Ndugu wana JF naomba tujadili hoja na si watu..........nawasilisha hoja ya Mrema na waandishi wa habari jana dhidi ya Spika
SPIKA WA BUNGE LA TANZANIA MH.SAMWELI SITTA AMEKOSA SIFA YA KUWA MHIMILI WA DOLA
Ndugu Waandishi wa Habari, leo nimewaiteni ili kutoa dukuduku langu kuhusu baadhi ya viongozi wakuu wa nchi wanavyoleta uchochezi ambao unaweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu hapa nchini.
Mimi nikiwa mkereketwa wa amani na utulivu hapa nchini, siwezi kukaa kimya wakati kuna viongozi ambao wanatoa kauli za uchochezi ambazo zinaweza kuhatarisha amani na utulivu.
Nimesikitishwa sana na kauli zinazotolewa na Spika wa Bunge Mh Samweli Sitta ambaye amekaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba kulikuwepo na mipango ya kumfukuza uanachama wa CCM kwa sababu ya msimamo wake kuhusu suala la Richmond.
Mh Spika ameyasema hayo akijua wazi kwamba Bunge la Jamhuri lilishafunga mjadala huo na ni yeye aliyedai kuwa yeyote atakae aanzisha mjadala huo anapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge. Kwa kauli hiyo Mh Spika amekiuka Azimio la Bunge, jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya uongozi.
Aidha Mh Spika anataka kushawishi watu wamuone kwamba anaonewa katika suala zima la Richmond na kwamba huenda pengine serikali ilikuwa inataka kuficha kitu fulani kuhusu suala la Richmond, ndio maana CCM ilitaka kumfukuza uanachama wa CCM. Huo ni uchochezi, ni sawa na kuwapaka matope viongozi wenzake wa chama na serikali.
Akiwa kama Spika wa Bunge anapaswa kuwa mtu wa kwanza kulinda Azimio la Bunge na si vinginevyo.
SPIKA ALIKUWA MWAMUZI NA MCHEZAJI
Tangu mwanzoni mwa mgogoro wa Richmond Mh Spika alionyesha kuwa alikuwa mchezaji na mwamuzi.
Spika kama mwamuzi anayesimamia haki ndani ya Bunge hakupaswa kuonyesha ushabiki au kujionyesha kwamba anaunga mkono upande fulani, alitakiwa asiwe na upande wowote. Lakini yeye alionyesha kabisa kwamba yuko pamoja na wabunge wanaojiita makamanda wa vita dhidi ya ufisadi, hapo tayari ana kundi lake. Na hatimaye alifanya ziara mikoani akifuatana na wabunge hao pamoja na wafadhili wao.
Kwa maana hiyo Spika alikuwa mwamuzi na mchezaji kwa wakati mmoja jambo ambalo ni kinyume na utawala bora.
Spika hadi leo anaendelea kuonyesha ukereketwa wake kwa kusema kwamba alinusurika kufukuzwa CCM lakini bado haogopi, bali ataendelea na mapambano. Na anasisitiza kwa kusema kwamba huo ndio ukweli kwani tatizo lipo wapi?
Hiyo ina maana kwamba ameshaamua kuegemea upande mmoja dhidi ya upande mwingine, wakati yeye akiwa msimamizi wa haki. Je kwa staili hiyo haki itatendeka?
Je, kwa mfano Jaji Mkuu angesema kwamba yeye ni mkereketwa wa vita dhidi ya ufisadi. Je,. watuhumiwa wa ufisadi wangepewa haki yao ya kujitetea mahakamani?
Kwa kauli zake Spika anathibitisha kwamba yeye bado yuko pamoja na wabunge ambao wanajiita makamanda wa vita vya ufisadi. Ambao wanasema hawajaridhika kwa sababu baadhi ya Maazimio ya Kamati ya Bunge bado hayajatekelezwa.
Vile vile kauli za Spika zinawachochea na kuwapa nguvu wanaharakati ambao wanasema wataandamana nchi nzima kupinga jinsi serikali ilivyolishughulikia suala zima la Richmond
JINSI YA KUONDOA MAKUNDI NDANI YA BUNGE
Mgawanyiko ndani ya Bunge hauwezi kuisha kama Spika ataendelea kuwa na makundi. Kwa sababu yeye tayari ameonyesha kwamba ana kundi lake ndani ya Bunge. Na pia ameshindwa kusimamia haki ndani ya Bunge, kwa sababu amekuwa mwamuzi na wakati huo huo mchezaji.
Vile vile analeta migogoro na uchochezi baina ya Bunge na Serikali kutokana na kauli zake. Ili kuleta upendo na mshikamano ndani ya Bunge, na kuondoa migongano na migogoro kati ya Bunge na Serikali, nashauri Mh Spika Sitta ajiuzulu au aondolewe, na asiendelee kuwa Spika wa Bunge lijalo.
Pia namshauri Spika pamoja na hao wabunge wanaojiita makamanda wa vita dhidi ya ufisadi, kwamba endapo hawaridhiki na jinsi serikali ilivyolishughulikia suala la Richmond, wajiondoe CCM, badala ya kuleta uchochezi ambao unaweza kuhatarisha amani na utulivu.