) inasema, hali kadhalika Mbunge anaweza kusimama wakati wowote ambapo hakuna Mbunge mwingine anayesema. (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge naomba usipoteze muda, Mheshimiwa Mbunge .............................. (Kicheko/Makofi)
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Mheshimiwa Spika, ngoja ............................... (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kaa chini. (Kicheko/Makofi)
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Mheshimiwa Spika, naomba unilinde nimalize. Kama ni sahihi kuzungumzia mwenendo wa Rais ………………… (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge nimesimama naomba ukae chini. Mheshimiwa Chacha Wangwe Spika akisimama unatakiwa Mbunge ukae chini na Kuhusu Utaratibu ni vizuri ukajiandaa halafu unaenda kwenye ……..……..……, tumeshapoteza dakika tano, kwa hiyo naomba aliyekuwa anazungumza aendelee. (Makofi)
MHE. JOHN S. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninapenda niendelee. Kama nilivyokuwa nikisema CCM kamwe haitalinda ufisadi na tutapambana na ufisadi kwa nguvu zetu zote na mimi nina hakika sisi wote tutamuunga mkono kama Rais wetu alivyosema kwamba hela za EPA zirudi na zitarudi na zisiporudi ni kweli kwamba tutakuwa na haki ya kuuliza kwa nini hazikurudi. Lakini mimi nina imani na Rais wetu na kwamba akishasema yale aliyosema nina hakika yatatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba viti vya Bunge letu vimesimikwa kwa bolt, otherwise kwa hali ya namna hii kusimama tu mtu hata hana pointi na wala hajui ile order ni namba ngapi, katika Mabunge mengine watu huinua viti halafu kuanza kutupiana. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ………………….
KUHUSU UTARATIBU
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Kuhusu utaratibu.
NAIBU SPIKA: Kuhusu utaratibu, kifungu namba gani?
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu namba 64 katika e inasema, hatazungumzia mwenendo wa Rais, Spika, Mbunge, Jaji, Hakimu au mtu mwingine yeyote anayeshughulikia utoaji wa haki isipokuwa tu kama kumtolea hoja mahususi kuhusu jambo fulani. Sasa msemaji alikuwa anamzungumzia Rais na mwenendo wake kuhusiana na suala la EPA.
Je, hajavunja hiyo? (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge naomba mnisikilize, nadhani tunayo kazi kubwa ya kuweza kusoma kanuni. (Makofi)
Kwa hiyo swali la kumzungumzia Rais, anasema Rais ameahidi kwamba anameunda tume ambayo ina miezi sita na alichosema msemaji mimi nimesikia kwamba atakapotoa Rais kama hatujaridhika ndio tutauliza, sasa hapa hajamsema Rais, naomba tuendelee mzee. (Makofi)
MHE. JOHN S. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina matumaini yangu kwamba muda nitaongezwa.
NAIBU SPIKA: Unaongezwa.
MHE. JOHN S. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini huyo ni Makamu wa Mwenyekiti wa Chama cha CHADEMA sishangai, ninaendelea. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningependa kwenda kwenye suala la Serikali la Mitaa, ..................................
KUHUSU UTARATIBU
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Kuhusu utaratibu. (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge naona sasa tunaanza kutumia nyumba vibaya, tunaanza kutumia nyumba vibaya kwa sababu hakuna alichokisema Mzee Malecela toka wakati ule.
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kipo hapa.
NAIBU SPIKA: Wewe siyo Makamu Mwenyekiti.
MHE. CHACHA Z. WANGWE: Mheshimiwa Naibu Spika, maana unamlinda sana, usimlinde zaidi ya mahitaji. (Kicheko/Makofi)
NAIBU SPIKA: Haya tunaendelea, mzee Malecela unaendelea, kwa sababu sasa tunafanya utani ndani ya Bunge hili, naomba tuendelee naona sasa tunafanya utani. (Makofi/Kicheko)
MHE. JOHN S. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kama nilivyokuwa nasema sasa nataka nije kwenye suala la Serikali za Mitaa. Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wenzangu mtakumbuka kwamba tangu mwaka 1974 tulishughulika sana kuunda vijiji na haja yetu ilikuwa kwamba kuwaleta wananchi wetu pamoja ili tuweze kuwapa maendelea, sasa mimi kwanza pendekezo langu la kwanza ningependa nimuombe Waziri Mkuu kwamba aunde katume ka watendaji siyo ka Wabunge hapana, ka watendaji waende wakaangalie hivi vile vijiji tulivyoviunda tukaambiwa viwe na Serikali na Serikali za vijiji zipo lakini je, zinaendesha mambo kama inavyotakiwa? Nia ya marehemu Baba wa Taifa ilikuwa ni kupeleka madaraka kwanza mikoani, wilayani na baadaye vijijini, je, tangu wakati huo ni madaraka gani tumepeleka huko vijijini na hayo madaraka yanatumiwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mimi niseme Mheshimiwa Waziri Mkuu ni hakika kabisa kwamba sasa hivi vijiji vyetu vimekosa watu wa fani ya fedha, wamekosa fani ya fedha kwa hiyo hakuna mtu anayeshughulika na ukusanyaji wa mapato ya kijiji, matumizi yake na kuwaambia wanavijiji kama inavyotakiwa na sheria fedha zilivyotumika. Sasa mimi ningeomba jambo hilo liangaliwe sana, tuliwaahidi wananchi wetu tukiwapeleka vijijini vitu vikubwa vitatu maji, elimu na afya sasa je, tumefika kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningependa nianze kutoa dokezo Mheshimiwa Waziri Mkuu, wanavijiji wamejenga Shule za Msingi katika kila kijiji Tanzania na kwa kweli jambo hilo ni la kujivunia sana na hata tunapotaja takwimu za watoto walioenda darasa la kwanza, waliomaliza kidato cha nne ni kutokana na hiyo kwamba baadhi yao walianza kusoma chini ya mti lakini kwenye kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nadhani ni wakati umefika Serikali iangalie namna ya kuboresha Elimu ya Msingi, Serikali iangalie namna ya kuboresha Elimu ya Sekondari wananchi wamejitolea wamejenga shule, wamejenga nyumba za walimu sasa linapokuja suala hakuna madawati, walimu hawatoshi mimi nafikiri hilo linakuwa ni la kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende upande wa afya, ni kweli kwamba tamko lililotokea hivi karibuni kutoka Serikalini ni kwamba tunataka tuwe na zahanati kila kijiji, mimi nina hakika jambo hilo litawezekana kwa sababu tuliposema tuwe na Shule ya Sekondari kila kata sasa hivi ni kata chache ambazo hazina Shule za Sekondari lakini ningeomba safari hii maadam tumepanga hivyo, basi Wizara inayohusika iwe na vitu vifuatavyo. Kwanza, wananchi watakapoanza kujenga vile vitu ambavyo viko juu ya uwezo wao vitu kama mabati, vitu kama mbao hivi tuweze kuwasaidia na pili, tuhakikishe kwamba watumishi watakaoenda kwenye zahanati hizo waanze kutayarishwa sasa kwa sababu tuna vijiji zaidi ya 10,000 sasa kupata watumishi kwa vijiji vyote hivyo itakuwa ni vigumu kama hatukujitayarisha bado mapema.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningeomba kwamba kwa upande wa vijiji miundombinu, ni kweli sasa hivi mambo haya ya simu za mkononi yanaenea vizuri sana lakini mimi ningeomba hii miundombinu ya simu za mkononi angalau ziende katika kila kijiji kama itawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuje kwenye suala la barabara, nataka kwenda haraka kwa sababu muda wangu mwingi umechukuliwa, mimi nina hakika kama tukiunganisha vijiji vyetu na mabarabara ya kudumu hata suala la usafiri litakuwa jepesi, leo Dar es Salaam wamesema kwamba wao hawataki hivi vi-haice wanasema hivi vinaleta matatizo kwenye mji, sisi vijijini tutavihitaji kwa usafiri kutoka kijiji hadi kijiji lakini kwa sasa hawawezi kuja vijiji kwa sababu mabarabara hayapitiki vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ningekuja kwenye upande wa kilimo, mara nyingi sana tunasema wakulima wetu kilimo chao bado ni kilimo duni, sasa kitaachaje kuwa duni ikiwa leo Mkoa wa Iringa, Mkoa wa Ruvuma, Mkoa wa Mbeya, Mkoa wa Rukwa kila siku kilio chao ni mbolea, kwanza haifiki kwa muda na mbolea haitoshi na nisisitize hasa lile kwamba mbolea haitoshi halafu tunamwambia mkulima ana kilimo duni, sasa hapa sijui ni vipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo nije kwenye suala la mifugo, Mheshimiwa Waziri Mkuu kama kuna watu ambao kwa kweli wamesahaulika katika bajeti zetu mara kwa mara ni upande wa mifugo. Ningependa nisisitize kwamba wakati umefika wafugaji waangaliwe, wengi tunasema wenzetu Botswana wana mfugo mizuri na wanapata bei nzuri, ndiyo lakini ukienda utakuta miundombinu yote maji na kadhalika wanatengenezewa na Serikali, sasa sisi bahati mbaya katika Tanzania mifugo wanastawi katika sehemu zilizo na ukame Dodoma, Singida, Arusha, Shinyanga na kadhalika. Sasa kote humu mimi nilitazamia kama kweli tunataka kuwahudumia wafugaji basi suala la maji lingekuwa ni suala la msingi sana kwa binadamu na mifugo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa madawa, kweli Serikali kama inaweza kutoa ruzuku kwa mbolea basi kwa nini isitoe ruzuku kwa madawa ya mifugo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo ningependa tu kusema ninamshukuru sana Waziri Mkuu kwa hotuba yake tunamtakia kila jema na awe na hakika kwamba tutakuwa naye na tutamsaidia kuweza kufaulu na hasa katika kuleta maendeleo ya wananchi vijiji mwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja mia kwa mia. (Makofi)