SoC02 Mapambo yanayoishi na umuhimu wa Samaki wa mapambo

SoC02 Mapambo yanayoishi na umuhimu wa Samaki wa mapambo

Stories of Change - 2022 Competition

Livinus wa Bitumbe

New Member
Joined
Oct 21, 2020
Posts
4
Reaction score
6
MAPAMBO YANAYOISHI

UTANGULIZI

Katika dunia inayobadilika na uchumi unaoanza kutengamaa baada ya pigo la ugonjwa wa UVIKO-19, ni vizuri kuwaza nje ya njia za kawaida za uzalishaji mali ili kujikwamua kiuchumi. Jitihada mbalimbali zimeshauriwa na wajuzi wa mambo na katika hizo nimeona bora leo niwang’ate sikio juu ya ufugaji wa viumbe wa majini.
Ufugaji huu huusisha kuzalisha, kulea, kukuza ama kunenepesha viumbe waishio majini katika vizuizi ambavyo huweza kuwa mabwawa (njia ambayo imeenea maeneo mengi), matenki, vizimba na njia nyingine nyingi tofauti.

Karibia nusu ya viumbe wa majini wanaopatikana katika soko la dunia sasa wanatokana na ufugaji wa viumbe hao katika mazingira tofauti na yale ya asili yake.
Ukiacha viumbe kama kaa, jongoo bahari, sato, kambale na uduvi ambao hufugwa kwa malengo ya chakula, kuna sehemu ya ufugaji huu ambayo bado haijawa maarufu sana. Sehemu hiyo inahusisha ufugaji wa samaki wa mapambo (mapambo yenye uhai). Samaki hawa hupatikana katika maji chumvi na maji baridi. Asili ya samaki hawa ni maeneo ya matumbawe katika bahari na sehemu zenye miamba na mapango ya kujificha katika maziwa, mito hata mitalo ya maji tiririka mitaani tunakopita !

SAMAKI WA MAPAMBO

Samaki wa mapambo huwa wadogo kwa umbo, wenye rangi nzuri za kuvutia, maumbile yakushibisha macho, tabia ama jinsi ya kuogelea inayostaajabisha sana. Samaki hawa huitwa majina mara nyingi wakifutishwa na viumbe wa nchi kavu wenye muonekano kama wao kama samaki pundamilia (mwenye michirizi mithili ya pundamilia) na samaki kasuku (mwenye umbile la mdomo mithili ya kasuku). Kadhalika, samaki hawa hupewa majina kufuatia rangi zao mfano samaki dhahabu. Ukiacha ukweli kwamba sio eneo la ufugaji ambalo limepewa kipaumbele nchini Tanzania, ni wazi hata sera na sheria za nchi zimeligeuzia mgongo. Hii inajidhihirisha wazi maana hata katika sheria ya uvuvi ya mwaka 2003, samaki hawa wa mapambo wametajwa mara moja tu tena kama mfano na sio kwa kuelezewa hasa!

Screenshot_20220719-123710_Google.jpg

Samaki pundamilia (Zebrafish Kwa hisani ya Google)

Hata hivyo nchi yetu ina rasilimali za samaki hawa wa kuvutia tofauti tofauti katika matumbawe yake. Vilevile maziwa kama Tanganyika na Nyasa yamesheheni viumbe hawa wanaokuthibitishia fahari ya macho. Sayansi imeeleza sababu kadha wa kadha kuhusu umuhimu wa kuwaweka samaki hawa majumbani, maofosini na hata maeneo ya viwanja vya ndege.

Screenshot_20220719-123747_Google.jpg

Samaki dhahabu (goldfish kwa hisani ya Google)

Samaki hawa wanaweza kufugwa katika mabwawa ya kawaida japo madogo, na matenki. Ingawa wanaweza kula vyakula tofauti katika mazingira kama mwani pamoja na ubongo wa wanyama kama ng’ombe na kondoo, soko lina chakula mahususi kinacho wapa muonekano mzuri zaidi kwa rangi zilizokoza.

UMUHIMU WA SAMAKI WA MAPAMBO

Imethibitishwa kuwa wanaweza kupunguza ukali wa magonjwa kama presha, wanaweza ongeza uwezo wa umakini kwa watoto wasiotulia, wanasaidia katika kuimarisha uwezo wa kumbukumbu, na wanaweza ongeza uwezo wa kustahimili kusubiri huduma katika ofisi za umma na binafsi kama watawekwa maeneo wateja wanapoketi kuzisubiri huduma huduma hizo.

Ukiachilia mbali umuhimu wake kisayansi, kibiashara samaki hawa wana soko kubwa la kimataifa na wanauwezo wa kuingiza kipato kikubwa kushinda hata samaki wanaofugwa kwa matumizi ya chakula. Wafanyabiashara wa samaki wa mapambo huuza rejareja ama kwa jumla kulingana na mahitaji na upatikanaji wa wateja. Gharama zinatofautiana kulingana na aina ya samaki lakini mara nyingi huuzwa juu sana na huleta faida kubwa. Samaki aina ya ‘gold fish’, kwa mfano, wakiuzwa wawili katika uwiano wa wakiume na jike huweza kugharimu mpaka shilingi elfu arobaini pesa ya kitanzania.

Ukiacha umuhimu wa samaki hawa katika kuuzwa pia biashara ya maboma ya vioo ambamo hawa samaki huwekwa kwa ajili ya kupambwa (‘aquarium’) ni sehemu muhimu sana katika mnyororo wa thamani wa samaki hawa. Yapo maeneo machache nchini ambayo huifanya biashara hii masoko mengi yakiwa Dar es Salaam. Ukiacha soko la nje sehemu tofauti katika mashirika wameanza utamaduni wa kuweka maboma haya ya vioo kama sehemu ya mapambo ambamo ndani yake huwekwa samaki hawa wa kuvutia hivyo kuongeza wigo wa soko la biashara ya samaki wa mapambo.

0cfa7d77-dc23-4c1e-990e-892ec0378342.jpeg


Boma la vioo ‘Aquarium’ (Kwa hisani ya Google)

HITIMISHO
Pamoja na umuhimu huu, ni wazi nchi haijafumbua macho na watu hawaja ‘shitukia mchongo’ na sehemu chache zinazojua kuhusu umuhimu wa ufugaji wa samaki hawa hazisemi kulinda faida yao. Zipo sababu za msingi kama nlivyoziainisha hapo juu ambazo ni vyema tuzizingatie kama wadau wa maendeleo lakini pia kama serikali katika kufufua uchumi uliodidimizwa na janga la UVIKO-19 ambalo kidogo linafifia na dunia inafunguka.

Wachache wengine ambao hawafugi huwavua samaki hawa wa mapambo na kuwasafirisha kwa faida kubwa kuelekea soko la dunia ambalo halijaweka mfumo sahihi wa utambuzi wa mahala asilia samaki hawa walipotoka. Hawa hufaidika kwa sababu hawalipi kodi na mara nyingi wadau hawa huwapitisha kwa magendo kuelekea nchi jirani ambayo ‘huwabrand’ na kuwauza kama samaki watokao nchini hapo. Haya hutokea kwa sababu ni rasilimali ambayo haijawekewa mkazo wa aina yeyote.

Wachache hawa wanaofaidika na samaki hawa bado huharibu rasilimali asilia hasa kwa sababu hutumia sumu ‘cyanide’ katika kuwalewesha hawa samaki kwa sababu ya asili yao ya kujificha katika miamba. Utaratibu huu haramu huchangia kuua viumbe wengi wanaoishi katika maeneo sumu hii inapomiminwa. Hilo pia ni eneo muhimu sana la kulitilia maanani kama tunalenga kufaidika na rasilimali hii hadhimu ya mapambo yanayoishishi.

Nawaita wadau wa uvuvi, serikali na wizara husika, vyombo vya tafiti za uvuvi katika maji chumvi na maji baridi walitizame suala hili kwa undani na wabuni mbinu zitakazo lifaidisha taifa na watu wake kupitia rasilimali iliyopo, yenye uwezo wa kukuza kipato ambayo hata hivyo bado haijapewa kipaumbele.
 
Upvote 8
Nimekupigia kura naomba na mimi unipigie kura kwenye langu la "Uuzaji na usambazaji wa samaki kuipitia app maalumu ya Samaki kiganjani mwako '
 
Back
Top Bottom