Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
UFAFANUZI JUU YA TAARIFA YA MALALAMIKO ILIYOTOLEWA NA MTANDAO WA KIJAMII (JAMIIFORUMS) JUU YA KITUO CHA AFYA MBANDE
Tarehe 03/05/2026 JamiiForum imechapisha taarifa ya malalamiko kutoka kwa Mdau wa JamiiForums.com akitoa Wito kwa Mamlaka kufanya uchunguzi katika Kituo cha Afya Mbande kwa kuwa kuna mazingira ambayo siyo mazuri kwa Watendaji kutokana na uwepo wa Matukio ya ukiukwaji wa taratibu za fedha na Maadili ya Utumishi wa umma.
Hoja ya awali ~ Uchunguzi ufanyike Kituo cha Afya Mbande, kuna matumizi mabaya ya madaraka, uonevu, ukiukwaji wa haki za watumishi
Taarifa hiyo imekishutumu Kitengo cha malipo kufanya ujanja wa kudai mtandao unasumbua ili Wananchi walipe cash kisha baadae kuingiza kiasi cha fedha kisichokuwa na uhalisia wa kile kilichokusanywa. Taarifa hiyo imeenda mbali na kusema kuwa kuna mazingira ya uonevu kwa Watumishi ikiwemo vitisho na uhamisho usiofata taratibu za kiutumishi.
Aidha, taarifa hiyo imetaka pia uchunguzi ufanyike juu ya fedha zilizotumika kukarabati chumba cha mapumziko cha wanawake na Jengo la TB. Manispaa ya Temeke inapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
1. ΜΑΡΑΤO YA KITUO
Ukusanyaji wa Mapato Kituo cha Afya Mbande unatumia Mifumo iliyowekwa na Serikali ambao ni Centralized GotHOMIS na GePG portal. Endapo mfumo wa Centralized GotHOMIS unapoleta changamoto Wakuu wa vitengo kwa kushirikiana na HMT wa zamu pamoja na Mhasibu wa kituo wanasimamia ukusanyaji wa mapato, pindi mtandao unaporudi wakuu wavitengo (kitengo cha dawa, maabara, mionzi, meno) kwa kushirikiana na kitengo cha mapokezi wanatoa namba ya malipo (control number) kwa fedha zilizopokelewa nje ya mfumo na kwenda kuwekwa kwa wakala wa benki. Huduma kwa wateja / wagonjwa hazipaswi kusimama pindi changamoto ya mtandao inapotokea, huduma zinaendelea kama kawaida.
Kituo kwa sasa kinakusanya kati ya 98% mpaka 100.3% kwa mwezi mapato ya papo kwa papo. Halmashauri ya Manispaa ya Temeke inaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mifumo na kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya.
2. UHAMISHO WA WATUMISHI
Watumishi waliohama kuanzia Oktoba 2024 mpaka sasa kutoka Kituo cha Afya Mbande ni 8 na sio 12 kama ilivyoripotiwa, Uhamisho huu ni wa kwenda Vituo vingine vya kutolea huduma ndani ya Manispaa ya Temeke, hii ni kwa ajili ya msawazo wa Watumishi unaotokana na kuboreshwa kwa Vituo na kufunguliwa kwa vituo vipya. Uhamisho huu umegusa Wataalam ambao ni Muuguzi wa usingizi, Tabibu wa meno, Daktari, Daktari msaidizi, Mfamasia, Muuguzi, Afisa muuguzi msaidizi na Afisa tabibu.
3. UKARABATI WA MAJENGO
Maeneo yaliyofanyiwa ukarabati ni Jengo la Kifua Kikuu (TB), Kitengo cha meno, Kitengo cha Mionzi na Jengo la kutolea huduma kwa kina Mama waliopata changamoto ya mimba kuharibika (jengo hili limeunganishwa na Wodi ya akina Mama). Ukarabati ulifanyika kwa ukamilifu kama ilivyotakiwa na huduma zinaendelea kama kawaida.Picha na maelezo ya ukarabati zimeambatishwa.
Manispaa ya Temeke inatoa rai kwa umma kupuuza malalamiko hayo na kuwahakikishia itaendelea kutoa huduma bora za kitabibu na kufanya uboreshaji wa miundombinu hususani kwenye Sekta ya Afya katika Manispaa hii.