Mambo ya msingi unayopaswa kuyafahamu kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii kibiashara (1)

Mambo ya msingi unayopaswa kuyafahamu kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii kibiashara (1)

Status
Not open for further replies.

Sam Gidori

Senior Member
Joined
Sep 7, 2020
Posts
165
Reaction score
417

Mitandao Kibiashara.png

Kwanini Unahitaji Mitandao ya Kijamii katika biashara yako?

Mitandao ya Kijamii imekuwa kiungo muhimu katika miaka ya hivi karibuni tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma, hasa katika ulimwengu wa biashara ya mtandaoni ambao umewawezesha wafanyabiashara kuwafikia mamilioni ya wateja kwa urahisi kote duniani. Takwimu zinaonesha kuwa kuna zaidi ya watu bilioni 3.5 duniani wanaotumia mitandao ya kijamii, sawa na asilimia 45 ya watu wote duniani na idadi hiyo huongezeka kila siku.

Kwa mfanyabiashara, hii ni fursa ya kujipatia wateja na kuongeza soko la bidhaa au huduma yako. Zipo sababu nyingi za kukufanya uiamini mitandao ya kijamii na kuifanya kuwa sehemu ya biashara yako. Baadhi ya faida 10 za kutumia mitandao ya kijamii kukuza biashara yako ni pamoja na:

1. Kuwafanya wateja kuelewa zaidi biashara yako
Mitandao ya kijamii ni moja kati ya njia zenye manufaa makubwa katika kutangaza biashara yako kwa urahisi na kuwafanya wateja wako kuifahamu biashara yako. Unachopaswa kufanya ni kufungua akaunti katika mitandao ya kijamii kwa kutumia jina la biashara yako na kuanza kutangaza biashara yako kwa wateja wako. Utafiti unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wafanyabiashara wamekuza jina la biashara zao baada ya kutumia saa kadhaa kila siku mitandaoni kutangaza biashara zao.

2. Gharama ndogo
Karibu mitandao yote ya kijamii inaruhusu kufungua akaunti na kuiendesha bila gharama yoyote. Lakini unaweza kulipia huduma ya matangazo ya biashara yako ili kuwafikia watu wengi zaidi. Ni vyema kulipa kiasi kidogo cha pesa unapoanza kutumia huduma ya matangazo mtandaoni ili kujiridhisha na kiwango cha ufikiwaji wa wateja na kupangilia tena malengo yako.

3. Kuongeza ukaribu na uaminifu na wateja
Mara zote, mrejesho kutoka kwa wateja ni mbolea katika kuhakikisha biashara yako inakua. Mitandao ya kijamii ni njia bora zaidi ya kupata mrejesho kuhusu bidhaa au huduma unayowapatia wateja wako, ikiwa wanafurahia au kuna malalamiko yoyote; unaweza kupata kwa wateja kutoa maoni katika machapisho yako au kuja moja kwa moja 'inbox' na ni rahisi wewe kuyajibu malalamiko au maoni yao moja kwa moja.

Baadhi ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook inatoa uwanja wa kuandika mrejesho, ambapo wateja hutoa mrejesho kulingana na huduma au bidhaa iliyotolewa. Mrejesho chanya kutoka kwa wateja wako huweza kuwachochea wateja wengine kununua bidhaa au huduma kutoka kwako.

4. Kuongeza kuridhika kwa wateja
Mitandao ya kijamii inachukua sehemu kubwa ya mawasiliano ya moja kwa moja kati yako na wateja wako. Unaweza kutumia mitandao ya kijamii si tu kwa kukuza mwonekano wa biashara yako, lakini pia kwa kuhakikisha kuwa wateja wako wanapata huduma ya kuridhisha. Unapopata maoni ya wateja wako katika machapisho yako au kwa ujumbe wa moja kwa moja, haupaswi kuwajibu kwa ujumbe wa 'kiroboti,' badala yake, ni vyema ukawaandikia ujumbe unaomlenga mteja moja kwa moja ambao, mara nyingi, hupokelewa vyema zaidi. Utafiti wa Jarida la Forbes unaonesha kuwa asilimia 71 ya wateja walioridhika na huduma ya biashara mtandaoni wanaweza kupendekeza huduma au bidhaa hiyo kwa rafiki au familia zao.

5. Kufahamu mahitaji ya wateja wako
Njia bora ya kufahamu mahitaji ya wateja wako ni kwa kuwasiliana nao moja kwa moja, na mitandao ya kijamii imekuwa sehemu nzuri zaidi ya kuwafanya wateja wako kukufikia moja kwa moja kwa njia rahisi zaidi. Kwa kupitia maoni ya wateja wako, unaweza kupata ufahamu wa mahitaji yao kwa namna ambayo usingeweza kufahamu bila uwepo wa mitandao ya kijamii. Mitandao ya kijamii inaweza kukusaidia kuwaelewa wateja wako kwa kuangalia umri wao, kipato chao, sehemu wanazoishi, nk. Ukipata wafuasi wa kutosha, unaweza kutumia vifaa maalum kufuatilia mgawanyiko wa wateja wako katika mitandao ya kijamii.

6. Kuongeza idadi ya watu wanaotembelea tovuti yako
Faida nyingine kubwa ya mitandao ya kijamii ni kuwavutia wateja kutembelea tovuti yako, kwa kuwapa sababu ya kutembelea tovuti yako pale unapochapisha kutangaza bidhaa ambayo taarifa zake zinapatikana kwa undani katika tovuti yako. Kadiri utakavyoendelea kusambaza bidhaa bora katika mitandao ya kijamii ndivyo unavyowavuti watu wengi zaidi kutembelea tovuti yako.

Kama hiyo haitoshi, mitandao ya kijamii inasaidia kufanya tovuti yako ionekane kwa haraka katika utafutaji (Search Engine Optimization au SEO). Tovuti zinazopata wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii zinasaidia kujumuisha wingi wa utafutaji hivyo kupata nafasi kubwa ya kuonekana zaidi katika matokeo ya utafutaji.

7. Kufikia wateja wengi, hata walio mbali
Mitandao ya kijamii inakupa fursa ya kuwafikia wateja waliopo nje ya eneo la kijiografia la biashara yako. Bila uwepo wa mitandao ya kijamii, utalazimika kufungua matawi katika maeneo mbali nae neo lilipo kituo chako cha biashara kwa ajili ya kuuza bidhaa au kutoa huduma kwa wateja waliopo katika maeneo hayo. Lakini uwepo wa mitandao ya kijamii umeondoa kizuizi cha mipaka ya kijiografia, sasa unaweza kutangaza biashara mtandaoni, kuwasiliana na mteja na kumfikishia huduma pale alipo. Hii ni faida si tu kwa kupata wateja wengi, lakini kuongeza fursa ya kibiashara katika maeneo mapya utakayoyahudumia kibiashara.

8. Kupunguza gharama za uanzishaji biashara
Mitandao ya kijamii imerahisisha uanzishaji wa biashara, hasa kwa watu wenye kipato kidogo. Ili kuanzisha biashara rasmi, utahitaji gharama kubwa na rasilimali za kutosha, ikiwamo eneo la kibiashara, kodi ya fremu, msimamizi wa biashara, usafiri wa kwenda na kurudi kutoka eneo la biashara, nk. Lakini kwa kutumia mitandao ya kijamii, unaweza kufanya biashara kiganjani mwako ikiwa tu utakuwa na uaminifu kwa wateja wako. Mitandao ya kijamii imegeuka maduka ya kidigitali ambapo unaweza kuonesha bidhaa zako, kukubaliana bei na wateja wako na kufanya biashara kwa gharama nafuu.

9. Kuwezesha kufanya biashara muda wote (hata usiku)
Tofauti na biashara ambazo huwa na muda wa kazi, ambao ni muda wa kufungua kituo cha biashara hadi muda wa kufunga, biashara katika mitandao ya kijamii haina kizuizi cha muda wa kufanya kazi. Unaweza kuwasiliana na wateja wako na kufanya biashara hata usiku. Hii huongeza ufanisi katika biashara, bila kusahau faida utakayoipata kwa kufanya kazi ndani ya muda wa ziada.

10. Kukuwezesha kufanya shughuli Zaidi ya moja (ajira na biashara, biashara Zaidi ya moja)
Pale utakapokuwa na kituo cha biashara, unaweza kulazimika kuuza aina moja ya bidhaa katika kituo kimoja cha biashara. Lakini mitandao ya kijamii inakupa uwezo wa kuendesha biashara zaidi ya moja kwa kutumia kifaa kimoja: simu yako ya mkononi. Mitandao ya kijamii, mfano Facebook, inakuwezesha kuendesha zaidi ya ukurasa mmoja kwa kutumia akaunti moja. Utahitaji kuwa na program (app) ya Facebook Pages Manager kwa ajili ya kuhakikisha kurasa zako zote zinafanya kazi sawasawa.

Kama hiyo haitoshi, kufanya biashara mtandaoni kunakuwezesha kuendelea kutekeleza majukumu mengine bila kulazimika kuwepo katika kituo cha biashara, mfano, unaweza kuwa umeajiriwa huku ukiendelea kuendesha biashara yako mtandaoni, kwa kuwa mawasiliano yote ya kibiashara yanafanyika mtandaoni. Hii itakusaidia kuweza kufanikisha shughuli zingine huku bila kukwamisha mwenendo wa biashara yako, hivyo kukuwezesha kuwa na zaidi ya njia moja ya kujipatia kipato.

Ukiangalia mitandao ya kijamii kwa jicho la kibiashara, ni wazi kuwa faida inayoweza kupatikana kwa matumizi sahihi ya mitandao hiyo haiwezi kupuuziwa. Kama haujaanza kutumia mitandao ya kijamii kwa matumizi ya kibiashara, haujachelewa. Sasa umeelewa faida za kutumia mitandao ya kijamii kibiashara.

Katika sehemu ya pili ya makala haya, tutaangazia mambo ya msingi ya kufahamu kabla haujaanza kutumia mitandao ya kijamii kibiashara, ikiwamo uchaguzi wa mtandao wa kijamii wa kuutumia kulingana na mahitaji yako kibiashara.
 
Upvote 2
Status
Not open for further replies.
Back
Top Bottom