Ripoti kuhusu ufanisi wa mradi wa reli mpya ya kisasa ya SGR nchini Kenya kwa mwaka uliopita, imetolewa rasmi na ofisi ya takwimu ya kitaifa ya Kenya (KNBS). Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wasafiri milioni 1.99 walitumia reli hii mpya mwaka wa 2021, na kuleta mapato ya shilingi bilioni 2.2 sawa na dola milioni 19.2 za kimarekani. Hii ni ongezeko kutoka pato la dola milioni 8 mwaka wa 2020, ambako ni wasafiri 811,522 pekee waliotumia reli ya SGR.
Ikumbukwe kuwa mnamo mwaka wa 2020, Kenya ilipitia wakati mgumu kutokana na janga la UVIKO-19 lililosababisha takriban sekta zote za uchumi kufungwa, na masharti makali kuwekwa ili kudhibiti virusi hivyo.
Ufanisi wa usafiri kwa reli mpya ya kisasa mnamo mwaka wa 2021 ulitokana na serikali ya kitaifa kulegeza masharti makali ya kudhibiti virusi vya Corona, kando na sekta mbalimbali za uchumi kufunguliwa tena. Bwana Philip Mainga, meneja mkuu wa shirika la reli la Kenya anasema ufanisi huu ni ishara nzuri kuwa Wakenya wanafurahia mradi wa reli ya SGR.
‘Kwa miaka mitatu mfululizo, kuanzia mwaka wa 2019, SGR imekuwa ikiandikisha faida. Licha ya kuwa mwaka wa 2020 shirika la reli la Kenya liliathirika sana na janga la Corona, tulipata faida. Tunashukuru sana Wakenya wote ambao hutumia huduma zetu za usafiri. Mwaka huu, tunatarajia kupata faida zaidi ikilinganishwa na ile ya mwaka jana,’ anasema Mainga.
Kulingana na ripoti ya KNBS, idadi kubwa ya wasafiri waliotaka kutumia huduma za SGR mwezi Desemba mwaka wa uliopita, ililazimu shirika la reli nchini Kenya kuongeza idadi ya mabehewa ya abiria kati ya Nairobi na Mombasa. Sekta za utalii na hoteli haswa katika eneo la Pwani vile vile zilipigwa jeki kutoka na kuongezeka kwa idadi ya abiria.
Kwa upande mwingine, usafirishaji wa mizigo pia ulipigwa jeki baada ya kuondolewa kwa masharti yaliyokuwa yamewekwa ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona. Ofisi ya takwimu za kitaifa ya Kenya (KNBS) inaonyesha kuwa zaidi ya tani milioni 5.4 za mizigo zilisafirishwa mwaka wa 2021, na kuletea shirika la reli la Kenya dola milioni 115. Hili ni ongezeko kutoka mwaka wa 2020 ambapo KNBS iliripoti kuwa SGR ilisafirisha tani milioni 4.4 za mizigo na kuletea shirika la reli dola milioni 108. Aidha, shirika hilo limesema kwamba ukuaji huo umechangiwa na kupanuka kwa masoko katika mataifa ya Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na DRC ambayo yamekuwa yakitumia huduma za SGR.
Reli hiyo iliyotengenezwa kupitia ufadhili wa shilingi bilioni 3.2 kutoka kwa serikali ya China, ndio mradi mkubwa wa miundo msingi kuwahi kutekelezwa na serikali tangu Kenya kujipatia uhuru wake. Mradi huo wa reli kutoka Mombasa hadi Nairobi ulichukua miaka mitatu na nusu kukamilika, huku wataalam wakitumia teknolojia ya ujenzi wa reli ya China kuukamilisha.
Wakenya wengi na wageni kutoka mataifa ya nje wanaotembelea Kenya wanapenda kutumia reli ya kisasa kwa sababu ya muda mchache wa safari kati ya Nairobi na Mombasa. Kwa kutumia basi, abiria wangetumia saa tisa kusafiri kutoka Nairobi hadi Mombasa, ila sasa ni saa nne na nusu kwa kutumia reli ya SGR.
Aidha, ikumbukwe kuwa sasa kuna madereva wazawa wa Kenya ambao wamepata mafunzo kutoka kwa Wachina na wana uwezo wa kuendesha treni za kisasa.