Maonyesho ya Sabasaba kuja kivingine
Dar es Salaam. Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imejipanga kufanya mabadiliko kwenye maonyesho ya kimataifa ya biashara (Sabasaba) kwa mwaka huu ikiwa ni pamoja na kutumia vitambulisho vya washiriki kwa mfumo wa kieletroniki.
Pia, wakati wa maonyesho hayo ya 41, kutakuwa na siku ya Afrika Mashariki ambapo washiriki kutoka nchi wanachama watakutana na kubadilishana uzoefu juu ya uzalishaji bidhaa pamoja na siku ya kuonja asali ambapo washiriki wanaofanya biashara ya asali watawaonjesha wateja wao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TanTrade, Edwin Rutageruka amesema wamefanya maboresho hayo kutokana na ushindani uliopo kwenye biashara.
“Tumeamua kujipanga na yapo mambo mengi tuliyoyafanyia marekebisho. Kuanzia vitambulisho vya washiriki ambapo mfumo unaotumika ni wa kielektroniki hadi utaratibu wa watazamaji kuingia kwenye maonyesho, hakutakuwa na foleni ndefu na hata ukataji tiketi utakuwa wa haraka,” amesema Rutageruka na kuongeza.
“Tutakuwa na mikutano ya mara kwa mara kati ya wafanyabiashara, watabadilishana uzoefu na mshiriki atakayefanikiwa kumshawishi mwenzake hadi akapata mkataba wa kufanya naye biashara na atasaini makubaliano hayo mbele ya mgeni rasmi siku ya kufunga maonyesho ili ulimwengu mzima uone.”
Maonyesho ya Sabasaba kuja kivingine