zurima ramadhan
Member
- Oct 26, 2024
- 5
- 0
Na Zurima Ramadhan, Zanzibar
Wadau wa kupinga vitendo vya udhalilishaji nchini wametakiwa kuzitumia siku 16 za kupinga ukatili kwa kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Akifungua maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili katika ukumbi wa bima Mpirani wilaya ya mjini, Mjumbe wa bodi ya Tamwa Zanzibar Mwatima Issa amesema vitendo hivyo vimekuwa vikishuhudiwa kutokea siku hadi siku hivyo nguvu za pamoja zinahitajika kufikia lengo la mapambano hayo.
Soma pia: Zanzibar: Jamii yatakiwa kupinga vitendo vya ukatili, uzalilishaji na rushwa
Amesema licha juhudi zinazochukuliwa na wadau mbalimbali kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia lakini bado vinaendelea kutokea katika jamii hivyo kuelekea 2030 ni vyema kuungana na kuchukua hatua za kumaliza vitendo hivyo.
Akiwasilisha majumuisho ya takwimu za vitendo vya udhalilishaji kuanzia Januari hadi Octoba 2024 afisa mawasiliano kutoka TAMWA Zanzibar Khairat Haji amesema jumla ya matukio ya udhalilishaji 1,582 yameripotiwa huku waathirika wakiwa 1,583.
Aidha amesema idadi ya kesi 693 zilizohusisha watoto wa umri wa miaka 15 hadi 17 jambo linalowafanya watoto kuwa wahanga kila kukicha.
Mwanaharakati na msaidizi wa sheria Sabahi Bakari Hassan amesema familia nyingi zinazokumbana na vitendo hivyo huweka muhali katika kuwafikisha mahakamani watuhumiwa jambo ambalo linarudisha nyuma jitihada za kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Kwa upande Sajenti Rahma Ali Salum kutoka jeshi la polisi Zanzibar ameziasa familia zinazokubwa na vitendo vya udhalilishaji badala ya kumalizana kienyeji.
Nao baadhi ya washiriki wa maadhimisho hayo wamesema ni vyema jamii kuendelea kupatiwa elimu ya kutambua haki zao sambamba na kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji ikiwemo sehemu za michezo.
Maadimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili yamewashirikisha wadau mbali mbali wa wanaharakati, taasisi za serikali na binafsi pamoja na wanamichezo wanawake yameandaliwa na TAMWA Zanzibar kwa kushirikia na shirika la maendeleo la Ujerumani G.I.Z