Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Oktoba 29, 2026, Idara ya Sheria ya Marekani (DOJ) ilisema uchunguzi huo, uliopewa jina la Operation Ghostbusters, umebaini udanganyifu unaokadiriwa kuzidi dola milioni 200, sawa na takribani KSh25.9 bilioni.
Kwa mujibu wa wachunguzi, washukiwa walitumia taarifa binafsi za raia wa Marekani kufungua akaunti bandia kupitia mfumo wa Federal Student Aid (FAFSA), kisha kuwasajili watu hao katika vyuo bila wao kujua.
Baada ya vyuo kupokea maombi hayo, fedha za mikopo na misaada ya masomo zilitolewa, huku sehemu ya fedha zilizobaki baada ya kulipia ada zikielekezwa kwenye akaunti za benki zilizodhibitiwa na washukiwa nchini Marekani na Kenya.
Katika baadhi ya visa, wahusika wanadaiwa kutumia teknolojia ya akili unde (AI) kukamilisha kazi za masomo ili kufanya ionekane kwamba wanafunzi hao walikuwa wakiendelea kuhudhuria masomo na hivyo kuendelea kupokea fedha.
DOJ imetangaza mashtaka dhidi ya watu watano katika kesi zinazohusiana na mtandao huo katika majimbo ya Nebraska, Virginia na New Jersey.
Miongoni mwa washukiwa ni Mkenya Francis Mogambi, anayekabiliwa na mashtaka 10 yanayohusiana na wizi wa fedha za serikali na matumizi ya utambulisho ulioibwa.
Wachunguzi wanadai kuwa Mogambi alikuwa akibakisha asilimia 30 ya fedha alizopata na kutuma kiasi kilichobaki kwa washirika wake nchini Kenya.
Katika kesi nyingine, washukiwa watatu wa New Jersey wanadaiwa kutuma fedha kwa washirika walioko Kenya wanaohusishwa na kampuni inayodaiwa kufanya biashara ya safari za utalii.
Uchunguzi huo pia umebaini akaunti 830,840 zinazoshukiwa kuwa za udanganyifu, zikiwa zinahusishwa na karibu dola milioni 130 za msaada wa elimu.
Aidha, mamlaka za Marekani zimekamata zaidi ya dola 750,000, sawa na takribani KSh97 milioni, katika sarafu za kidijitali zinazohusishwa na raia wa Kenya.
Hata hivyo, kiasi cha zaidi ya KSh25 bilioni ni makadirio ya ukubwa wa ulaghai unaochunguzwa, wala si fedha zote zilizothibitishwa kuibwa na washukiwa hao watano. FBI imesema imebaini hasara zinazozidi dola milioni 32 katika miradi kama hiyo.
Marekani imesema inashirikiana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya (DCI), Mamlaka ya Kurejesha Mali (ARA) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kufuatilia fedha hizo na washukiwa wengine.
Kwa sasa, uchunguzi unahusisha zaidi ya kesi 40 katika ofisi 26 za FBI nchini Marekani, huku washukiwa wote wakichukuliwa kuwa hawana hatia hadi itakapothibitishwa vinginevyo mahakamani.