Kakke
JF-Expert Member
- Dec 4, 2010
- 1,883
- 1,482

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula
MWELEKEO wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mabadiliko ya muundo mpya wa Serikali ya Muungano, ni wa kuwa na Serikali moja, yenye Rais mmoja atakayesaidiwa na mawaziri wakuu wawili wenye hadhi sawa, mmoja kutoka Tanzania Bara na mwingine kutoka Zanzibar, imefahamika.
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, ameliambia Raia Mwema kuwa pamoja na kwamba sera ya sasa ya chama chake ni kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali mbili, lakini yeye binafsi ni muumini wa Serikali moja ya Muungano, yenye Rais mmoja. Mangula, katika maoni yake hayo, anasema angependa Katiba Mpya ipendekeze muundo wa Serikali ya Muungano yenye Rais mmoja, atakayesaidiwa na mawaziri wakuu wawili au viongozi wakuu wawili kulingana na jinsi Katiba itakavyoona inafaa vyeo vyao viitwe, watakaokuwa wasimamizi wakuu wa shughuli za Serikali katika pande mbili zinazounda Muungano huo, kwa maana ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, wakimsaidia Rais wa Muungano katika maeneo yao hayo.
Kwa maoni hayo ya Mangula, ya kuwa na Serikali moja yenye mawaziri wakuu au viongozi wakuu wawili wenye hadhi sawa kutoka pande mbili hizo za Muungano, maana yake ni kwamba anapendekeza nafasi ya Mgombea Mwenza, ambaye moja kwa moja anakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, na nafasi ya Rais wa Serikali ya Mapiduzi Zanzibar, zifutwe katika muundo mpya wa uongozi wa Serikali hiyo moja ya Muungano. Msingi mkuu wa maoni yake hiyo, ni kwamba kuruhusu muundo wa Muungano wenye Serikali tatu na marais watatu katika nchi moja ya Tanzania, kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, la kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali tatu, ni sawa na kujitwisha mizigo mitatu kwa mpigo ya gharama.
Aidha, anasema kwa utaratibu wetu wa sasa wa kuwa na ukomo wa Rais wa miaka 10, kama wananchi, katika maoni yao yanayosubiriwa, watakubaliana na muundo wa Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume, baada ya miaka 30 tu ijayo, nchi itakuwa na marais wastaafu tisa, mbali na wa sasa, watakaokuwa wanahudumiwa na taifa hili. "Ilani ya CCM ni ya Serikali mbili. Mimi ni muumini wa Serikali moja na Rais mmoja mwenye kusaidiwa na mawaziri wakuu wawili au viongozi wawili kulingana na majina ya vyeo vyao yatakavyotambuliwa katika Katiba Mpya," anasema Mangula katika mawasiliano yake mwishoni mwa wiki iliyopita na mwandishi wa habari hizi na kuongeza:
"Hata ukiangalia takwimu za watu walivyotoa maoni yao kwenye Tume ya Jaji Robert Kisanga, asilimia zaidi ya 80 walipenda tuwe na Muungano wa Serikali mbili, wakifuatiwa na waliopenda tuwe na Serikali moja. Ni asilimia ndogo sana, ingawa hapa sina takwimu, waliopendekeza tuwe na Serikali tatu wakati wa Tume ya Jaji Kisanga. "Serikali tatu na marais watatu, ni mizigo mitatu kwa mpigo. Kwa utaratibu wetu wa ukomo wa Rais wa miaka 10, maana yake ni kwamba miaka 30 ijayo ya uhai wa taifa letu, tutakuwa na marais wastaafu tisa, ukiacha hawa wa sasa, ambao watakuwa wanahudumiwa na taifa hili.
"Lakini pia, izingatiwe kwamba Rais wa Tanganyika akiwa na kichwa kibovu, atajitia yeye ni ‘super Rais, na kujiona ndiye mwenye kura ya veto katika maamuzi yote ya Serikali ya Shirikisho. Wakati huo huo, wakishapitisha Serikali tatu, watu hawa watataka pia Katiba iwe na kifungu cha sheria kinachoruhusu kuundwa kwa House of Lords (Bunge la Mabwanyenye) litakalikuwa na wajumbe sawa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani."Ingawa CCM haijatoa msimamo wake hadi sasa kama chama, kuhusu pendekezo la Tume ya Jaji Warioba, la kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali tatu, lakini maoni hayo ya Mangula, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Taifa, yametafsiriwa na wachambuzi wa mambo kama mwelekeo na msimamo wa chama hicho katika Katiba Mpya ijayo.
Vigogo kadhaa wa CCM, kwa nyakati tofauti, wamekuwa wakikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini wakipinga muundo huo wa Serikali tatu kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo sababu za gharama za kuziendesha pamoja na hofu ya kuvunjika kwa Muungano wenyewe. Baadhi ya vigogo hao wa CCM, ambao wamepinga wazi wazi pendekezo hilo, ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa, Saddifa Juma Hamis, ambaye amekaririwa wakati akiwahutubia wasomi wa vyuo vikuu mkoani Kilimanjaro ambao ni wanachama wa jumuiya hiyo, akisema Serikali tatu zitakuwa mzigo kwa uchumi wa Tanzania. Wengine, wanaopinga ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hivi karibuni ilizindua rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya, ambayo pamoja na mambo mengine, imependekeza kuwa na Muungano wenye Serikali tatu. Mapendekeza hayo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali tatu, kwa kiasi fulani yamezua mjadala mkubwa miongoni mwa makundi ya kijamii, ingawa walio wengi, kwa upande wa Tanzania Bara, wanaonekana kuunga mkono pendekezo hilo, huku upande wa Zanzibar wakitaka muundo huo wa Serikali tatu utoe uhuru zaidi kwa nchi hiyo kujiamualia mambo yake yenyewe, ikiwemo kutambuliwa kama nchi huru na jumuiya za kimatifa.
Kwa mujibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, baada ya kuzinduliwa rasmi kwa rasimu hiyo ya Katiba mpya, hatua inayofuata ni kwa wananchi kutoa maoni yao kupitia mabaraza yao ya kata kwa uapande wa Tanzania Bara na mabaraza ya shehia kwa upande wa Tanzania Visiwani, juu ya mambo gani wanataka yazingatiwe katika rasimu ya mwisho ya Katiba hiyo. CCM, ambacho sera yake inaamini katika muundo wa Muungano wenye Serikali mbili, hadi sasa hakijatoa msimamo wa pamoja wa kichama baada ya Tume hiyo ya Jaji Warioba ipendekeze kuwa na Serikali tatu; ya Tanganyika, Zanzibar na Shirikisho.
Kamati Kuu ya CCM iliyokutana hivi karibuni mjini Dodoma, iliwataka wanachama wake nchi nzima kujitokeza kutoa maoni yao katika mabaraza ya kata na shehia zao, kuamua kama wanakubaliana na mapendekezo hayo ya Tume ya Jaji Warioba ya Serikali tatu au la.
Hili ni jaribio la pili kwa taifa hili la Tanzania kuingia katika mjadala mkubwa wa kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali tatu, baada ya jaribio la kwanza lililoongozwa na wabunge 55 waliopachikwa jina la G55, wakati huo wabunge wote hao wakiwa ni wa CCM, kuibuka mwaka 1993, likitaka kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika kabla ya jaribio hilo la kwanza kuzimwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kutumia hoja ya sera za chama chake, CCM, inayosisitiza muundo wa Serikali mbili; Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
- See more at: Raia Mwema - Mangula hamtaki Makamu Rais