Mama, Mungu akupe umri mrefu uone matunda ya uzao wako

Mama, Mungu akupe umri mrefu uone matunda ya uzao wako

cmomwa

Member
Joined
Jun 19, 2016
Posts
55
Reaction score
8
Isingekuwa rahisi mimi kuendelea kukuona ukiongeza maji kwenye mboga ya mchuzi ili mimi na ndugu zangu yatutoshe kwaajili ya ugali. Isingewezekana mimi kuendelea kukutazama ukifokewa na vijana wadogo unaoweza kuwazaa, eti kisa kukosa hela ya kulipa madeni yao.

Isingefaa mimi kuendelea kukuona na doti moja ya kanga huku godoro jembamba ukilitandika chini kama makazi ya kupumzisha mwili wako. Isingekuwa na maana ya mimi kuwa na jinsia hii, isingekuwa vyema mimi kuzaliwa wa kwanza. Nimekupunguzia mzigo Mama. Mwanao nimekuja kutafuta.

Tangu nifike bado sijapata uwezo hata wa kulipia kodi ya chumba kimoja, naishi kwa rafiki yangu DiCksoNga, maisha duni ya kwangu pakavu.Kwa bahati mbaya lilipo giza totoro si ishara ya mapambazuko tena.
Bado graph yangu inasoma kwenye zero, hakuna hatua ya kwenda mbele niliyowahi kuipiga.

Ooh, Ona sasa nimesahau hadi kukupa salamu, Heshima yako Mama.Naisikia sauti yako haina chembe ya furaha ila bado haijapoteza tumaini.

Hata bila kuniambia nafahamu unaniombea Mama, kwangu kuendelea kuvuta pumzi mpaka leo hii ni miujiza.

Kuhusu uhusika wangu, mwanao kama ulivyonilea, bado nipo vilevile nisiyependa kuishia njiani, kumaliza kila ninachokianzisha. Koo langu bado halijakauka sauti kwaajili ya kubisha hodi mlango wa ndoto yangu.Vidole vyangu vina sugu ya kuendelea kugonga milango ya uthubutu. Ni kweli sijapata lakini bado napambana Mama.

Kuna nyakati naamini huenda labda sikukuaga vizuri, uelekeo wangu umeingia doa lisilofutika na sabuni yeyote ya upako.Nipo kwenye vita ya mchana na usiku, ni kama napishana na nilichokifuata huku, zidisha maombi mama. Na deal na watu wenye fitina mama, kila wakigundua njia ya mkate wangu huwa wanamuua mpishi na kuliteketeza jiko lake.

Mpaka leo sijawahi kutuma chochote nyumbani, si ubahili au labda matumizi ni mengi, hapana, hata hiyo hela kiduchu mimi sina mama.Wadogo zangu usiwaambie haya, Yatawaumiza. Baba mwambie augue pole. Yote haya yafanye ukiwa na tabasamu mama.

Msiache kuniombea, endeleeni kumnyenyekea Maulana. Mimi huenda nina dhambi sana nyingi kiasi cha Mungu kushindwa kunisikiliza. Najua siku moja jasho langu litanilipa, Dada atakwenda shule na mdogo wangu Sanga atapata mavazi, kwa sasa waambie washukuru kwa hiyo pumzi ya bure wanayoimiliki.

Kwenye mazungumzo yetu mengine nitakwambia najishughulisha na nini huku, naogopa lisije likakuumiza zaidi.

Mungu akupe umri mrefu, uone matunda ya uzao wako Mama. Nitarudi.

#Cpmode
 
Back
Top Bottom