Mwanamwana
Platinum Member
- Aug 1, 2011
- 9,604
- 22,722
Wananchi wa Jimbo la Mwibara, lililopo mkoani Mara, wamemwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), awasikilize kilio chao kwa kuwapatia mgombea mpya katika uchaguzi ujao, wakieleza kutoridhishwa na utendaji wa viongozi waliopita akiwemo mbunge wa sasa.
Katika video iliyosambaa mitandaoni, wananchi hao wamesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Samia kuboresha maisha ya Watanzania, jimbo lao limeendelea kukumbwa na changamoto nyingi za maendeleo kutokana na ahadi kutotekelezwa na mbunge wao wa sasa Charles Kajege anayemaliza muda wake.
Wamesema ahadi nyingi walizopewa na viongozi hao hazijatekelezwa huku wakiwa wamesubiri kwa muda mrefu bila mafanikio, hali iliyowakatisha tamaa. Aidha, wamedai kuwa hata baadhi ya wabunge waliopita hawakuweza kuwasaidia kubadili maisha yao kiuchumi wala kijamii.
"Tunampongeza sana Mama Samia kwa kazi kubwa anayofanya nchi nzima, lakini huku Mwibara bado hatujaona matokeo ya maendeleo hayo. Tunaomba atusikie na kutuletea mtu mwingine ambaye atatusaidia kufikia maendeleo tunayoyahitaji," alisema mmoja wa wananchi hao.
Wananchi hao pia wameeleza kuchoshwa na vita vya kisiasa vinavyoendelea ndani ya jimbo hilo, wakisema kuwa wanahitaji kiongozi mwenye nia ya dhati ya kuwatumikia badala ya kupigania madaraka.
Mpaka sasa mbunge wa sasa Charles Kajege hajazungumza lolote kuhusu malalamiko hayo ya wananchi wake.
Chanzo: JamboTv