UTPC
Journalists' Union
- Apr 17, 2026
- 51
- 38
Kwa mujibu wa tafiti za kilimo za mwaka 2023/24 zilizochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mnamo Oktoba 16, 2025, tani 968,910 za ndizi zilizalishwa nchini. Kati ya hizo, tani 968,156 zilizalishwa na kaya na tani 754 zilizalishwa na mashamba makubwa, huku mkoa wa Morogoro ukizalisha tani laki tatu. Takwimu hizi zinaonyesha wazi uzito wa kiuchumi uliopo hatarini iwapo hatua za makusudi hazitachukuliwa kuokoa zao hili.
Nguvu ya Sheria na Maeneo ya Karantini
Ingawa ugonjwa wa BBTV hauna dawa wala chanjo, wataalamu wa afya ya mimea, tafiti za kisayansi, na wadau wa maendeleo wanakubaliana kuwa unaweza kudhibitiwa kikamilifu na kutokomezwa iwapo Waziri mwenye dhamana ya kilimo atasaini kanuni za mkakati wa kudhibiti BBTV.
Kusainiwa kwa kanuni hizo kutasaidia kutekelezwa kikamilifu kwa kifungu cha 45(3)(a) cha sheria ya afya ya mimea ya mwaka 2020 na kutangaza rasmi maeneo yaliyoathirika kama vile Bigwa, Kauzeni, na Mzinga kuwa maeneo ya karantini. Hatua hii itatoa nguvu za kisheria kwa maafisa kilimo kuzuia usafirishaji holela wa miche kutoka au kuingia katika maeneo hayo.
Hivi sasa, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ina miundombinu msingi, ikijumuisha wakaguzi wa afya ya mimea katika kanda saba na vituo vya mipakani 35, huku ikishirikiana kwa karibu na wadau wa maendeleo na utafiti kama Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Chama cha Kilimo Hai (TAHA), Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA), pamoja na Halmashauri za wilaya. TPHPA pia ina maabara katika makao makuu na ofisi za kanda.
Mkulima Mohamedi Shuffernoor kutoka Kata ya Mzinga, Manispaa ya Morogoro,
akiwa katika shamba lake alilotoa migomba na kupanda maharage.
PICHA: FARIDA MANGUBE
Lyimo anafafanua kuwa, “bado serikali haijakubali kuwa ugonjwa wa BBTV ni dharura ya kitaifa. Anasisitiza kuwa kuna haja kwa serikali kutenga rasilimali za kutosha za ndani kupambana na ugonjwa huu, kwani hadi sasa sehemu kubwa ya fedha za udhibiti zinatoka kwa wafadhili kama vile Shirika la Kimataifa la Marekani la Misaada ya Maendeleo (USAID), jambo linalohatarisha uendelevu wa vita hii kutokana na uhaba wa rasilimali za kuwezesha udhibiti wa kina”.
Sambamba na hilo, Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) ikishirikiana na TPHPA zinapaswa kuanzisha operesheni kali za kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wauzaji wa miche kiholela wanasajiliwa na kuthibitishwa kisheria.
Suluhisho la kisayansi na teknolojia ya kidijitali
Mbali na utengaji wa bajeti na usimamizi wa sheria, majibu ya kisayansi na matumizi ya teknolojia ya kidijitali ni nguzo kuu katika kukata mnyororo wa maambukizi ya kirusi cha BBTV. Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Idara ya Sayansi ya Mimea, Vipando na Kilimo cha Bustani, Dkt. Beatrice Mwaipopo, anaeleza kuwa wataalamu tayari wameanza kuchukua hatua za kimfumo ili kusaidia utambuzi wa mapema wa ugonjwa huo kabla haujasambaa kwa kasi.
Pia soma ~ Biashara Holela ya Miche ya Migomba Inavyowazamisha Wakulima
Dkt. Mwaipopo anabainisha kuwa SUA, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo likiwemo Shirika la USAID, ilipokea ufadhili kupitia mradi wa PlantVillage, ambapo watafiti walitembelea wakulima moja kwa moja kwenye mashamba yao, hususani katika mkoa wa Kigoma uliokuwa umeathirika vibaya.
“Kupitia mradi huo, wakulima walipewa mafunzo ya kijiografia na kiufundi jinsi ya kutambua dalili za ugonjwa wa Fungashada kwa kutumia simu zao za mkononi,” alisema.
Akimulika mkakati wa baadaye wa chuo hicho, Dkt. Mwaipopo anasisitiza kuwa SUA inaendelea na tafiti za kutafuta suluhu ya kudumu ya ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mifumo na programu mbalimbali za simu (Mobile Applications) za utambuzi wa magonjwa ya mimea.
Pia soma ~ Mamilioni yanapotea Shambani Serikali Inasubiri ‘Dharura’ Itangazwe
“Mfumo huu wa kidijitali utamwezesha mkulima kubaini ugonjwa na kuchukua hatua za awali za kujihudumia akiwa shambani kwake, kabla hata ya kufika afisa ugani,” alisema.
Elimu ya ugani na mabadiliko ya tabia kwa wakulima
Mohamedi Shuffernoor, mkulima kutoka Kata ya Mzinga Manispaa ya Morogoro, anasisitiza kuwa elimu endelevu ya ugani inapaswa kutolewa mara moja kwa wakulima ili kuwajengea uwezo wa kutambua na kudhibiti kirusi cha BBTV. Shuffernoor anawashauri wakulima wenzake kusitisha mara moja upandaji wa migomba kiholela hadi pale suluhisho la kitalaamu litakapopatikana, au badala yake watumie miche bora iliyothibitishwa na wataalamu.
Naye mkulima Steven Mwita anasema suluhisho la muda mfupi kwa wakulima ni kung’oa migomba yote iliyoathirika ili aanze upya.
Alisema kwa upande wake kauli hiyo ameiekeleza kwa vitendo kwani ndiyo suluhisho kwa sasa ambapo ameamua kung'oa na kuteketeza migomba yote iliyoathirika shambani kwake.
“Badala ya kuacha masalia ya virusi vya BBTV yakiendelea kuzaliana, niliamua kubadili matumizi ya ardhi kwa kupanda mazao ya mbogamboga, hatua inayosaidia kukata mnyororo wa chakula kwa wadudu vidukari wanaosambaza kirusi hicho, huku ikiacha shamba likiwa salama kabla ya kurejea tena kwenye kilimo cha ndizi,” alisema Mwita.
Uzoefu na ushauri wa wakulima hawa unathibitisha kuwa kutoa elimu ya ugani na kuhamasisha mabadiliko ya tabia ndiyo suluhisho la msingi kwa ngazi ya chini.
Akiongezea mtazamo wa kijamii, Afisa Uhusiano na Utetezi wa Shirikisho la Wakulima Wadogo (SHIWAKUTA), Tomas Laiza, alisema lazima shirikisho hilo litoke kwenye ukimya na kuanzisha kampeni kabambe ya kuhamasisha wakulima kuacha kuazimana au kununua miche mtaani bila kibali cha ubora kutoka TOSCI.
Ushiriki wa sekta binafsi na taasisi za fedha
Kufanikiwa kwa vita hii kunahitaji mtaji na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa maendeleo na sekta binafsi. Mashirika yasiyo ya kiserikali na kampuni za pembejeo za kilimo zinapaswa kuwekeza katika ujenzi wa vitalu bora vya miche (Certified Nurseries) karibu na wakulima wa vijijini.
Nkani David Waziri, Mkurugenzi wa Mipango wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), anapendekeza kuwa taasisi za kifedha zishirikiane na makampuni ya bima kubuni bima ya majanga ya magonjwa ya mimea, ili kuwalinda wakulima wanaopata hasara kubwa wakati wa kuteketeza mashamba yao yaliyoathirika.
Tanzania Bila BBTV
Ikiwa wizara ya kilimo, TPHPA, TOSCI, SUA, na Halmashauri za wilaya zitafanya kazi kwa pamoja kunusuru kilimo cha migomba, kasi ya kusambaa kwa virusi vya BBTV itapungua kwa kiasi kubwa. Hatua hiyo haitaokoa kipato cha mamilioni ya wakulima, bali pia italinda usalama wa chakula na utulivu wa uchumi wa familia nchini.
ANDIKO LA: Farida Saidi Mangube, Morogoro
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.