Date::10/29/2008
Manji wa Yanga sasa alazwa chumba uangalizi maalum hospitalini
Na Mwandishi Wetu
HALI ya mfadhili Mkuu wa Yanga, Yusuf Manji bado haijaimarika na sasa amepelekwa chumba cha wagonjwa mahututi, ICU, katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.
Habari ambazo Mwananchi imezipata jana jioni kutoka hospitalini hapo, zinasema kuwa hali yake ilibadilika ghafla jana mchana na uamuzi uliofikiwa na madaktari ni kumpeleka katika chumba cha uangalizi maalum.
Manji hajarejea katika hali ya kawaida, amekuwa akizungumza maneno yasiyoeleweka, lakini inawezekana ni malaria kali iliyopanda kichwani
bado hali haijatengemaa, wasiwasi umekuwa mkubwa lakini tunaimani atapata nafuu, kilisema chanzo cha habari.
Mwananchi iliwasiliana na Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega kutaka kufahamu hali ilivyo kwa mfadhili huyo, na kusema hali yake bado haijaimarika. Hata hivyo Madega hakutaka kuzungumza zaidi suala hilo.
Nimepata taarifa kuwa hali yake bado haijatengemaa, nilikwenda hospitali lakini sikuweza kumuona na nilizungumza na msaidizi wake, Sabas Kiwango mambo ya Yanga na baadaye nikaondoka hospitali
kwa kweli siwezi kulisemea zaidi, lakini hali ndiyo hiyo, alisema Madega.
Habari zaidi kutoka hospitalini hapo zinasema kuwa hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kumwangalia Manji isipokuwa watu wa karibu tu na tayari yuko katika chumba hicho cha wagonjwa mahututi.
Manji alipatwa na kilichoelezwa kuwa ni malaria kali siku moja baada ya timu yake kuichapa Simba bao 1-0, katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja Mkuu wa Tanzania. Baada ya kuugua na kuanguka ghafla, alikimbizwa Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu.
Ilielezwa kuwa Manji alipatwa maradhi hayo juzi wakati akijitayarisha kwenda kazini majira ya saa tatu asubuhi lakini ghafla alianguka. Unajua inawezekana ni furaha za ushindi na kuwa bize inawezekana kulimfanya apatwe na hali hiyo
inawezekana alikuwa na malaria ya muda mrefu na kutokana na kuwa bize na mchezo ndipo ikaibuka.
"Baada ya kufanyiwa vipimo Aga Khan aligundulika kuwa na malaria kali na uchovu, mwili ulikuwa umechoka kwa mawazo akapewa dawa na kumpumzika nyumbani, lakini baadaye majira ya saa 11 alfajiri akatoka nyumbani bila ya kueleweka akielekea maeneo ya Viwanja vya Gymkhana, lakini walinzi wake walimfuata na kumrudisha tena hospitali," alisema Madega alipozungumza na gazeti hili juzi.
Madega alisema hali ya mfadhili huyo ilikuwa inaendelea vizuri baada ya kuchomwa sindano ya kumtuliza lakini baadaye hali yake ilibadilika ghafla.
Juzi Madega aliwataka Wanayanga kutulia katika kipindi hiki ambacho mfadhili wao anasumbuliwa na maradhi na kumuombea aendelee vema na matibabu.