Na. M. M. Mwanakijiji
Niwe kwanza mletaji wa habari mbaya; hiki kinachoitwa "vita dhidi ya ufisadi" ni vita ambavyo mshindi wake anajulikana mwaka mmoja kabla, mafisadi. Niongeze katika hii habari mbaya; wale wanaojiita wanapigana vita dhidi ya ufisadi wametengeneza mazingira ya kushindwa kwao na hivyo kuwahakikishia mafisadi ushindi rahisi na wa haraka ambao unafanana na ule ushindi wa "chee" wa kwenye mithali. Ni bora tu kama wasingejitokeza kupigana vita hii.
Leo naomba nisiwazungumzie mafisadi moja kwa moja bali wale ambao wanaongoza mapambano dhidi ya ufisadi nchini na maoni yangu ya jumla kuhusu vita hivi na kwanini ninaamini kuwa kama hawatafanya mabadiliko ya haraka ni bora wakae pembeni.
Vita siyo mchezo wa kuigiza na wala si mchezo wa kufuatana mgongoni kama wale wachezao mduara. Anayeingia kwenye vita akifikiria ameingia kwenye mchezo wa "tiari bado" ili kuona ni nani "wa mwisho" ili akamatwe basi hafai vitani. Hakuna mtu wa hatari wakati wa mapambano vitani kama askari ambaye anafanya mzaha kwenye uwanja wa vita. Askari ambaye hajui uzito wa vita anayopigana au kujua uwezo wa adui hafai kunyanyua silaha yake.
Wakati masuala ya EPA yameibuka na kikosi kazi cha kina Mwanyika kilipoanza kazi yake ilisemwa kwamba mafisadi "wameiteka nchi". Mwanzoni nilichukulia kwa kejeli maneno hayo nikiamini ni msemo tu wa kuelezea ugumu wa kazi iliyopo mbele yao. Karibu mwaka mmoja baadaye na baada ya mimi mwenyewe kufuatilia masuala mbalimbali ambayo yameripotiwa katika ripoti ya kwanza ya Meremeta nimefikia hitimisho kuwa kwamba "wameiteka nchi" haielezei kwa haki kile ambacho mafisadi wamekifanya kwa nchi yetu.
Na hata ulipokuja ugumu wa kuwashtaki wahusika wa Kagoda kuwa ikifanywa hivyo kwa pupa basi "nchi italipuka" nako kunaelezea kwa kiasi tu uzito wa hii vita. Sasa ninaelewa vizuri zaidi kina, upana, uzito, urefu, na kimo cha vita hii. Hii SIYO vita ya watoto kurushiana matope; hii si vita ya watu kugombania ng'ombe au majirani kugombania kuku.
Hii ni vita inayohusu Uhuru wetu. Kilichoko hatarini siyo utajiri wao na tunachogombania siyo kugawana umaskini wetu; ndugu zangu vita hii ni vita ya kuhakikisha tunakuwa huru kutumia nafasi zote halali na za haki kujitengenezea utajiri kila mtu kwa uwezo wake. Ni vita ya kugombania uhuru wetu ambao sasa uko mikononi mwa mafisadi. Siyo tu wameiteka nchi bali mafisadi sasa wanatumiliki; na ushindi wao mwaka 2010 ni kugongelea muhuri tu katika hati ya umiliki wao.
Hiki ndicho kiini cha vita hii; asiyeelewa hili aweke silaha zake chini ajisalimishe kwa adui au arudi nyumbani kulima kama watamuachia arudi. Vinginevyo, kama wale wanaojiita, kujiona au kudhaniwa kuwa ni wa "wapambanaji" wana lengo lolote lile la kushinda vita hii basi wanahitaji kuyapanga majeshi yao upya, kupima uwezo wao, kufikiria mbinu mpya na hatimaye kupigana siyo kupigana ili kutoka sare, wala siyo kupigana ili kutokushindwa; bali kupigana ili KUSHINDA, kwani gharama ya kushindwa ni kukubali kwa taifa zima siyo tu kumilikiwa na mafisadi kama ilivyo sasa bali kuzungushiwa wigo kama wa zizi la mbuzi tukijidhania kuwa tuko huru.
Ndugu zangu, uhuru wa mbuzi ni uhuru kwa kadiri ya kwamba chui hajaamua yupi wa kumla na ni uhuru unaotegemea njaa ya chui. Ukimuona mbuzi anakula majani njiani, na kuacha "karanga" zake barabarani huku akilia "mee mee" usimshangilie kwa kudhania yuko huru.
Bahati mbaya hata hivyo, kwa mwendo wa sasa wa wapiganaji wetu na nikiangalia mwelekeo wa harakati za mabadiliko nashawishika kuamini kuwa vita hii ni vita ya maneno na siyo ya yenye mkakatiwa ushindi. Ni vita ya mbele ya vyombo vya habari na kwenye majukwaa ya siasa. Ni vita ya wanaharakati kulalamika kuwa "mafisadi wanataka kutunyang'anya majimbo" na kuwa "mafisadi wanamwaga fedha kwenye majimbo yetu". Sisikii kauli za wapiganaji wenye fikra za ushindi.
Ni kwa sababu hiyo naomba niendelee kuwa mletaji wa habari mbaya kwenu. Mafisadi watashinda 2010. Watashinda si kwa sababu wana ujumbe wa uadilifu au wanakubalika zaidi na wananchi, watashinda kwa sababu kwa mtazamo wao vita hii inahusu maisha yao. Wao wanajua vizuri kabisa kuwa endapo watashindwa 2010 hatima yao ni pingu kwenye mikono yao na kuburuzwa kuishia keko; siyo kwa makosa ya kitoto walioshtakiwa kina Mramba, Yona, Mgonja na Liyumba bali kwa makosa makubwa na ya kutisha dhidi ya Jamhuri yetu.
Wanajua wakishindwa 2010 mwisho wao ni Keko au Segerea huku ufunguo wa selo zao ukitupwa katika kichaka cha usahaulifu. Ni kwa sababu hiyo wamejiandaa kushinda na kushinda kwa kishindo cha kutufanya wote wenye kimbelembele cha "ufisadi, ufisadi" kuinamisha vichwa vyetu kwa haya na kurudisha sime zetu alani na kutembea kwa kuchechema kama wafalme walionyang'anywa mataji yao vitani.
Kwanini naamini bila ya mabadiliko ya haraka kwa wapiganaji mafisadi watashinda?
- Mafisadi wana vipaji. Mojawapo ya mambo ambayo nimegundua katika muda huu wa miaka mitatu ya kufuatilia suala hili ninaweza kusema kwa uhakika mkubwa kabisa kuwa wale watu tunaowataja kuwa ni wanahusika na ufisadi na wale ambao majina yao hatujaanza kuyataja kwa wana vipaji vikubwa vya ushawishi na uwezo wa ajabu wa kufanikisha malengo yao.
Ninapozungumzia vipaji sizungumzii karama zao wenyewe tu bali nazungumzia mkusanyiko wa watu wanaowakubali, kuwaamini na kuwaitikia kila wanapoita. Ni kwa sababu hiyo wamejipanga katika nafasi mbalimbali za serikali, vyombo vya usalama, vyombo vya habari, taasisi za kidini na kama vinyonga vikaragosi vyao vinapita katikati yetu na kujionesha kwa rangi ya upambanaji. Ugumu wake ni kujua yupi ni kinyonga na yupi ni mpambanaji wa kweli. Si wote wapigao kelele za "vita ya ufisadi" ni wapiganaji wa vita hivyo; wengine wanalazimishwa na wake zao!
- Mafisadi wana raslimali: Katika hili wala kusiwe na utata; mafisadi wamekusanya raslimali zao na wakiunganisha na vipaji vyao kikomo chao ni mbingu tu. Kimsingi wanachofanya kama mtu mmoja alivyoangaliza siku chache zilizopita ni kuwa wanatumia utajiri waliounyonya toka migongoni mwetu kuhakikisha tunabakia chini ya miguu yao. Yaani, wamepanga kutukaanga kwa mafuta yetu wenyewe huku sisi wenyewe tukichekelea chekelea.
- Mafisadi hawaogopi vyombo vya sheria au usalama. Hili linaweza lisiwe dhahiri kwa mtu mwingine lakini kwa mtu yeyote ambaye amefuatilia suala la ufisadi tangu kuanza kwake kwa mtindo wa kuuza raslimali zetu wakati wa Loliondo hadi leo Meremeta mafisadi wamejifunza kujiamini kiasi kwamba sheria zinazotufunga sisi wengine wao wamejipa udhuru.
Asikudanganye mwanasiasa yoyote, mafisadi, makuwadi wao, vikaragosi na wapambe wao hawamuogopi Mwema wala shemeji yake Mwema; hawamuogopi Othmani wala Feleshi na kwa hakika hawana hofu ya kitu kinachoitwa "utawala wa sheria". Katika fikra zao wao NDIO sheria. Walitengeneza mfumo huo wa wao kuwa juu ya sheria tangu walipoanza kuvunja vunja sheria zetu mwaka 1995, 1996, 1997, 1998, 1999, na 2000. Kuanzia 2000 ilikuwa ni wakati wa mavuno. Mafisadi wamezuiliwa kidogo tu kati ya 2005 na sasa lakini wameshajifunza somo moja hawawezi tena kukaa nje ya madaraka ifikapo 2010.
- Mafisadi hawamuogopi Rais Kikwete. Kuna watu wanafikiri kuwa Kikwete ni tishio la mafisadi nchini; kwamba kwa namna moja au nyingine mafisadi wanatetemeka mbele yake. Naomba niendelee kuwa mjumbe wa habari mbaya kwenu; mafisadi hawamuogopi Kikwete, cheo chake wala jina lake.
Laiti wangekuwa na chembe ya woga wasingethubutu au kuwa na ujasiri wa kuendelea kutenda wayatendayo. Wakiangalia mashtaka mbalimbali dhidi ya wenzao wanajua kwa uhakika kuwa hakuna jambo lolote ambalo linaweza kuwakuta ambalo ni kali kuliko haya mengine.
Na hii ndiyo sababu hadi hivi sasa kwenye suala la Richmond kwa mfano, hadi hivi sasa hakuna hata mmoja wao aliyesimama na kusema "tulifanya makosa" na kukubali kuwajibika. Ninashangazwa na jinsi gani Richmond inaonekana kama vile ililetwa na mizimu kwani hakuna mtu ambaye anakubali moja kwa moja kuhusika. Kikwete anakana, Rostam hawajui, Lowassa ndio kabisa.
Sasa imebakia kutoa matamko kwenye vyombo vya habari. Inapofikia Ikulu wanajiuma uma maneno kuwachukulia hatua wahusika wa Richmond na Kagoda ujue mafisadi hawana hofu.
Hata hivyo siyo yale tu ambayo wanafanya mafisadi ndiyo yatawahakikishia ushindi 2010. Ninaamini na ndio sababu pia ya kuandika hili kuwa yale wayafanyayo wapambanaji ndiyo yanawatengenezea ushindi mafisadi na makuwadi wao. Miongoni mwa mambo ambayo wapambanaji wanayafanya na ambayo hayamfai mpiganaji yeyote vitani ni haya:
- Wamegawanyika: Hivi sasa ukiangalia kwa karibu utaona kuna makundi ya wapambanaji. Wapo walioko ndani ya CCM na wapo walioko kwenye upinzani. Kwenye CCM wapo watu kama kina Ole Sendeka, Mpendazoe, Kilango, Mwakyembe n.k na kwa upande wa upinzani wapo kina Dr. Slaa, Zitto, Ahmed Rashid n.k Ukiangalia kwa karibu utafikiri kuwa wote wanapigana vita moja.
Bahati mbaya kama ilivyoonekana Busanda wapiganaji hawa wanasema wanapigana vita ile ile na adui yule yule lakini wao wenyewe wanapigana vile vile. Haya ni maajabu vitani. Kwenye uwanja wa vita askari akigeuza silaha yake na kuanza kuwarushia risasi wapiganaji wenzake askari huyo ni msaliti wa vita na ni kinyume na mwelekeo wa ushindi.
Hivyo, ninapoona na kusikia wabunge wapambanaji wa upinzani wakirusha maneno dhidi ya wale wa CCM au kinyume chake nina uhakika wapiganaji wa upande wa ufisadi wanachekelea tu kwani wanajua kuwa wapiganaji dhidi yao hawajaungana (united front). Hakuna jeshi rahisi kulishinda kama jeshi lililogawanyika.
- Hawana ujumbe mmoja: Mojawapo ya vitu ambavyo vinanishangaza ni kuona jinsi gani wapiganao vita dhidi ya ufisadi walivyokosa ujumbe mmoja. Hivi ukiwauliza wanapigana vita hii wakiwa na ujumbe gani watasema nini? Kusema "kuna ufisadi" siyo ujumbe wa matumaini; kusema "mafisadi wameiteka nchi" siyo ujumbe wa faraja; kusema kuwa "tuwapinge mafisadi" haitusaidii.
Matokeo yake utaona kuwa kila mpambanaji akianza kuzungumza anazungumzia maslahi yake. Jinsi gani mafisadi hawamtakii mema, wanapanga njama za kumuangusha n.k Hadi hivi sasa Watanzania wanajua kile ambacho mafisadi wamekifanya kwa nchi yetu. Lakini Watanzania hawahitaji ujumbe wa kuwaelewa mafisadi au ubaya wake kwani hilo limeandikwa vya kutosha.
Watanzania wanataka kujua hawa wapambanaji wakipewa nafasi ya ushindi 2010 watafanya nini na mafisadi? Leo hii, wote wanaogopa kusema watakachofanya kuwashughulikia mafisadi na kurudisha uwajibikaji katika ulingo wa siasa. Wapiganaji wanahitaji ujumbe mpya wa matumaini ambao ndani yake utashughulikia mambo makubwa mawili; kwanza, utaeleza hatua za kumaliza kashfa hizi zote za kifisadi (msamaha si mojawapo) na pili, utaelezea ni jinsi gani wataleta mabadiliko ambayo hayatafungua mlango wa ufisadi mpya na hivyo kutuelekeza katika ujenzi wa taifa la kisasa.
Vinginevyo hii ni vita ambavyo mwisho wake tutagundua kuwa ina chuki za ndani, visasi, wivu, n.k na haihusiaji hata kidogo na maslahi ya taifa letu.
- Hawajaunganisha raslimali zao na vipaji: Mojawapo ya mambo ambayo ninaweza kuona tofauti kubwa kati ya kambi ya mafisadi na kambi ya wapambanaji ni kuwa wapambanajij wanategemea kudra na imani kuwa wananchi wanawaunga mkono. Wanaombea kuwa hatimaye mafisadi watashindwa. Hiyo siyo vita.
Vita ni mbinu na ni mikakati. Na unapoingia vitani usisite kuchukua mateka na ukirusha makombora yako hakikisha unalenga kwenye kuangamiza siyo kuchekelea. Kama kweli hii ni vita ya uhuru wetu basi ningetarajia wapambanaji na wenyewe wangeonesha kuwa wanaweza kupigana.
Juzi nimesoma mmoja wao akilalamika kuwa kuna vipeperushi vimeangushwa kwenye jimbo lake na mwingine alilalamika kuwa mafisadi wanapeleka misaada na fedha kwenye jimbo lake. Nikajiuliza, wao wanafanya nini kujibu mashambulizi?
Nimechoka na sauti zao za kulia lia na kulalamika kama watoto walionyang'anywa pipi. Nimeshasema hapo juu kuwa mafisadi hawafanyi utani kwani katika vita hii wao wanapigania maisha yao. Nilitarajia wapiganaji wetu na wenyewe wangeacha utani. Moto kwa moto na kombola kwa kombola. Haya mambo ya "acheni malumbano" ni mambo ya kitoto. Ni lazima mgongano wa kifikra utokee na uendelee na wapiganaji wasiombe radhi kwa kuchukua msimamo huo.
Wakifanya hivyo nao wajue kuwa watashambuliwa. Hiyo ndiyo maana ya vita. Haiwezekani wao warushe makombora halafu watarajie mashada ya maua toka kwa maadui. Mafisadi nao watarusha makombora yao na kama wale wapiganaji wa waasi kule Iraq na Afghanistani mafisadi hawafuati sheria za vita hivyo watakuja hata na mbinu chafu. Mpiganaji ambaye hajatarajia hilo au hajajiandaa kwa hilo ni bora akae pembeni kwani huko tunakokwenda siyo mishale na mikuki itatumika bali hadi makombora ya masafa marefo ya bara na bara (Inter-Continental Ballistic Missiles -ICBMs).
Nina uhakika hata mimi niliye kijijini huku sitoachiliwa makombora hayo. Bahati nzuri miye na kikosi changu tunasubiri kwa hamu kwani tayari makombora yetu ya "Patriots" (mzalendo) yako tayari kujibu mashambulizi.
Hivyo, kama hawawezi kukaa chini na kuangalia ni raslimali gani walizonazo, ni vipaji gani walivyonazo na wakajipanga kuelekea ushindi basi wajue mafisadi watauelekea ushindi kwa raha yao wenyewe.
Ninachosema ni kuwa mapambano haya yataendelea. Hata hivyo, mafisadi ndio wamejipanga vizuri zaidi wakijua wanachopigania na wakiwa tayari na ujasiri wa kufanya lolote ili kurudi madarakani 2010. Na kama mwendo utaendelea hivi hivi basi nitakuwa mtu wa mwisho kushangaa nikisikia "wapiganaji" wakianguka mwakani. Msije mkasema hamkuweza kuona hilo likija. Mmeonywa mwaka mmoja na zaidi kabla. Mafisadi wakishinda msiwalaumu; mmewatengenezea njia na kuipalilia.
Niandikie:
mwanakijiji@jamiiforums.com