Mambo matano yatakayokusaidia kutengeza mahusiano bora ya ndoa

Mambo matano yatakayokusaidia kutengeza mahusiano bora ya ndoa

Joined
May 23, 2024
Posts
15
Reaction score
43
ZINGATIA HAYA ALFAJIRI.
KIJANA JINSI ZOTE.

Nimeiita alfajiri tusiyojua kilichobebwa na mchana wake. Ndio ni alfajiri na mapema ya mahusiano unayoona pengine kuna umbali yataenda na hata kukupeleka kwenye ndoa.

Watu wengi huanguka mwanzo/asubuhi lakini athari huonekana jioni kwa sababu tu mchana hua na hekaheka za kutosha.

Tuangalie Mambo 5, ambayo ukisimama nayo yanaweza kukupelekea kuunda mahusiano bora ya ki' ndoa kutokea huku mwanzoni kabisa mwa uhusiano wa kirafiki na uchumba.

Ndani ya mambo hayo matano usishangae uwepo wa mambo mengine matano. Kiufupi utapata mambo kumi muhimu ndani ya mambo matano niliyokusudia mwanzo, twende kazi!

1. MAONO
Hii ni picha au taswira kubwa ya mbali juu ya jambo fulani. Ki falsafa, maono ni picha halisi ya ndoto aotazo mtu mwenye tamaa chanya ya kizikimbilia. Maono yanaweza kusema kwa niaba ya fikra za mtu. Tuko kwenye dunia inayojitaji kila mtu alete mkate mezani, iwe ki nadharia au kivitendo ila aongeze thamani kwenye maisha ya mwenzake, familia na jamii. Mtu mwenye maono ni mbora kuliko mwenye kauli za kishujaa zisizo hata na mtazamo wenye malengo.

Hapa tusichanganye mambo, kuna mtu ana mipango na kuna mtu ana maono hivi ni vitu viwili ambavyo kiutekelezaji vinaelekeana: kinacholeta tofauti ni kwamba mwenye maono anaweza kuweka malengo hali mwenye mipango anaweza kuahirisha muda wowote na kupanga mingine. Maono yako kiti kimoja na malengo. Vikiwekwa kwenye utekelezaji basi matokeo si jambo la kuuliza. Mtazame huyo binti/mkaka. Ana maono? Yaani kuna mahali anakuonyesha fikirani na unamuona mwenye malengo ya kupambana apafike? Ana mikakati ya ki' malengo ya kutimiza maono yake? Kuna mtu asubuhi anakwambia kajiona akiwa kiongozi mkubwa wa kisiasa huko mbeleni na hiyo ni kiu yake; halafu jioni anaendazake darasani kusomea ufamasia. Maono na matendo ya kuyaendea haviendani hata kidogo.

Ndani ya maono tuangalie,

MTAZAMO WA MAISHA
Baadhi ya watu wanaamini kwamba, maana ya maisha ni kupata furaha na uradhi, huku wengine wakiamini, maana ya maisha ni kutimiza kusudi la juu zaidi la kuufanya ulimwengu uwe mahali pazuri. (Kuifanyia dunia jambo fulani) Huku wengine wanaamini, maana ya maisha ni kuwepo tu na kujionea ulimwengu unaotuzunguka namna unakwenda. Wachache wanasema maisha ni kutafuta, kufanikiwa na kuyaishi mafanikio kwa kuyafurahia wenyewe. Wengine wanaamini kuishi ni kwa ajili ya kutoa walichonacho kwa manufaa ya dunia. Kuna sisi wa ndoto na maono, tunaamini tumekuja kuwa mabadiliko tunayotamani kuyaona hapa duniani.

Hii ni namna watu kwa sababu zao wanavyoyatazama maisha. Kwa tafsiri yangu ndogo mimi kama Eva, Maisha ni swali ambalo majibu yake yapo ndani ya kila mja mwenye uhai. Ukiangalizia majibu kwa mtu sahihi utafaulu, ukiangalizia kwa kilaza umeendaa!

Kwenye mahusiano yoyote, haswa haya ya kuunda familia, MTAZAMO WA MAISHA UNAHUSIKA SANA.
Fikiria tu, maono yako ni kuwa mfanyabiashara mkubwa, lakini unaingia kwenye ndoa na mtu anayeamini ajira ndo mafanikio.... hiyo vita itakuwaje? Yaani pale unapoona FURSA mwenzio anaona ni MATOPE, Utawezana na hili maisha yako yote?

Mtazamo wa maisha ni vile mtu anavyoona au kuyatazama maisha katika hali ya kuwa na kutokuwa sahihi. Mtu anaamua vile anatazama kwa sababu alizochagua kuziamini. Kabla ya kuzama kwenye dimbwi la huba litakaloua maono yako hakikisha mitazamo yenu juu ya maisha inaweza kulandana.

2. IMANI
Imani ni kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Imani sio hisia kama wengi wadhaniavyo, imani ni chaguo la kusadiki. Huyo mtu uliyempenda, je ana imani fulani anayoiamini? Imani zenu zinawiana kwa namna yoyote? Yaani, kuna mahali mnakutana kwenye kipengele cha imani? Iko hivi, mbali na kuwa baadhi yetu tulichaguliwa imani za kuziamini tukiwa wadogo, huku utu uzimani ni sisi tunachagua kuziishi. Sasa unakutana na binti, sio wa imani yoyote nzuri ya kiroho, yaani Msikitini hajulikani, wala kanisani hapamuhusu, unamuaminije? Kweli dadaangu, huyo mkaka ni mweusi, mrefu, ana sikisipaki, lakini hana msimamo wowote wa kiimani wa kiroho una uhakika gani anaweza kukupenda wewe?

Binafsi naamini imani juu ya Mungu humpa mtu msimamo thabiti, kwamba, kama unaweza kumpenda Mungu asiyemuona zaidi wasikia tu habari zake, si ni rahisi zaidi kumpenda mtu unayemuona? Kama unaweza kuziishi amri za Mungu na ukajizuia kutenda maovu, je si rahisi sana kuwa mwaminifu kwa mwenza wako? Imani hutupa udhibiti kwenye kutenda kwa kiasi. Ukiamini kesho itakuja na riziki yake kutoka kwa Mungu ni ngumu mno wewe kumuua mtu upate kitu.

Kwenye imani kuna UTU. Kwenye UTU kuna UPENDO na udhati wa mema.

3. NIDHAMU BINAFSI
Ni udhibiti wa mambo yako kwa uaminifu pasipo shinikizo la mtu wa ziada. Nidhamu ni Adabu. Huu ni utamaduni anaojijengea mtu mwenyewe kwa kuzingatia IMANI yake na MAONO yake. Ni kama kusema mtu mwenye nidhamu ni yule anayejiwekea sheria fulani maishani na kuzilinda. Huthamini sana Muda, huheshimu nguvu na pesa yake anayoitafuta kwa jasho. Mtu mwenye nidhamu binafsi kufanikiwa ni rahisi kuliko kmwenye rasilimali na hana nidhamu.

Kama lengo la kuwa na mwenza wa maisha ni ili mkue pamoja basi ni muhimu sana kumchunguza kama anayo nidhamu binafsi. Lakini pia, jishughulikie wewe upande huo. Hakikisha unayo nidhamu binafsi.
Nidhamu binafsi inatupeleka kwenye.

KIPAUMBELE:
Ni tendo linatofanyika kwa maamuzi binafsi baada ya kuchagua jambo ambalo ni muhimu zaidi kuliko mambo mengine na linalohitaji kutazamwa au kushughulikiwa kwanza.

Ni nini kipaumbele chako? Ni nini kipaumbele cha mwenza wako? Je kuna mahali vipaumbele vyenu vinaoana? Kipaumbele hutokana kwa namna fulani na jinsi mtu anayatazama maisha. Je, anaweza kuweka watu wake wa muhimu kuwa kipaumbele kabla ya vitu? Je kazi yake inakuja baada ya familia? Je marafiki ni chaguo la ziada na familia ni kipaumbele chake? Tazama kwa makini. Kama kipaumbele chako ni hela na chake ni kutafuta hela basi kuna namna mnakutana. Ila kama kipaumbele chako ni ukaribu wa kifamilia kabla ya fedha, mnapishana njiapanda. Tazama kwa makini.


4. UTAMBULISHO WAKE
Yeye ni nani? Anajitambua kama nani? Je ajionavyo ndivyo aonekanavyo. Maneno na matendo vimekutana hapa kwenye utambulisho? Ninamfahamu mwanamke ambaye alimiliki ndoa mbili, moja ya ujanani huko ipo mkoa mmoja na nyingine ya utu uzimani mkoa alikohamishiwa kikazi. Ana majina mawili na yote aliyatumia sehemu mbili tofauti. Huku aliitwa hivi na kule aliitwa vile. Likizo kwa mume mkubwa, akirudi kazini aenda kwa mume mdogo. Zaidi ya miaka 6 Mume mdogo ndo anabaini jina analolijua sio halisi. Mashaka kumzidi akafuatilia. Fikiria tu mtu kala kiapo cha kutenganishwa na kifo na watu wawili. Mambo haya kwa wanawake hutokea kwa nadra ila kwa wanaume tunayasikia kila leo, mtu kaja kutafuta mjini, kaoa hai kijijini kaacha mke wa halali na watoto. Jambo hili limepelekea watu kuuana na kuharibiana kabisa maisha hivyo kwa dunia ya sasa kabla hujaolewa huku mjini omba upelekwe kijijini kwao. Hata akisema walikufa wote, akupeleke ukaone japo mizimu ya kwao. Kuwa na uhakika na utambulisho wa mtu kabla hujazama tukaja kukulowa na ndoano.

Kwenye utambulisho tutazame,
CHIMBUKO/FAMILIA.

Ukimjua mtu vyema kwa utambulisho halisi mapema, utajua chimbuko lake. Ni zipi mila na desturi zao? Wanawachukuliaje wageni kwao? Najua unaoa au kuolewa na mtu mmoja kwenye huo ukoo ila amani yako inategemeana sana na kuujua uhalisia wa familia ili ujifunze namna ya kuendana nao. Ijue familia yake. Angalia ndugu na jamaa yake ya karibu. Tazama maisha yao, ona yote ya msingi ili hata ukija kukaa rohoni ujue ya kushughulikia kwenye dua na sala zako.

Ni hivi, familia zetu zinao uwezo wa kututambulisha kivitendo zaidi. Jua familia, kama kuna kesho yenu pamoja/ndoa basi jifunze namna ya kuishi nayo kwa upendo.

Ukipata kibali ukajua tabia zao, mienendo yao na hapo utaona mitazamo yao juu ya maisha na mambo kadha wa kadha. Utajihakikishia juu ya imani ya mpendwa wako na utaona kwa mapana vipaumbele vyake.


5. MVUTANO WA NDANI
Huo ubavu unaodhani ni wa kwako, unakuvutia? Yaani ukitoa hiyo sura na shepu unahusu nini juu yake? Hebu jipe zoezi la upofu kwa muda kisha jiulize kama anakuvutia? Kuna chaziada ukitoa vile vinavyoonekana kwa macho? Vipi juhusu tabia yake? Vipi kuhusu imani yake? Vipi kuhusu utu wake? Vipi kuhusu moyo wake mwema?
Tafuta huo mvutano wa ndani baina yenu kabla ya hatua yoyote. Kadri tunavyokua vile vya kutamanika kwa kuvitazama huanza kukatisha tamaa, unacho cha kujshika nacho kwa huyo mwamba?

Hebu tutazame UPENDO
Situlikubaliana upendo ni hisia nzuri, hisia za kujali na kuthamini? Na tunaambiana kila leo huwezi kutoa usichonacho kwa hakika? Haya, UPENDO ni lazima uanzie ndani ya mtu juu yake yeye mwenyewe. Je mubebi wako anajipenda? Anawapenda wale aliowajua kabla yako, (kuijua familia ni muhimu). Ni hivi, mtu ambaye hajatawaliwa na maisha ya upendo ni ngumu kukipenda na kupenda wengine. Wachache hujifunza kwa kigezo cha kutoipenda zamani yao ila wapo walioona maisha yasiyo na upendo ndo fungu lao. Yuko wapi mpenzi wako? Tambua hili mapema.

Kusema unahitaji mtu wa kukupenda hakikisha unajipenda na huyo uliyekutana naye anajipenda. Mvua dalili yake manyunyu. Ni aheri uingie ndoani ukiwa unajua huyu mtu ni mwema ni vile tu hajafundishwa/hajajifunza kupenda. Utaweza kuona ni namna gani utaenda naye kuliko kuwa na matarajio ambayo hayatokaa yatokee. Upendo una matunda yake, nayo ni yale mema

Upendo wa kindoa una jambo moja ambalo halizungumziwi sana, na ni muhimu mno jamani.
Wanandoa walio fanikiwa hapa wameishi pamoja na kufanikiwa pamoja. Juzi naperuzi mtandaoni nilikutana na chapisho la mwandishi Japhet Nyangoro, aliweka picha akiwa na mke wake akaandika, "NIKIFANIKIWA NI KWASABABU NILIKUSIKILIZA, NA NISIPOFANIKIWA NI KWASABABU NIMESHINDWA KUKUSIKILIZA"

Neno lilinikaa hili, acha tu. Nikajiuliza ni wanandoa wangapi wanathamini KUSIKILIZANA?

Ni hivi, mkishindwa kusikilizana wakati wa urafiki na uchumba, hamtosikilizana kwenye ndoa. Ni nyie nyie mtaingia kwenye ndoa. Kitakachowabadilisha sio ndoa ni maamuzi yenu ya kubadilika mapema ama kuwa na ndoa isiyo na furaha. Asikwambie mtu, kuishi na mtu anayekupinga kwenye kila wazo, ni kasheshe.

Hayo ni machache niliyoamua kuyapa kipaumbele na kukuambukiza rafiki yangu kwa siku ya leo. Ni mimi mimi kungwi wa kisasa.

Karibu sana. Nitaleta sehemu ya pili ya andiko hili.
 
Wadau hawataki kutoa comments kwenye uzi
 
Back
Top Bottom