Kazi nzuri tuliifanya mimi na maama'ake
Matunda yake si khaba na mwana tukajaliwa
Ndoa kati yetu tuliiogopa kwani ni ndoana
Mwafaka ukafikiwa wa mgawanyo wa majukumu
Lakini matunzo ni ya mtoto na mama'ake atoka wapi?
Mie jukumu langu lawa ni kubeba gharama
Mzazi mwenzangu kazi yake ni malezi tu..
Baada ya kipindi mwenzangu somo kageuza!
Akidai bila kumbeba na yeye malezi hayawezekani!
Lakini matunzo ni ya mtoto na mama'ake atoka wapi?
Bili ya mtoto yabebeka lakini kero za mama'ake zatisha!
Kwani mtoto hana makuu lakini mama'ake ataka mengi!
Mtoto yeye ni wa kulamba celerac lakini ya mama'ake!
Mama'ake ataka atunzwe akidai bila yeye hakuna malezi!
Lakini matunzo ni ya mtoto na mama'ake atoka wapi?
Baada ya purukushani na kasheshe kibao sasa..
Siri sasa yafichuka na mama'ake kashindwa uteja!
Kumbe mwenzangu ana dongo aona kadhulumiwa!
Anipasha khabari kuwa mtoto ni wa kwangu tu!
Lakini matunzo ni ya mtoto na mama'ake atoka wapi?
Mama'ake apasua jipu kuwa jasho langu ni lake pia!
Adai kama tumeweza kuzaa kwanini tusile wote?
Mie simwelewi kwani mwafaka tuliweka sote.
Yawaje sasa anigeuzie kibao bila ya sababu?
Lakini matunzo ni ya mtoto na mama'ake atoka wapi?
Mpangie mwana chumba, ajitenge na mamaye,
hadi apate mchumba, hapa si wewe ni yeye,
tajitenga na ushamba, ka meno na kiseyeye,
VYA MLEVI VISHALIWA, MGEMA ATAPATAPA.
tashibisha vya mlevi, tumbole kuning'inia,
wala huu si uchimvi, wahenga wanatambua,
ngadu wala sii mwivi, mwendowe tu sio nia,
VYA MLEVI VISHALIWA, MGEMA ATAPATAPA.
Mgema atapatapa, zamu imemuwadia,
eti harufu ya papa, ndio anasingizia?
kitaa anajitapa, kama jaji rugazia!
VYA MLEVI VISHALIWA, MGEMA ANATAPATAPA.
kakongorokea mediko, kaponzewa na mwanao!
simchumie viboko, akageuka kideo,
ambebe kwa mbeleko, kama mbege kwa kileo.
VYA MLEVI VISHALIWA, MGEMA ANATAPATAPA.
Kaditama wa aama! sumari nagongomeka,
mwanao kwake mama, utumbo umeungika,
takulaje vya shirima, mwanao macho tumbuka?
KUZIZOA SIFA KWA MWANA, MTUNZE NA MAMAYE.
Rutashubanyuma