Sisi wengine si wachambuzi bali wapenda soka, tuwekeze kwenye vipaji na wanaoweza kundeleza hivyo vipaji na si kwenye ndumba, tuachane na uchawi, kurogana, kufanyiana hujuma zozote katika soka, kusiwepo na kuhonga marefa au baadhi ya wachezajai wa timu pinzani, sijui kamati ya roho mbaya au kamati ya ufundi zipe jina lolote lile hazina tija kwenye maendeleo ya soka letu. Na wachezaji wetu wacheze mpira wa kistaarabu na si mpira wa kuumizana na kumfanya mchezaji akae nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha. Viongozi waliyopewa dhamana ya kuongoza taasisi zetu za mpira wafanye kazi zao kwa nia ya kuendeleza soka na si kupendelea timu wanazozishabikia au kukandamiza timu wasizozipenda. Mkufunzi Gamondi ni kocha ambaye ataleta mageuzi makubwa kwenye soka letu la Tanzania, kwani kila timu sasa itakapocheza na Yanga itabidi wafanye juhudi kubwa za kimbinu, fitness za wachezaji kuhakikisha wanaweza kuwamudu Yanga kwa dakika 90.