Urafiki unakuwa na "hatua", zinazoanza tangu siku mnakutana hadi mnafika wakati kila mmoja wenu anahisi moyoni kuwa "huyu ni rafiki yangu wa kweli". Tusichanganye baina ya watu tunaowajua kwa sababu ni majirani, tunafanyakazi nao pamoja, tunakutana nao vilabuni, mikutanoni, mitaani na marafiki wa kweli. Wote hawa mnakutana, mnaulizana, na wote wana umuhimu wao ingawa hatuchangiani nao kila kitu. Ikifika hatua ya kuchangiana naye mambo muhimu kwa mfano anakuwepo wakati unamhitaji japo kwa mawazo au kukusikiliza, anakusaidia unamsaidia, anakuliwaza unamliwaza bila ya kudai kurejeshewa fadhila, huyu ndie rafiki wa kweli. Kwa rafiki wa kweli hakuna "commitment" wala makubaliano, bali ushindani wa kutendeana mema.
Inaemekana, rafiki wa kweli anakuwa kama kioo chako. Unajiangalia na unajirekebisha ufane naye, na yeye ndio hivyo hivyo. Ndio mana katika kundi la wahuni si rahisi kumkuta asiyekuwa mhuni, na kama yumo, anajifunza kuwa kama wao kwani ndivyo anavyotaka awe.
Pamoja na yote, urafiki kama mapenzi vinabaki kuwa vitu vya mjadala kwani ni mahusiano baina ya mtu na mtu.