Habari za mchana wana jukwaa!
Nikiri wazi tu,nimepokea kwa mashaka taarifa za watuhumiwa wanaoshtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, kuwa tayari kulipa kiasi kinachofikia shilingi bilioni 107 za kitanzania. Kusema wanaotuhumiwa kuchukua pesa na wako tayari kuzirudisha upo tayari kuwasamehe ninajiuliza maswali kadhaa;
● Je, ni wote walioshtakiwa/kukamatwa kwa hilo kosa wana hatia?
● Je, kwa wale wasio na hatia na hawana cha kulipa wao wataendelea kusota rumande mpaka lini?
WanaJukwaa, ninayaandika haya kwa sababu siku hizi kumejengeka dhana kwamba hili kosa linatumika kuwakomoa wabaya wa serikali kwa kuwapachika kosa la uhujumu uchumi ili kuwafunga midomo, kwa kuwasweka rumande kwa sababu hilo kosa halina dhamana. Na tumeona ni jinsi gani upande wa jamhuri/ upelelezi wameshindwa kuwa na ushahidi wa moja kwa moja na wa haraka dhidi ya hao wanaotuhumiwa, matokeo yake wapo waliokaa rumande yapata mwaka wa pili au wa tatu sasa. Kwa upande wangu,hilo nalo naliona haliko sawa, kwani ni wazi hawa watuhumiwa wananyimwa haki yao ya kuwa uraiani na kuungana na familia zao, na marafiki wao.
■ KWANINI HILI KOSA LA UHUJUMU UCHUMI HALINA DHAMANA?
■KWANINI TENA HIZI KESI ZA UHUJUMU UCHUMI ZINACHUKUA MUDA MREFU SANA KUSIKILIZWA NA HATIMAYE KUTOLEWA HUKUMU?
Wana jukwaa,hayo hapo juu ni maswali yanayonipasua kichwa kila nikifikiria kuhusu hizi kesi, tujiulize, ni wangapi kati ya wote waliokamatwa kwa hilo kosa wameshahukumiwa, kulinganisha na wale ambao wanaendelea kusota magerezani hapa nchini kisa tu upelelezi wa kesi dhidi yao bado haujakamilika?
Naomba nieleweke wazi, siwatetei na wala sitaki huruma ya aina yoyote kwa wote walioliibia hili taifa wakati wa tawala zilizopita, na hii taarifa ya leo kwamba wapo tayari kurudisha Tshs bilioni 107 ni njema sana kwangu. Ninachotaka nieleweke vizuri hapa ni vipi kuhusu wale waliokamatwa miaka miwili mpaka mitatu iliyopita, wanaona wameonewa kwa kupewa hizo kesi, na kesi zao zinaendelea kuahirishwa kila siku mahakamani na hawana pesa za kulipa ili tu nao wawe huru, kwa sababu ninaamini hakuna anaependa kukaa gerezani, au ni kwamba wote walioko magerezani wakituhumiwa kwa hilo kosa wana hatia?!
HITIMISHO.
Mheshimiwa Rais, umekuwa ni muumini mkubwa sana wa kutaka haki itendeke kwa raia wako, hivyo basi, kwa nafasi yako nikuombe uziamuru idara zote zinazohusika na usikilizwaji wa hizi kesi, kuanzia upelelezi mpaka mahakamani, waharakishe ili kuwasaidia wale wote wanaoshtakiwa kwa hili kosa lisilo na dhamana. Hii itasaidia sana kuondoa dhana inayoanza kujengeka kwamba hili kosa lipo kwa ajili ya kuwakomoa wanaoonekana kuwa wabaya wa serikali yako, na hivyo kuzidisha imani ya serikali yako kwa watanzania.
Wasalaam!