Mkuu, asante sana. Nimekutana na mjadala huu muda huu. Nimpongeze mleta mada. Ukisoma kwa makini, hutaona mahali ambako nimepinga ujio wa Katiba mpya. Nilichojaribu kueleza hapa ni kwamba Kumbe yapo mambo ambayo hata kabla ya ujio huo wa Katiba mpya, tunaweza kabisa kuyafanya. Ilivyo sasa ni kama vile watu wengi wanaamini kwa katiba mpya, kila kitu kitakwenda sawa-nadharia ambayo naipinga. Katiba mpya (kama ile iliyopendekezwa na Jaji Warioba, ukiacha vipengele vichache) ni muhimu. Hoja yangu ni kwamba tusibweteke kwa kuamini kuwa kuwashughulikia hawa mafisadi au vibaka, lazima kwanza tuwe na Katiba mpya. Nadhani wakati tukielekea kwenye hiyo Katiba mpya, yapo ambayo tunaweza kabisa kuyarekebisha. Ilivyo sasa ni kama vile wengi wanaamini kufeli kwa Kikwete kulisababishwa na Katiba mpya. Dhana hiyo ina ukweli mdogo sana. Kuwa na viongozi wenye maono na wenye kuipenda nchi yao ni jambo muhimu sana.
Hadhari yangu ni kuwa wananchi wasibweteke sasa kwa kuamini kuwa mwarobaini wa kero zao zote ni Katiba mpya. Kama nilivyosema, upya wa gari pekee si jibu la kukomesha ajali. Kuwa na sheria kali pekee si mwisho wa kukomesha ubakaji na makosa mengine. Muhimu kuliko yote hapa ni kwa wananchi wenyewe kujenga utamaduni wa kuheshimu hicho kilichopo. Mfano mdogo tu, hivi kipindupindu kinaweza kumalizwa kwa Katiba mpya? Ajali zitapunguzwa kwa Katiba mpya? Hofu yangu ni kwamba tunaweza kupata Katiba mpya, lakini wananchi wengi wakawa bado wenye kuwaza na kutenda vilevile walivyotenda kwenye Katiba ya mwaka 1977. Sijapinga Katiba mpya, isipokuwa Katiba hiyo pekee si suluhisho la matatizo yetu. Matatizo ya Watanzania (baaadhi) ni zaidi ya Katiba. Tuna matatizo ya Watanzania wengi kutoipenda Tanzania. Tuanze na la kujitambua ili hiyo Katiba mpya iwe na tija.