Date::10/13/2009
Mrithi wa Kondic atua Yanga asema anaijua Simba tangu Serbia
Kocha mpya wa Yanga, Kostadin 'Kosta' Papic, baada ya kutua Dar amedai kuwa anaifahamu Simba toka akiwa kwao Serbia.
Na Frank Sanga
KOCHA mpya wa Yanga, Kostadin 'Kosta' Papic ametua nchini na juzi usiku alitarajia kuingia mkataba akisema kwamba anajua vema kuwa kuna mechi baina ya timu yake dhidi ya Simba, Oktoba 31.
Papic, mzoefu wa soka ya Afrika ambaye alitembelea makao makuu ya klabu jana alisema hakuna mechi rahisi duaniani kwani kila mchezo katika ligi ni ngumu hivyo anaamini katika ligi kuu bara kila mechi kwake itakuwa ngumu.
"Ninajua Jumamosi tunakutana na Azam na Oktoba 31 tutacheza na Simba, mechi zote hizo kwangu ni ngumu, ukweli hakuna mechi rahisi , mimi nitaanza maandalizi ya uhakika katika mechi zote na si Simba tu."
"Kama kocha kabla hujaenda sehemu unayotaka kwenda kufundisha, lazima ujue mazingira ya huko, na kabla sijafikaTanzania ninajua kuwa kuna timu pinzani nitakutana nazo, naijua Simba tangu nikiwa Serbia na najua mfumo wa ligi ya hapa, hivyo hainipi shida," alisema.
Jana usiku, kocha huyo alitarajia kukutana na mfadhili wa klabu hiyo, Yusuph Manji na kusaini mkataba na ilitarajiwa kuwa kocha anayemaliza muda wake, Dusan Kondic angemkabidhi kila kitu.
"Kesho (leo) nitaangalia mazoezi ya timu hii asubuhi na jioni ili niweze kumjua kila mchezaji yukoje na nijue nitaanzia wapi.
"Lakini, nitaanza kibarua katika mechi na Azam na sitarajii kurejea Serbia hivi sasa hadi pale msimu wa Ligi Kuu utakapomalizika, kwani wakati nakuja huku nilikuwa najua lazima nisaini mkataba," alisema.
Papic, ambaye amewahi kufundisha Enyimba ya Nigeria na Hearts of Oak ya Ghana, zote za Afrika Magharibi kwa muda tofauti anasifika kwa kuinoa timu kucheza kwa pasi fupi, lakini ni kocha asiyependa majina makubwa katika kikosi chake.
Kocha huyo, maarufu 'Bill Clinton' kutokana na kufanana wajihi na rais wa zamani wa Marekani, wiki iliyopita alikuwa Afrika Kusini kufanya mazungumzo na timu za Moroka Swallows na Mamelodi Sundowns, lakini hawakufikia muafaka na sasa imebaki kumalizana na Yanga.
Kimaisha, alizaliwa Juni 17, 1960 mjini Novi Sad, Serbia na hutumia mfumo wa 4:4:2. Alitimuliwa na Hearts of Oak ya Ghana Juni 20, mwaka huu.
Timu nyingine ambazo amewahi kufundisha akiwa Afrika Kusini ni Maritzburg United aliyoifundisha kwa miezi sita na Kaizer Chiefs.
Alipohamia Nigeria, kocha huyo alifundisha timu nne zikiwamo Lobi Stars, Enyimba, Enugu Rangers na Kwara United kabla ya kuhamia Hearts of Oak ya Ghana alikotimuliwa Juni 20.
Iwapo atasaini mkataba na Yanga, Kosta atakuwa akilipwa mshahara wa dola 5,000 (shilingi milioni sita) kwa mwezi na kuishi makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam.
Mtangulizi wake, Kondic alikuwa analipwa dola 10,000 (sh milioni 12) kwa mwezi na muda mwingi aliishi katika hoteli ya New Africa ambako kila siku alikuwa akitumia zaidi ya Sh. 250, 000.
Kondic na msaidizi wake, Spaso Solokovisk wanamaliza mkataba wao mwezi ujao, lakini Manji hana mpango wa kuendelea nao na kuna habari kuwa hii itakuwa ni wiki ya mwisho kwa makocha hao.
Source: Gazeti la Mwananchi